DK SHEIN AELEZA KUWA MUUNGANO UPO IMARA HUKU KERO ZINAFUTIWA UFUMBUZI
RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema katika kipindi cha mwaka mmoja madarakani katika awamu ya pili, amepata mafanikio makubwa.
Moja ya mafanikio, Dk Shein alisema ni kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015-2020 katika miradi ya maendeleo na ustawi jami.
Dk Shein alisema hayo wakati alipofanya mazungumzo na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali nchini ikiwa ni kutimiza mwaka mmoja na kusisitiza kuwa Muungano hautavunjika na kero zake zitapatiwa ufumbuzi kwa mazungumzo.
Alisema anajivunia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha pili kutokana na kushinda katika uchaguzi wa marudio wa Machi 20, 2016 ambayo yameonesha njia ya kukua kwa uchumi na ustawi wa jamii huku sekta binafsi ikishirikishwa kikamilifu katika ujenzi wa nchi miradi mikubwa ya maendeleo.
Aliwataka wananchi kumuunga mkono katika mipango hiyo na kuwataka kuachana na ndoto za baadhi ya wanasiasa wenye uchu wa madaraka ambao wamekuwa wakipita na kuwadanganya wananchi kwamba wanasubiri kuingia madarakani.
“Ninyi waandishi wa habari wakongwe na wale wanaochipukia mnajua kwamba njia pekee ya kuwa rais katika nchi ni kushiriki katika uchaguzi.....njia nyingine ni kufanya mapinduzi ambayo hayakubaliki katika nchi za kidemokrasia,” alieleza.
Alijibu swali hilo wakati alipotakiwa kutoa ufafanuzi kama ipo mipango inafanyika chini chini ya kuwepo kwa makubaliano kati yake na Chama cha Wananchi (CUF) ikiwemo mazungumzo ya suluhu ya kisiasa.
Alisema hakuna mazungumzo ya kisiasa kati ya CCM na CUF yanayoendelea sasa, kwani anafahamu kuwa uchaguzi umekwisha na serikali halali ipo madarakani inafanya kazi kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
“Mimi simzuii mtu kusema....... anayesema anajitayarisha kuapishwa mwache aseme kwa sababu huo ni uamuzi wake na mdomo ni nyumba ya maneno, lakini asivunje sheria za nchi tu,” alisema Dk Shein.
Aliongeza kwamba mafanikio makubwa yamepatikana katika kipindi cha mwaka mmoja tu cha uongozi wake awamu ya pili ikiwemo kulipa pensheni ya jamii kwa wananchi wote waliofikia umri wa miaka 70 ikiwemo wale ambao hawajapata kuajiriwa na serikali.
Aidha, alisema serikali imefanikiwa kusimamia mapato katika vyanzo vyake mbalimbali hatua imeifanya kulipa viinua mgongo kwa wafanyakazi wastaafu wapatao 2,736 na kutumia Sh bilioni 38.
Alisema kwamba mafanikio yote hayo sasa yataiwezesha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kulipa mishahara mipya kwa wafanyakazi wake kuanzia mwezi ujao ambapo kima cha chini kitaongezeka kwa asiimia 100.
0 comments:
Post a Comment