HIVI NDIVYO RC MAKONDA NAMNA ALIVYOSHIKA VYOMBO VYA HABARI TANZANIA
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ameendelea kulaaniwa na wadau mbalimbali wa habari, huku wakimtaka Rais Dk. John Magufuli asikilize sauti za Watanzania kuhusu kiongozi huyo. Hatua hiyo imekuja baada ya mkuu huyo wa mkoa kufanya uvamizi katika kituo cha televisheni kinachomilikiwa na Clouds Media Group kwa lengo la kuamuru kurushwa kwa kipindi kinyume cha sheria na kanuni za uandishi wa habari.
Makonda alivamia kituo hicho Ijumaa ya Machi 17, mwaka huu saa 4:46 usiku akiwa na askari pamoja na maofisa wa idara nyeti, ambao walikuwa wamebeba silaha nzito kwa lengo la kwenda kuwatisha watangazaji waliokuwa zamu. Akizungumza jana Dar es Salaam, Waziri Mkuu Mstaafu wa Serikali ya awamu ya tatu, Frederick Sumaye, amesema hawezi kushangaa mambo anayofanya Makonda endapo atakuwa amepata alama sifuri katika taaluma yake.
Sumaye ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alisema hawezi kumtupia lawama Makonda kwa kile anachokifanya, endapo matokeo ya elimu yanayozungumzwa yana ukweli ndani yake. Alisema licha ya Rais Dk. John Magufuli kumkingia kifua kwa kusema kuwa hataki kupangiwa nani awe nani katika utawala wake, ila kama kuna mtu anakosesa ni vema akashauriwa ili aweze kufanya marekebisho.
“Kutokana na alichokifanya Makonda kuvamia Clouds Media Group na anayoendelea kulaumiwa na kulalamikiwa katika utendaji wake, hafai kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. “Rais anatakiwa kumpangia kazi nyingine yoyote itakayomfaa kulingana na uwezo wake wa kuongoza, lakini sio kuongoza Mkoa wa Dar es Salaam, hapa hapamtoshi kabisa,’’ alisema Sumaye.
Alisema kinachotokea kwa sasa kinaitwa ‘Level of incompetence’, hapo ndiyo kiwango chake cha mwisho, haiwezekani Mkoa wa Dar es Salaam ukategemea maajabu zaidi ya anayofanya Makonda. Sumaye alihoji kauli ya juzi ya Rais Magufuli kwa kusema kwamba alichukua fomu yeye mwenyewe, huku akimtaka kukumbuka kuwa wananchi ndio ambao walimpigia kura hadi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano jambo ambalo anatakiwa kuwasikiliza wanachoshauri kwake.
Alisema kutokana na mambo mbalimbali anayofanya Makonda, ambayo yamekuwa hayawapendezi wananchi, wao hawatoshirikiana naye katika utendaji wowote katika Mkoa wa Dar es Salaam, kama ambavyo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alivyosema wakati wa mkutano wa uchaguzi wa Kanda ya Pwani. Katika hatua nyingine, Sumaye alizungumzia Mkoa wa Pwani kutokuwa na maendeleo kuliko kanda nyingine yoyote jambo ambalo kama Chadema walisema kuwa wataanza na hilo.
Alisema Pwani imeelemewa na migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, hivyo wao watatumia uwezo wao katika kuisukuma Serikali kuweza kusimamia na kutatua matatizo hayo. Sumaye alisema kwa upande wa maendeleo ya Mkoa wa Dar es Salaam, ni kutokana na mkoa huo kuongozwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na ni lazima Serikali itatekeleza maendeleo kwa kuwa iko chini yao.
Pia aliutambulisha uongozi mpya wa Kanda ya Pwani ikiwa ni pamoja na Makamu Mwenyekiti, Saed Kubenea, ambaye pia ni mbunge wa Ubungo na kuahidi kushirikiana katika kuinyanyua Pwani kutoka ilipo sasa. KITUO CHA SHERIA Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimesema kitendo kilichofanywa na Makonda kuvamia Kituo cha Televisheni cha Clouds ni kosa la jinai, hivyo Serikali imchukulie hatua. Mbali na hilo, kituo hicho kimewashauri Clouds kumshtaki Makonda, huku kikivitahadhalisha vyombo vya habari kuwa na urafiki usiovuka mipaka na badala yake visimamie weledi wa kazi.
Kituo hicho pia kimemshauri Rais Magufuli kusikiliza sauti za Watanzania kwani licha ya kuchukua fomu ya kugombea urais peke yake, hakujipigia kura mwenyewe.
Akizungumza jana, Mkurugenzi wa kituo hicho, Dk. Hellen Kijo-Bisimba, alisema hatua hiyo ya Makonda inaangukia katika kosa la jinai chini ya kanuni ya adhabu ya mwaka 2002.
“Kitendo kilichofanywa na Makonda ni ukiukwaji mkubwa wa misingi ya uhuru wa habari na utawala wa sheria, vitendo kama hivyo vinaidhalilisha Serikali kitaifa na kimataifa kama nchi ambayo inajipambanua kuwa kisiwa cha amani. “Vyombo vya habari vipo kwa mujibu wa sheria na vinaongozwa na sheria kadhaa, ikiwamo ya huduma za vyombo vya habari ya mwaka 2016, hivyo vinapaswa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na si kuingiliwa na mtu binafsi au mamlaka,” alisema Dk. Bisimba. Kwa mujibu wa Dk. Bisimba, sheria hiyo imeeleza wazi mamlaka ambazo zinaweza kuviwajibisha vyombo vya habari pale ambapo vitaonekana vinatoa habari za uchochezi kama ilivyoelezwa katika kifungu cha 49 (1) na 50 (1).
“Pale inapotokea watu binafsi au mamlaka kutumia nafasi walizonazo kutaka kushinikiza habari fulani kutolewa na vyombo vya habari kwa masilahi binafsi, ni kukiuka misingi ya sheria. “Na kama jambo hilo linafanywa na mtu mwenye mamlaka ya kuhakikisha utekelezwaji wa sheria na ulinzi wa amani katika mkoa, kwa mujibu wa sheria ya Tawala za Mikoa kifungu cha 5 (1), ni jambo la kihuni na la kupingwa kwa nguvu katika taifa linalofuata misingi ya haki na utawala wa sheria,” alisema.
Mkurugenzi huyo pia aliwataka viongozi kuacha kutumia vyombo vya dola kwa manufaa binafsi kama ilivyofanyika katika kituo cha Clouds. “Vyombo vya habari viwe na msimamo kama ilivyowahi kutokea wakati waandishi Christopher Kidanka na Mpoki Bukuku walivyopigwa. Viache kufanya naye kazi,” alisema.
HAPA KAZI TU Kituo hicho kimesema jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano ya kuhamasisha uwajibikaji kupitia kaulimbiu ya ‘Hapa kazi tu’, inatakiwa kuwa chachu ya kulinda misingi ya sheria na si kutumika kama kichaka cha kuvunja sheria. “Rais alichukua fomu, lakini fomu zake hazikumpigia kura, awe na tabia ya kusikiliza kwa sababu alipigiwa kura na hata wasiompigia walikubali matokeo,” alisema.
WANASHERIA TANGANYIKA Baraza la Uongozi la Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), limetoa tamko na kusema limesikitishwa na kauli iliyotolewa na Rais Magufuli ya kukubali uvamizi wa ofisi za Clouds. Clouds Media Group ilithibitisha kwamba uvamizi huo ulilenga kulazimisha chombo hicho kurusha video ambayo imetengenezwa chini ya mwongozo wa Makonda.
“Baraza linapenda kuweka wazi kwamba tabia ya aina hiyo kutoka kwa mtu anayeaminika na mwenye majukumu ya kulinda na kuheshimu sheria, sio tu kosa kwa uhuru wa habari na haki ya Watanzania katika uhuru wa kupata taarifa ambazo zote zinalindwa na katiba na sheria, lakini pia katika ahadi za kimataifa na kikanda chini ya mikataba mbalimbali ya kimataifa ambayo sisi tumesaini.
“Baraza limeona uvamizi wa silaha katika ofisi za Clouds Media ni mwanga na kuamini kuwa kitendo hicho kimeharibu taswira kama nchi ya kidemokrasia ambapo uhuru wa habari unaheshimiwa,” ilieleza taarifa hiyo ya TLS iliyosainiwa na Rais wake Tundu Lissu.
Kutokana na hali hiyo, TLS ilisema imesikitishwa na kitendo hicho cha Makonda na kauli ya mkuu wa nchi inatuma picha kwa Watanzania na dunia nzima kwa ujumla kuwa serikali na maofisa wake wanaruhusiwa kufanya vitendo vya uhalifu bila kuadhibiwa.
“Taswira ambayo imetengenezwa, iliyotengenezwa inaweza tu kuhamasisha wale ambao wangependa kuona nchi hii kuungukia katika utawala wa uasi, ukandamizaji na machafuko ya kisiasa,” ilifafanua taarifa hiyo.
Kutokana na hali hiyo Baraza hilo la Wanasheria Tanganyika, limelaani kitendo cha uvamizi wa Clouds Media kwa nguvu zote na linaisihi Serikali na maofisa wake kujiepusha na vitendo vya uhalifu na uvunjaji wa sheria siku za mbele.
Mbali na hilo, pia limemuomba Rais Magufuli kutafakari upya kauli yake kwa kumsaidia Makonda katika uharibifu uliosababisha Serikali kukosa sifa kitaifa na kimataifa.Mtanzania
0 comments:
Post a Comment