Meneja mahusiano ya jamii Mamlaka ya MajiSafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) Neli Msuya akiwa amepiga mweleka chini baada ya kuteleza na kuanguka baada ya zoezi la kupanda miche ya miti aina ya mkangazi kupanda kwenye chanzo cha maji cha mto Dalu kijiji cha Langali tarafa ya Mgeta wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro ambapo jumla ya miti 5000 ilipandwa katika kuhitimisha kilele cha wiki ya maji 2017.
Gratius Haule akimsaidia Meneja mahusiano huyo kunyanyuka baada ya kuanguka kutokana na utelezi ambapo msafara huo ulikumbwa na changamoto kubwa ya utelezi.Hapa bila msaada !. Watumishi wengine wakipanda kwenye mlima kuelekea kwenye chanzo cha maji cha mto Dalu kwa ajili ya kupanda miche ya miti katika kilele hicho.Mholojia kutoka bonde la maji la Wami-Ruvu, Magrath George akitelemka kwa tahadhari kutokana na utelezi uliosababishwa na mvua kunyesha baada ya kazi ya upandaji miti kumalizika
Mandhari ya msitu unaonzia chanzo cha maji cha Dalu kisha kuingiza mto Mgeta na kumwaga mto Ruvu ukitapakaa kijani
Mkazi wa kijiji cha Langali wilayani Mvomero mkoani Morogoro, Paul Lubwasi akipanda mti kando ya chanzo cha maji cha mto Dalu kijiji hapo ambapo Mamlaka ya MajiSafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) iliandaa jumla ya miti 5000 na kupandwa wakati wa kuhitimisha kilele cha wiki ya maji 2017.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Langali tarafa ya Mgeta wakiwa wamebeba vifaa vyenye miti wakati wakielekea kwenye chanzo cha maji cha Dalu tayati kwa kupandwa.
Neli Msuya akiongoza msafara ya kuelekea kwenye chanzo cha maji tayari kwa zoezi la kupandwa kwa miche ya miti.Meneja mahusiano ya jamii Mamlaka ya MajiSafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) Neli Msuya akikagua miche ya miti aina ya mkangazi katika ofisi ya kata ya kijiji cha Langali wilayani Mvomero mkoani Morogoro muda mfupi kabla ya kwenda kupandwa kwenye chanzo cha maji ya mto Dalu ambapo jumla ya miti 5000 ilipandwa katika kuhitimisha kilele cha wiki ya maji 2017.
Na Juma Mtanda, Morogoro.
Mamlaka ya MajiSafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) imehitimisha kilele cha wiki ya maji mwaka 2017 kwa kupanda miche ya miti 5000 aina ya mkangazi na kutoa elimu ya kutunza mazingira kwa wanavijiji wanaoishi na kulima kando ya vyanzo vya maji ya mto Ruvu katika safu ya milima ya Uluguru mkoani Morogoro.
Maadhimisho hayo yaliendana na kufungua miradi ya maji na kuweka jiwe la msingi la mfumo wa usambazaji maji Dar es Salaam na Pwani.
Akizungumza na wananchi wakati wa upandaji miti katika chanzo cha mto Dalu kijiji cha Langali tarafa ya Mgeta wilaya ya Mvomero mkoa wa hapa, Afisa Uhusiano wa jamii wa Mamlaka hiyo, Neli Msuya alisema kuwa jumla ya miche 5000 imepandwa ili kuendeleza uoto wa asili katika vyanzo vya maji.
Neli alisema kuwa asili ya chimbuko la mto Ruvu imeanzia katika safu ya milima ya Uluguru baada ya kuwa na vijito 127 inayorisha mito mikubwa na kuungana kuwa mto Ruvu unaotegemewa na wakazi wa mikoa ya Pwani na Dar es Salaam kwa matumizi mbalimbali ya maji.
“Dawasa tunawajibika kupanda miti na kusaidia kutoa elimu ya kutunza mazingira kwa wananchi wanaolima kando ya vijito vinavyotiririsha maji kuingia mito mikubwa ili kutunza mazingira yasiharibiwe kwani vyanzo hivyo vimekuwa tegemeo kubwa kwa wananchi wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kupitia mto Ruvu.”alisema Neli.
Neli alisema kuwa kila mwaka Dawasa imekuwa ikishirikiana na wadau zikiwemo halmashauri zote za Dar es Salaam, ofisi ya mkuu wa mkoa huo, bonde la Wami-Ruvu na wananchi wa Morogoro kupanda miti kwenye vyanzo vya maji.
Kwa upande wa Mhalojia wa bonde la Wami-Ruvu, Rose Masikini alisema kuwa kazi kubwa iliyopo mbele ya wadau wa maji ni kutunza vyanzo vyote vya maji hasa kuzingatia sheria na kutunza mazingira kiujumla ili uoto wa asili uendelee kuwepo ili mito iweze kutiririsha maji vipindi vyote vya masika na kiangazi.
“Tayari bonde la Wami-Ruvu imeunda jumuiya tano za watumia maji na kazi za jumuiya hizo ni kusimamia matumizi sahihi ya maji lakini kutunza mazingira ikishirikiana na wananchi waishio kwenye vyanzo vya maji baada ya kupata elimu.”alisem Rose.
Afisa Mtendaji wa kijiji cha Langali wilayani Mvomero, Jesca Nyanga (29) alisema kuwa changamoto kubwa wanayokabiliana nayo viongozi ni kuzuia uchafuzi wa maji, kutunza mazingira na kutunza miti inayopandwa kwenye vyanzo vya maji.
Jescha alitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na kuzuia wananchi kulima kando ya vyanzo vya maji, uchafuzi wa maji na kuwa elimu zaidi inahitajika ili kukabiliana na hali ya mabadiliko ya tabianchi.
Mamlaka ya MajiSafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) imekuwa ikishirikiana na wadau wa maji kupanda miti kila mwaka katika vyanzo vya maji ya mito ya Mlali, Bunduki, Kiroka, Mgeta, Mzinga na mingine ili mto Ruvu uweze kuwa na maji ya kutosha.
0 comments:
Post a Comment