BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MADAKTARI 159 WA TANZANIA WAOMBA KAZI RASMI YA UTABIBU NCHINI KENYA

MADAKTARI 159 wamejitokeza kuomba kazi ya udaktari nchini Kenya kutokana na agizo la serikali kuruhusu madaktari 500 kwenda kufanya kazi huko.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema serikali inawatoa hofu madaktari hao juu ya usalama wao na kwamba waendelee kuomba nafasi hizo.

“Madaktari wetu hawa tunawatoa hofu wasiwe na wasiwasi kuhusu usalama wao wakifanya kazi nchini humo kwani Rais Uhuru Kenyatta ambaye ni mwenyeji wetu amemhakikisha Rais John Magufuli kuwa watakuwa salama wakati wote,” alisema Ummy.

Hivi karibuni, Rais John Magufuli aliridhia ombi la Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kwa kuruhusu madaktari 500 nchini kwenda kufanya kazi nchini Kenya, baada ya nchi hiyo kukumbwa na mgomo wa madaktari.

Waziri Ummy alisema imeandaliwa rasimu ya makubaliano kati ya Tanzania na Kenya ili kuhakikisha hayo yanasimamiwa kwa dhati na mambo waliyoahidiwa yanatekelezwa ikiwemo maslahi ya madaktari hao.

“Tunatarajia kutumia siku mbili serikali ya Tanzania na ya Kenya, kupitia rasimu hiyo na Machi 24, mwaka huu nitawasiliana na Waziri wa Afya wa Kenya ili tushauriane katika upungufu tutakaokuwa tumeubaini kabla hatujaweka saini Machi 27, mwaka huu,” alifafanua waziri huyo.

Aidha, alisema wadau mbalimbali wa sekta ya afya watahusishwa ili kupata maoni yao wakiwamo Chama cha Madaktari Tanzania (MAT).

Alikiri pia kuwa sekta ya afya kwa ujumla ina upungufu wa watumishi kwa asilimia 51 na kwamba upungufu huo sio wa madaktari pekee, bali watumishi wa sekta nzima.

“Tumewasiliana na wenzetu Utumishi na Wizara ya Fedha kuhusu ajira, lakini hatuwezi kuwaajiri madaktari hao wote 2,700 ambao wanazalishwa kila mwaka, mwaka huu tutaajiri, lakini tutaajiri madaktari 500 tu,” alibainisha Ummy.

Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohamed Bakari alisema serikali zote mbili zilijadili ajira hizo na faida zake kwa madaktari wa Tanzania na kwamba hiyo ni fursa za ajira kwa madaktari na pia itasaidia kuimarisha uhusiano baina ya Tanzania na Kenya.

“Madaktari 1,764 wanahitimu katika vyuo vya afya 11 vilivyopo nchini kila mwaka, mwaka huu tunatarajia idadi hiyo itaongezeka hadi kufikia madaktari 2,843, imekuja fursa hii ambayo tunaona itatupunguzia mzigo,” alisema Dk Bakari.

Alisema madaktari watakaokwenda nchini Kenya watapata uzoefu wa kufanya kazi nje ya nchi na kwamba kwa nyakati tofauti Tanzania imekuwa tukipokea madaktari kutoka katika mataifa mengine ikiwamo Kenya yenyewe.

Katika hatua nyingine, Waziri Ummy ametangaza kuwa wizara hiyo imefuta aina 20 za vinywaji vya pombe kali zilizofungashwa katika plastiki maarufu viroba.

Aidha, agizo hilo pia ni pamoja na kusitisha utoaji wa vibali vya viroba kwa pombe kali zilizofungashwa kwenye chupa zilizo na ujazo wa chini ya mililita 200 na kwamba usitishwaji huo umeanza rasmi Machi mosi mwaka huu.

Akifafanua agizo hilo, Ummy alisema Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ilikuwa imesajili aina 20 za vinywaji vya pombe kali vilivyofungashwa kwa namna hiyo na kati ya hizo aina tano muda wake wa usajili ulikuwa umekwisha.

“Uamuzi wa kupiga marufuku matumizi ya pombe hiyo, unatokana na athari mbalimbali zikiwamo za kiafya na kijamii, matumizi ya pombe hizi yamesababisha ajali nyingi, vifo, ulemavu na ni mzigo mkubwa kwa serikali katika tiba za magonjwa,” alisema.

Alisema uamuzi huo ni kwa mujibu wa Kifungu cha 25 (1) cha Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi, Sura 219 na kwamba kwa mujibu wa kifungu cha 20(2)(b)(2) cha sheria hiyo matumizi ya pombe hizo hayana tija kwa Taifa.

Alisema wizara hiyo inasubiri maelekezo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kujua iwapo vile viroba vilivyokamatwa viteketezwe au virudishwe viwandani ili vikafungashwe upya katika ujazo unaofaa.

Awali alipozungumza katika uzinduzi wa Bodi ya Taasisi ya Jakaya Kikwete, Waziri Ummy alisema pia kuwa watu wengi wanaoenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu ya saratani ni kwa ajili ya kipimo, hivyo serikali katika bajeti ijayo imetenga Sh bilioni 50 kwa ajili ya kununua mashine ya kipimo hicho.

“Maana yake Tanzania itakuwa ya kwanza ukanda huu wa Afrika Mashariki kuwa na kipimo hicho, kama tunavyojua wanavyoenda sio kwamba wanaenda kupata tiba, wanaenda kufanya kipimo, zaidi ya wagonjwa wa kansa wanaoenda nje ya nchi tutawapunguza kwa asilimia 50,” alisema Ummy.

Aidha, alisema serikali inadaiwa zaidi ya Sh bilioni 30 na hospitali za India ambazo zinawatibu wagonjwa wenye matatizo ya moyo wanaopelekwa na serikali na kwamba hospitali hizo zinakaribia kusitisha huduma kutokana na deni hilo.

“Acha niwe mkweli, fedha hizo tunatumia kulipa madeni, tunadaiwa zaidi ya bilioni 30, fedha kweli napata, lakini nadaiwa na hospitali za India tunazopeleka wagonjwa wetu,” alisema na kuahidi kuwa fedha zikitengwa kwa ajili ya matibabu nje ya nchi zitakuwa zinasambazwa Muhimbili, Taasisi ya Mifupa Moi na taasisi hiyo ya JKCI na Ocean Road.Habarileo
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: