KASHFA YA FARU JOHN KUWANG'A VIGOGO WAWILI WA SERIKALI YA RAIS MAGUFULI
KAMATI iliyoundwa kuchunguza utaratibu uliotumika kumhamisha Faru John kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko kwenye Hifadhi ya Grumeti Serengeti, imependekeza hatua za kinidhamu dhidi ya maofisa wawili wa serikali.
Kamati haikufafanua aina ya hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa kwa maofisa hao, lakini umakini uliopo katika serikali ya awamu ya tano unaashiria upo uwezekano mkubwa kwa maofisa hao kutumbuliwa.
Ingawa kamati hiyo iligundua kuwa Faru John alikufa kifo cha asili, imependekeza hatua za kinidhamu kwa sababu hakukuwa na kibali rasmi cha kumhamisha kwenda mazingira ambayo yalisababisha kifo chake.
Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyelle alitoa pendekezo hilo jana wakati akikabidhi ripoti hiyo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa juu ya uchunguzi walioufanya kuhusu uhamishwaji na kifo cha mnyama Faru John.
Kamati hiyo imependekeza hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya Mkurugenzi wa Wanyamapori wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Profesa Alexander Songorwa na Daktari wa Shirika la Hifadhi la Taifa (Tanapa), Dk. Moris Kileo.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kusomewa ripoti huyo, Waziri Mkuu aliishukuru kamati ya uchunguzi;
“Ofisi yangu itaipitia taarifa hii ambayo ni kubwa kiasi na kuifanyia kazi. Matokeo ya kazi hiyo, tutayatoa hivi karibuni ili kuonyesha serikali imeamua kufanya nini juu ya mapendekezo yaliyotolewa,” alisema Waziri Mkuu.
Majaliwa alimtaka Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori, Robert Mande, afuatilie mapendekezo yaliyoainishwa na kamati hiyo na wayafanyie kazi mapema iwezekanavyo.
Kamati ilieleza hapakuwapo na mkataba rasmi kati ya serikali na mwekezaji unaoonyesha mnyama huyo ametoka serikalini kwenda kwa mwekezaji.
Pia kamati hiyo ilisema imebaini mnyama huyo alikufa kutokana na kukosa matunzo, kutokuwapo kwa uangalizi wa karibu pamoja na kutokupata matibabu alipokuwa anaumwa, alipohamishiwa katika hifadhi ya Grumeti.
Kadhalika, imebaini kulikuwapo na mapungufu ya kiuongozi kwa wizara, hifadhi na taasisi zake pamoja na mazoea yanayotokana na kutofuata taratibu zilizowekwa kisheria.
“Pamoja na kwamba mawasiliano yanaonyesha zoezi hilo liliridhiwa na wizara, hapakuwapo na kibali rasmi kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori cha kuruhusu kumhamisha Faru John kutoka NCAA kwenda Grumeti,” alisema Prof. Manyele.
Faru John alizua gumzo nchini mwishoni mwa mwaka jana baada ya Waziri Mkuu, Majaliwa, kufanya ziara Ngorongoro na kuwatuhumu maofisa wa shirika hilo na wale wa Idara ya Wanyamapori kwa ‘kumuuza’ Faru John kwa kampuni ya Grumeti kwa Sh. milioni 200.
Hatua hiyo ilisababisha Waziri Mkuu Majaliwa kuunda kamati hiyo Desemba 10, mwaka jana.
Baadaye alipokea pembe mbili zilizodaiwa kuwa za Faru John.
Aidha Waziri Mkuu aliagiza kuchunguza utaratibu uliotumika kumhamisha mnyama huyo kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Sasakwa pamoja na kutafuta kaburi la faru huyo ambaye Ngorongoro ilidai alikufa.
KUPIMA VINASABA
Akiwasilisha ripoti hiyo kwa Waziri Mkuu, Prof. Manyelle alisema kamati yake ilifanya uchunguzi wa kifo cha Faru John kwa kupima vinasaba vya sampuli mbalimbali vikiwamo mzoga, fuvu, mifupa, pembe, damu, ngozi na kinyesi kilichokaushwa ambapo ilibainika kuwa vyote ni vya mnyama mmoja aina ya faru mweusi dume.
Prof. Manyelle alisema maabara iliyotumika kupima ni ya Chuo Kikuu cha Pretoria, Afrika ya Kusini.
Prof. Manyelle alisema timu ya wataalamu kutoka Tanzania, wachunguzi wa serikali na jopo la wataalamu walikaa kujadili matokeo hayo.
“Sampuli zote hizo zilionyesha ni za Faru John, sababu za kufa kwake ni kukosa matunzo, uangalizi wa karibu pamoja na kukosa matibabu wakati anaumwa,” alisema Prof. Manyelle.
Alisema kamati ilibaini kutokuwapo kwa kibali rasmi cha kumhamisha Faru John kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori cha kuruhusu kumhamisha mnyama huyo kutoka NCAA kwenda Grumeti.
Alisema kutokana na mapungufu hayo ya kiutendaji yaliyofanywa na Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Wanyamapori na NCAA kuhusu Faru John kuondolewa bila kibali, Kamati imeshauri hatua za kiutawala zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Alisema walibaini kulikuwapo kwa migongano ya kimaslahi kati ya watumishi waliolenga kusimamia taratibu na wale wenye kusimamia maslahi binafsi wakati wa kuhamishwa kwa mnyama huyo.
Alisema pia walibaini kukosekana kwa mkataba wa kupokelewa kwa Faru John katika hifadhi ya Grumeti.
“Hapakuwapo na mkataba rasmi kati ya serikali na mwekezaji unaoonyesha mnyama ametoka serikalini kwenda kwa mwekezaji, mwekezaji alikwepa kuji-commit kwa maandishi,” alisema Prof. Manyelle.
WALA KUANGALIWA
Alisema pia walibani kutokufuatiliwa kwa afya na maendeleo ya Faru John baada ya kuhamishiwa na kwamba walimtelekeza na hata alipougua, hakutibiwa wala kuangaliwa zaidi ya walinzi na mwekezaji ambapo ulinzi ulikuwa imara.
Alisema pia wamebaini Mkurugenzi wa Wanyamapori ana madaraka na maamuzi makubwa kisheria juu ya wanyamapori.
Pia wamebaini maslahi binafsi yalitawala na kusababisha kuhamishwa kwa baadhi ya watumishi pamoja na uwapo wa taasisi nyingi zenye mamlaka sawa juu ya masuala ya uhifadhi wa wanyamapori kama vile Tanapa, NCCA, Tawa na Mkurugenzi wa wanyamapori, mipaka ya kiutendaji kutokujulikana hivyo kuwapo kwa taasisi hizo kunasababisha mwanya vitendo vya ujangili.
Alisema pia wamebaini uwapo wa viwanja vya ndege ndani ya hifadhi vinavyomilikiwa na wawekezaji ambavyo ni visababishi vya matukio ya ujangili.
Alisema wamebaini pia uwapo wa kamati mbili za kitaifa ambazo hazipo katika kisheria wala kanuni ambazo zinafanya maamuzi mazito ya kitaifa ambazo ni Kamati ya Uongozi na Kamati ya Ufundi.
Kadhalika, alisema pia wamebaini kuwapo kwa ongezeko la watu na mifugo ndani ya hifadhi bonde la Ngorongoro ambayo imefikia watu 90,000 badala ya 8,000 kisheria na hivyo kuongeza mwanya wa vitendo vya ujangili.
Prof. Manyelle alisema vile vile wamebaini kuwapo kwa uchukuaji holela wa sampuli za wanyamapori kwa lengo la utafiti na kuzisafirisha nje ya nchi na kwamba kumbukumbu za watafiti na aina ya sampuli zinazochukuliwa haziwekwi vizuri.
MAPENDEKEZO YA KAMATI
Prof. Manyelle alisema Kamati imependekeza taratibu za kuhamisha wanyama walio katika hatari ya kutoweka kama vile tembo na faru ziwekwe bayana, ziainishwe kwenye kanuni na sheria.
Pia Serikali kuunda tume huru kuchunguza migogoro ya kimaslahi kati ya watumishi wa NCAA dhidi ya uwekezaji ndani ya hifadhi pamoja na hatua stahiki zichukuliwe.
Lingine ni sheria husika za wanyamapori zipitiwe upya pamoja na vibali vya uwindaji vya wanyama wanaoelekea kutoweka kama vile tembo na faru vifutwe na sheria ipitiwe upya.
Pendekezo lingine ni viwanja vya ndege vilivyomo ndani ya hifadhi vifanyiwe tathmini ya kina juu ya manufaa ya uwapo wake, usimamizi na uendeshaji wake ili kulinda maslahi ya taifa.
Lingine ni kufanyika kwa utambuzi wa wakazi halali ndani ya Kreta ya Ngorongoro na maeneo mengine ya Serengeti na kuzuia uhamiaji katika maeneo hayo.
Serikali kuanzisha na kuimarisha maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Ktengo cha Sayansi Jinai na uchunguzi wa vinasaba vya wanyamapori ili kutoa sapoti kwa vyombo vya haki na jinai katika kupeleleza.
Kuimarisha vikosi vya kuzuia ujangili kwa kushirikisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania pamoja na serikali kupitia Tanapa iandae taratibu na kanuni zilizo wazi ambazo zinahusisha uwapo wa mkataba kati ya serikali na wawekezaji.
Pendekezo lingine ni kuanzishwa kwa ‘database’ ya vinasaba vya wanyamapori ambavyo itasaidia katika kutambua nyara. Madaraka ya Mkurugenzi wa Wanyamapori yafanyiwe tathmini kwa maslahi mapana ya taifa.
0 comments:
Post a Comment