Emmanuel Elibarik, maarufu Nay wa Mitego.
MSANII wa muziki wa kizazi kipya, Emmanuel Elibarik, maarufu Nay wa Mitego, jana alikamatwa mkoani Morogoro na Jeshi la Polisi na kusafirishwa kwenda Dar es Salaam ambako anashikiliwa katika Mkoa wa Kipolisi wa Ilala.
Taarifa za kukamatwa kwa msanii huyo zilisambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii jana asubuhi baada ya Nay kutangaza kuwa kutiwa kwake mbaroni baada ya 'show' mjini Morogoro.
"Nimekamatwa kweli. Muda huu nikiwa hotel Morogoro baada ya kumaliza kazi yangu iliyonileta. Napelekwa Mvomero Polisi. Nawapenda Watanzania wote," aliandika Nay katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Ulrich Matei, aliiambia Nipashe jana kuwa walimkamata msanii huyo kutokana na maagizo waliyopewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Ilala na kutakiwa kumsafirisha kwenda jijini Dar es Salaam.
"Sisi tuliambiwa tukamatieni mtuletee," Kamanda Matei aliiambia Nipashe. "Tumemkamata na kumpeleka tayari yupo Dar."
Kamanda Matei alisema shauri la Nay wa Mitego lipo jijini Dar es Salaam, katika mkoa wa kipolisi wa Ilala ambako ndiko namba ya upelelezi wa shauri ilionyesha limetoka.
Alipoulizwa sababu za kumkamata na lini Polisi inatarajia kumfikisha mahakamani, Kamanda wa Polisi wa Ilala, Salum Hamduni alisema kwa njia ya simu kuwa yupo likizo hivyo "siko ofisini", na kutaka Nipashe iwasiliane na Kaimu Kamanda.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Ilala, ambaye pia ni Kamanda wa Operesheni Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya alisema hawezi kufahamu siku ambayo Nay atafikishwa mahakamani kwa kuwa ndiyo kwanza alikuwa amewasili jijini akitoka safarini.
"Hata mimi sina taarifa kwa kuwa katika siku mbili tatu hizi sikuwapo ofisini."
Hata hivyo, Kamanda Mkondya alithibitisha kufahamu kushikiliwa kwa Nay.
Kushikiliwa kwa Nay wa Mitego kumetokea ikiwa ni muda mfupi baada ya msanii huyo kutoa wimbo mpya unaofahamika kwa jina la 'Wapo'.
Katika mashairi ya wimbo huo, msanii huyo anataja kuwapo kwa kiongozi ambaye ameghushi vyeti, tuhuma ambazo zinaonekana kuunga mkono madai ya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephath Gwajima kuwa Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameghushi vyeti.
Askofu Gwajima alianza kuanika anachodai ni historia sahihi ya Makonda baada ya mkuu wa mkoa huyo kumtaja kuhusika na biashara ya madawa ya kulevya mwanzoni mwa mwezi uliopita.
Askofu Gwajima alikaa mahabusu kwa siku tatu tangu hapo, kupimwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kama anatumia dawa za kulevya, kupekuliwa, kuachia kabla ya kupekuliwa tena kwa tuhuma hizo hizo nyumbani kwake mwishoni mwa wiki iliyopita.
Hii ni mara ya kwanza Nay wa Mitego kutiwa mbaroni na polisi tangu alipopata mafanikio kimuziki, na ya nane katika maisha yake. Mwaka jana, Nay wa Mitego, katika mahojiano na Nipashe, alikiri kijihusisha na matukio ya kihalifu yakiwamo ya wizi kabla hajafanikiwa kimuziki na kubainisha kuwa ameshatubu kwa Mungu na anaamini ameshasamehewa makosa yake hayo.
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / kitaifa /
michezo /
slider
/ BAADA YA MSANII NEY WA MITEGO KUKAMATWA MORO, SASA ASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI DAR,
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment