BILIONEA BILL GATES AMBURUZA RAIS WA MAREKANI DONALD TRUMP
Mwanzilishi wa Microsoft Bill Gates kwa mara nyingine anaongoza orodha ya jarida la Forbes ya watu tajiri zaidi duniani mwaka huu.
Idadi ya mabilionea (wa dola) duniani imeongezeka kwa asilimia 13 na kufikia 2, 043.
Kwa mujibu wa jarida hilo, mali ya Bw Gates imeongezeka hadi $86bn, kutoka $75bn.
Anafuatwa na Warren Buffett, aliyeongeza utajiri wake kwa $14.8bn hadi $75.6bn.
Rais wa Marekani Donald Trump, hata hivyoa meshuka nafasi 220 hadi 544 kwenye orodha hiyo ya matajiri na sasa ana mali ya $3.5bn pekee.
Forbes wamesema kushuka kwa utajiri wa Bw Trump kwa $1bn kulitokana na kuupungua kwa kasi ya sekta ya biashara ya ardhi na makao Marekani.
Katika orodha hiyo ya Forbes, mabilionea 183 walijipatia utajiri wao kupitia teknolojia, utajiri wao ukiwa jumla ya dola trilioni moja za Marekani.
Orodha hiyo imetawaliwa na mabilionea kutoka Marekani.
Wengine walio kwenye 10 matajiri zaidi ni mwanzilishi wa Amazon Jeff Bezos, ambaye amepanda hadi nambari tatu utajiri wake ukiongezeka kwa kiwango cha juu zaidi kuliko wa mtu mwingine yeyote duniani.
Utajiri wake uliongezeka kwa $27.6bn hadi $72.8bn.
Mwanzilishi wa Facebook Mark Zuckerberg yupo nafasi ya tano na mwanzilishi mwenza wa Oracle Larry Ellison alikuwa nambari saba.
Idadi ya mabilionea duniani ambao sasa wanafikia 2,043, ilipata ongezeko kubwa zaidi kwa mwaka mmoja katika kipindi cha miaka 31 tangu orodha hiyo ianze kuandaliwa.
Mabilionea kutoka Marekani walikuwa 565, jambo ambalo Forbes wanasema huenda lilitokana na kuimarika kwa soko la hisa pakubwa tangu Trump aliposhinda uchaguzi Novemba 2016.
China ilikuwa ya pili kwa mabilionea ikiwa na mabilionea 319 nayo Ujerumani ya tatu na mabilionea 114.
Watu 10 matajiri zaidi:
Bill Gates (mwanzilishi mwenza wa Microsoft): $86bn
Warren Buffett (mwekezaji Mmarekani): $75.6bn
Jeff Bezos (mwanzilishi wa Amazon): $72.8bn
Amancio Ortega (mwanzilishi wa Inditex): $71.3bn
Mark Zuckerberg (mwanzilishi wa Facebook): $56bn
Carlos Slim (mfanyabiashara kutoka Mexico): $54.5bn
Larry Ellison (mwanilishi mwenza wa Oracle): $52.2bn
Charles Koch (mfanyabiashara Mmarekani): $48.3bn
David Koch (mfanyabiashara Mmarekani): $48.3bn
Michael Bloomberg (mwanzilishi wa Bloomberg): $47.5bn
Wanawake katika orodha hiyo waliongezeka hadi 227 kutoka 202, na wanamiliki jumla ya $852.8bn.
Kwa mwaka wa pili, Mfaransa Liliane Bettencourt, wa maduka ya bidhaa za urembo L'Oreal, alikuwa mwanamke tajiri zaidi duniani akiwa na mali ya $39.5bn. Alirithi biashara hiyo.
Wengi wa wanawake matajiri duniani walirithi utajiri wao, Forbes walisema.
Lakini pia wapo wafanyabiashara 15 wa kike ambao hawakurithi mali, sana kutoka Asia.
Mmoja ni Nguyen Thi Phuong Thao kutoka Vietnam anayemiliki kampuni ya safari za ndege ya VietJet.
Kuyumba kwa Trump
Forbes wanasema utajiri wa Rais wa Marekani Donald Trump ulishuka kutokana na kupungua kasi kwa ukuaji wa soko la ardhi na nyumba Manhattan, ambapo utajiri wake mwingi upo.
"Asilimia arobaini ya utajiri wa Donald Trump upo Trump Tower na katika majumba mengine manane yanayopatikana eneo la nusu kipenyo cha maili moja," Forbes walisema.
"Hivi karibuni, eneo hilo limetatizika kibiashara."
Jarida hilo pia limesema utajiri wake uliathiriwa pia na matumizi katika siasa, sana kwenye kampeni yake ya urais ambapo inakaribiwa alitumia $66m.
Aidha, alitumia $25m kumaliza kesi ambapo alishtakiwa kwa tuhuma za kuwatapeli wanafunzi kupitia Chuo Kikuu cha Trump.
Hata hivyo, Forbes wanasema thamani ya hoteli ya Mar-a-Lago jimbo la Florida ilipanda $25m kutokana na kuangaziwa sana baada ya uchaguzi.BBC
0 comments:
Post a Comment