BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

NAPE NNAUYE AONJA JOTO YA JIWE KABLA YA KUZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI NI MUDA BAADA YA KUNG'OLEWA UWAZIRI,

 
HATARI! Aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye jana alijikuta akikabiliana uso kwa uso na mtutu wa bastola wakati watu wanaodhaniwa kuwa ni askari walipokuwa wakijaribu kumzuia asizungumze na waandishi wa habari.

Nape alikumbana na mkasa huo kwenye eneo la Oysterbay, Kinondoni jijini Dar es Salaam alipofika eneo hilo kueleza msimamo wake baada ya kuondolewa katika nafasi ya uwaziri.

Awali, saa chache kabla ya tukio hilo la bastola jana, ilitolewa taarifa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ikieleza kwamba Rais John Magufuli amefanya mabadiliko madogo ya baraza lake la mawaziri kwa kumteua aliyekuwa Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe, kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, huku Prof. Palamagamba Kabudi akiteuliwa kuwa waziri mpya wa Sheria na Katiba, akichukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Mwakyembe.

Ingawa taarifa ya Ikulu haikueleza sababu za kuondolewa kwa Nape, lakini wengi walihusisha mabadiliko hayo na uamuzi wa Nape wa kupinga uvamizi unaodaiwa kutokea katika kituo cha runinga na redio cha Clouds na kuunda kamati ya watu watano iliyochunguza na kutoa ripoti iliyoonyesha kuwa ni kweli uvamizi ulifanyika ukihusisha askari wenye silaha.

Nape alisema ataiwasilisha ripoti hiyo kwa wakuu wake ili hatua zaidi zichukuliwe.

Baada ya kuenguliwa kwake katika nafasi ya uwaziri, ndipo Nape alipotoa taarifa kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter akisema kuwa angezungumza na waandishi wa habari saa 8:00 mchana jana, kwenye ukumbi wa hoteli moja iliyopo Oysterbay, jirani na Kanisa la St. Peters.

ILIVYOKUWA
Muda mchache kabla ya kuwasili kwa Nape, waandishi wa habari waliokuwa wakimsubiri kwa shauku kubwa walistushwa na taarifa kwamba mkutano huo usingekuwapo.

Uongozi wa hoteli yenye ukumbi huo ulitangaza kutokuwapo kwa mkutano huo wa Nape kupitia kwa ofisa aliyejitambulisha kwa jina la Suleiman Kapaso, ukiwaomba waandishi waondoke kwa sababu ya kile alichodai kuwa ni amri ya kuzuia mkutano huo waliyoipata kutoka kwa Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Suzan Kaganda.

“Nimeambiwa nizuie mkutano kufanyika,” alisema Kapaso.

Baada ya hapo, waandishi waliondoka kwenye eneo la hoteli. Hata hivyo, hawakwenda mbali bali walisubiri eneo jirani, kwenye viwanja vya Kanisa la St. Peters. Wengi waliamua kuendelea kusubiri kutokana na ujumbe wa Nape kupitia akaunti yake ya twitter kuwa angefika hapo na mkutano uko palepale.

Hatimaye, ilipotimia saa 7:50 mchana, Nape alifika eneo hilo akiwa kwenye gari lenye namba za usajili STL 3107. Kabla ya kuteremka, gari lenye namba za usajili T920 BJF, likiwa limewashwa taa kubwa liliendeshwa kwa kasi kwenye eneo hilo na kwenda kusimama pembeni ya gari la Nape huku waliokuwamo ndani wakiteremka na kumzuia Nape kuteremka garini.

Alipoteremka, ni hapo ndipo Nape alipoonyeshwa mtutu wa bastola na mmoja wa watu waliokuwa wakimzuia asiteremke garini.

Badala ya kutii agizo, Nape alipuuza vitisho hivyo ‘kikomandoo’ kwa kuwajia juu watu waliomuonyesha bastola, akiwahoji kwa sauti kali kuwa ni nani aliyewatuma na kwa nini wanatishia watu bastola katika nchi hii iliyo huru.

“Nataka aliyeinua bastola hapa, aje aeleze nani kamtuma na kwanini ameinua bastola hapa. Mimi mwanahabari… nisipopigania uhuru wa hawa wanahabari napigania uhuru wa nani? Mambo gani tunafanyiana?” Alihoji Nape.

Kuona hivyo, watu hao wakanywea. Nape aliwazidi pia ujanja askari waliokuwa wakijaribu kumzuia ili asiongee na waandishi na wananchi waliojitokeza eneo hilo kwa kuonekana kama ametii agizo kwa kurudi ndani ya gari yake. Kumbe haikuwa hivyo.

Sekunde chache baadaye akachomoza kwenye paa lililofunguliwa la gari lake hilo na kuanza kuzungumza yale aliyokuwa amepanga, yote hayo yakifanyika kwenye eneo la viwanja vya Kanisa la St. Peters.

Hata hivyo, utata kuhusiana na kile kilichotokea ulidhihirishwa na Kamanda Kaganda baadaye wakati alipoulizwa na Nipashe kuhusiana na suala hilo, saa 8:30 mchana.

Kamanda Kaganda alisema hajatoa agizo la kuzuia mkutano wa Nape na waandishi wa habari.

“Mwandishi, nani amekwambia kuwa nimezuia mkutano wa Nape usifanyike hotelini? Sijauzuia… na sasa hivi mbona naona mkutano unaendelea kufanyika?”Alisema Kaganda.

AVIASA VYOMBO VYA ULINZI
Akizungumza zaidi, Nape aliviasa vyombo vya ulinzi kuwa makini na kila wanachokifanya ili wasimamie wajibu wao.

“Nataka vyombo vya ulinzi na usalama vya nchi hii viangalie wanachokifanya… Sijasema nafanya lolote. Mimi niliteuliwa, sikuulizwa wakati nateuliwa. Wakati (Rais) anataka kuweka Mtanzania mwingine sina sababu ya kuulizwa na wala sina kinyongo na rais.

Sijasema nina kinyongo… kwa nini kuna watu wanataka kukaa mahali wao ndiyo wawe waamuzi wa mawazo ya vijana wa nchi hii?”Alisema.

“Vijana wa Kitanzani lazima wasikie. Hatuna cha kuogopa isipokuwa uoga wenyewe. Nimekuja, nimesimama mtu anatoa bastola nirudi kwenye gari. Nani amekupa mamlaka hayo, unalipwa kwa kodi ya wavujajasho alafu unatoa bastola nilirudi kwenye gari,” Nape aliongea kwa hasira.

AKUMBUSHIA ALIVYOINUSURU CCM
Huku akiwaonyesha waandishi wa habari kovu kwenye mkono wake wa kulia wakati akikumbushia jitihada zake za kukipigania Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape alisema:“Nimekwenda miezi 28 nalala porini (angalieni mkono wangu huu), nimepigana kuirudisha CCM madarakani…alaah mnataka mnionee? Haiwezekani. Mimi mtoto wa Kimakonde.”

Alisema hana kinyongo na uamuzi wa Rais na kwamba kama ambavyo hakumshawishi kumchagua ndivyo ambavyo hawezi kusema na uamuzi wake (rais) na kwamba wakati anaunda Baraza la Mawaziri walikuwapo watu wengi sana na alipoamua kumchagua (Nape) kuna ambao walikubali.

“Nimejitahidi kutimiza wajibu wangu.

Jana wakati naongea na vyombo vya habari kutoa ripoti ya kamati kuchunguza tukio la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, nilisema kuna gharama ya kulipa kwenye kusimamia haki za watu na mimi nipo tayari kusimamia gharama hiyo, sioni sababu kwanini vyombo au watu waogope,” alisema na kuongeza:

“Nape ni mdogo kuliko nchi. Tanzania yetu kubwa kuliko Nape. Tusihangaike na Nape tuhangaike na Tanzania yetu inakokwenda hilo ndilo kubwa kuliko yote.

Uzalendo wa Nape hauwezi kutiliwa shaka hata kidogo na vijana wahuni wanaokuja kunyoosha bastola kwa Watanzania walio huru,” alisema na kuongeza.

“Nimekuwa mzalendo, muungwana kwa nchi yangu na ninaapa kuendelea kuwa muungwana kwa nchi yangu, hilo hakuna atakayelibadilisha, lakini nimekuwa mzalendo kwa CCM ambayo niliikuta iko kwenye shimo inakwenda,nikasimama kuinua, Watanzania wanajua, uzalendo huo hauna shaka hata kidogo,” alisisitiza.

“Uzalendo huo ndiko nilikoambiwa nitasema kweli daima fitna kwangu mwiko.Nilichokisimamia juzi ni kusema kweli.

Kinachowakutanisha watu siyo magwanda ya kijani ni imani, kwamba tuwe wakweli daima tuachane na fitna na hicho ndicho nakisimamia siwezi kukana, nikikana nihame.”

Alisema yeye ni mzalendo kwa nafsi yake mwenyewe na amefundishwa na marehemu baba yake, mzee Nnauye, kusema kweli na kusimamia anachokiamini.

“Kama ninachokiamini kitaleta matatizo sina shida, nadhani mnakumbuka niliwahi kufukuzwa CCMna katika maisha ya kisiasa usipopitia kwenye migogoro, bado hujakomaa,” alisema na kuongeza:

“Shuruti mbegu iote lazima ioze ndipo iote, sasa mbegu niliyoipanda kwa hakika itaota, mbegu ya kusimamia haki kwa hakika itaota.

Vijana wenzangu wa Kitanzania hamna la kuogopa simamieni kile mnachokiamini. Tanzania ni yetu, Mwalimu Nyerere, wazee Kawawa na Nnauye walikuwapo wakaondoka, suala la kujiuliza tunawaachia Watanzania nchi ya namna gani? Uamuzi wa namna ya nchi ya kuwaachia ni wa kwetu wenyewe.”

AMSHUKURU MAGUFULI
Nape alimpongeza na kumshukuru Rais kwa kumwamini kwa mwaka mmoja na kumpa heshima ya kuingia kwenye Baraza la Mawaziri.

“Kama alivyoniamini ndivyo ambavyo anadhani nimetumika imetosha anamweka Mwakyembe,” alisisitiza.

AMPONGEZA MWAKYEMBE
Nape alimpongeza Dk. Harrison Mwakyembena kueleza kuwa ana Imani naye kwa kuwa ni mwanahabari na mwanasheria hivyo atasimamia haki.

Aidha, alisema alitumia akili, nguvu na uwezo wake wote kuwatumikia na kwamba walimpa ushirikiano wa kutosha na kwa kipindi chote amefurahi kufanyakazi nao.

“I real love you people (Nawapenda nyote) kwa dhati ya moyo wangu nimefurahi kufanyakazi na nyie, ninawaombeni muungeni mkono Waziri mpya aliyepewa dhamana ya wizara hii,”alisisitiza.

ASISITIZA RAIS AUNGWE MKONO
Nape aliwataka kuendelea kumuunga mkono Rais “ndiye tuliyenaye, ndiye tuliyepewa na Mungu, tumempigia debe sisi, Watanzania wakamuamini wakampa dhamana, nawaomba mumuunge mkono, Watanzania tuendelee kudumisha umoja na mshikamano wa nchi, najua wapo walioumia kwa namna moja au nyingine, ila maisha lazima yaendelee.”

Alisema siyo wakati mwafaka wa kuvuruga nchi, bali kuwa wamoja na kwamba ni lazima kusimamia wanachokiamini.

Kuhusu jimboni kwake Mtama, alisema alipoondoka Ukatibu Mwenezi wa CCM alikwenda kuomba ubunge na siyo kuomba uwaziri na kwamba anarudi kufanyakazi aliyotumwa na wananchi wa jimbo la Mtama kuhakikisha maendeleo ya dhati yanapatikana.

POLISI WAMVAA
Nape alimaliza kuzungumza na waandishi wa habari saa 8:30 mchana na kutaka kuondoka katika viwanja hivyo, lakini ghafla gari la Polisi lenye namba PT 2574 lilizuia gari la Nape kuondoa katika eneo hilo.

Dakika chache baadaye aliteremka askari kutoka katika gari hilo la polisi na kwenda moja kwa moja katika gari la Nape na kuzungumza naye, na muda mfupi Nape aliteremka katika gari lake namba STL 3107 na kumfuata Kamanda wa Polisi Kinondoni, Suzan Kaganda aliyekuwamo katika gari hilo la polisi.

Mazungumzo ya wawili hao yalichukua takribani dakika 15 kisha Nape alirudi katika gari lake na kuwaambia waandishi wa habari: “ Nipo salama, nawaomba muondoke mrudi nyumbani kama kutakuwa na lolote nitawataarifu, kwa sasa ninaenda nyumbani kwangu,” kisha aliondoka huku akiwapungia mkono.

“Namna ya kunisaidia ni nyie kuondoka kwenda kwenye kazi zenu, huyu RPC anaondoka na mimi nakwenda kwangu, nendeni mkatulie,” aliwaambiwa wanahabari waliotaka kujua nini kimetokea baina yake na polisi.

KINA BASHE, ZITTO WAMFARIJI
Baada ya kuwapo kwa taarifa ya Nape kuondolewa kwenye nafasi ya uwaziri jana, baadhi ya wabunge walituma ujumbe wa kumtia moyo na kumpongeza.

Aidha, wachambuzi na wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa nchini, walitoa maoni yao mbalimbali kuhusu kuondolewa kwa Nape kulikohusishwa na hatua yake ya kutetea uhuru wa vyombo vya habari baada ya tukio la kituo cha Clouds kuvamiwa na askari wenye silaha usiku wa Alhamisi iliyopita.

Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini ambaye pia ni Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema kuondolewa kwa Nape kunaonekana kuwa chanzo chake ni msimamo wake wa kupinga kuingiliwa kwa uhuru wa vyombo vya habari.

Zitto alisema Watanzania hawapaswi kumlilia Nape kuwa ameonewa bali, wawawajibishe wanaokwenda kinyume cha kanuni na taratibu za nchi.

“Sisi kama wanasiasa, tunapaswa kuwaongoza wananchi kuona mabaya na mazuri ili kuchukua hatua na naamini hatua zitachukuliwa," alisema Zitto.

Mbunge wa Nzega, Hussein Bashe (CCM), pia alituma ujumbe kupitia ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii wa twitter akimfariji Nape juu ya kile kilichotokea.

Katika ujumbe huo, Bashe alisema: "Karibu 'back bench' tutumikie taifa letu, majimbo yetu na chama chetu. Usivunjike moyo. It’s just begining of a new journey (ni mwanzo tu wa safari mpya)."

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hellen Kijo-Bisimba, alisema kitendo cha Nape kuonyeshewa silaha kimewasikitisha na ni aibu kwa nchi.

"Kwa askari kumtolea bunduki waziri kisa asiongee na waandishi wa habari!... Mbona hawakumzuia jana (juzi)? Iweje leo (jana) wamzuie kuongea na waandishi wa habari?" Alihoji Bisimba.

"Nchi yetu ni ya amani haijui masuala ya kutishiana silaha… hili ni kosa kisheria, polisi wamekiuka maadili na Katiba ya nchi kwa ujumla."

Mhadhiri Mwandamizi wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema Nape ni kiongozi pekee Afrika ambaye ameweza kuunda kamati ya uchunguzi ikafanya kazi ndani ya saa 24 na kuleta majibu ambayo matokeo yake ndiyo yaliyomuondoa kwenye nafasi yake ya uwaziri.

Alisema popote duniani kusimamia haki huzua mambo mengi yaliyojificha ndani yake.

“Ili ufanye kazi na Rais, waziri unatakiwa umsome Rais unayefanya naye kazi, ni vizuri mawaziri wakajifunza jambo hili ili wajue Rais anataka nini,” alisema Dk. Bana.

Dk. Bana alisema angekuwa katika nafasi ya Nape na anajua kuwa anatenda haki, asingesubiri hadi atumbuliwe bali angekaa kando mwenyewe ili aendeleze mapambano ya kuidai haki akiwa nje ya uwaziri.

Richard Mbunda, Mhadhiri UDSM, alisema anachokiona kwa ujumla ni wasaidizi wa Rais kukosa fursa ya kutenda.

"Kitu alichokifanya Nape baada ya tukio la kuvamiwa kwa studio (Clouds) ni kwamba alijaribu kufuatilia jambo hilo kwa kina kwa kuwa ndiye waziri mwenye dhamana. Asingeweza kuishia kusema watu waende polisi," alisema.

Mbunda alisema Nape alichukua uthubutu wa kujaribu kufuata taratibu kwa kuunda kamati na baada ya kukabidhiwa ripoti aliahidi kuiwasilisha kwa wakubwa wake wa kazi akiwamo Rais.

“Siku ya pili inatoka taarifa kuwa kuna mabadiliko yamefanyika… hii inaonyesha utawala wa hofu kwamba wasaidizi wawe wanafanya kazi kwa kuangalia kuwa hivi Mheshimiwa atalipenda hili kweli," alisema.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Deus Kibamba, alisema wanalaani vikali kitendo cha kutumika kwa silaha kumzuia Nape kuongea na waandishi wa habari na kwamba tukio hilo ni la hatari kwa taifa kwa sababu linawapa usugu Watanzania.

Alisema waliopewa mamlaka ya kutumia silaha hizo, wazitumie katika kudhibiti uhalifu, ujambazi na waovu, lakini siyo kutumika kinyume cha malengo hayo.

Alishauri Katiba ibadilishwe ili wateule wote wa Rais wawe wanapita bungeni wakaidhinishwe kama Tume ya Katiba ilivyokuwa imependekeza.

Chama cha Wananchi (CUF) kupitia Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi Taifa, Julius Mtatiro, jana kilitoa tamko kuhusu mabadiliko hayo yaliyomuondoa Nape madarakani kwa kueleza kuwa hakiungi mkono kwa sababu kuna ishara kuwa waziri huyo aliondolewa kibabe kutokana na kusimamia kwake haki, uhuru, uwajibikaji, nidhamu na maadili ya uendeshaji wa vyombo vya habari.

AKUMBUSHIWA YA GOLI LA MKONO, BUNGE ‘LIVE’
Katika hatua nyingine, baadhi ya wafuatiliaji wa siasa walikumbushia baadhi ya kauli za Nape wakati akiipigania CCM kwenye kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu na pia aliposimamia suala la kuzuia kurushwa matangazo ya mijadala ya Bunge moja kwa moja kuwa ni funzo kwa wanasiasa kuwa vitendo vinavyoashiria kuminya haki ya wengi huwa havichagui mtu kwani humkuta yeyote.

“Nape alikuwa maarufu wakati wa uchaguzi (mwaka 2015) kwa kauli yake kuwa lazima wao (CCM) washinde hata kwa goli la
mkono…na ndiye aliyekuwa kinara pia kusimamia utekelezaji wa amri ya kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya Bunge.

“Mambo hayo yote ni sehemu ya ukiukaji wa haki dhidi ya wengi na kilichomkuta ni mwendelezo wa ukiukaji huo wa haki,” mmoja wa wachambuzi wa masuala ya siasa aliiambia Nipashe.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: