NAPE NNAUYE AMALIZA KAZI YA KUMCHUNGUZA RC MAKONDA UVAMIZI WA KITUO CHA CLOUDS TV, RIPOTI KUTUA KWA WAKUBWA
Mwenyekiti wa Kamati Maalumu iliyokuwa ikichunguza tuhuma dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda za kuvamia ofisi za kituo cha Clouds, Dk Hassan Abbas (kushoto) akikabidhi taarifa ya kamati hiyo kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, Dar es Salaam. (Picha na Fadhili.
WAZIRI wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amepokea rasmi ripoti ya timu aliyounda kwa ajili ya kuchunguza tuhuma dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuvamia na silaha kituo cha habari cha Clouds, kilichopo Mikocheni, Dar es Salaam.
Aidha, Nape amewaahidi waandishi wa habari na Watanzania kwa ujumla kuwa ataiwasilisha ripoti hiyo pamoja na vielelezo vyake kwa wakuu wake wa kazi ambao ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Rais John Magufuli ili waitolee uamuzi sahihi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo, Nape aliipongeza kamati hiyo kwa kukubali kufanya uchunguzi huo kwa muda mfupi waliopewa hasa ikizingatiwa na uzito wa jambo lenyewe linalotakiwa kuchunguzwa.
“Nimepokea ripoti hii, najua kazi haikuwa ndogo, nawaahidi kuifanyia kazi kwa kuwasilisha kwa wakubwa zangu, kama kutakuwa na ushauri au maelekezo wao ndio wenye mamlaka ya kufanya hivyo,” alisisitiza waziri huyo.
Hata hivyo, alisema ni jambo la kawaida kwa binadamu kuwa na tatizo la udhaifu ila ni vyema inapotokea hivyo, binadamu huyo akakiri kulitambua tatizo hilo na kujirekebisha.
Aliwataka wanahabari kuwa watulivu na kuwahakikishia kuwa Dk Magufuli anawapenda wanahabari wote nchini na yupo mstari wa mbele kuhakikisha wanaboreshewa maslahi yao, lakini pia kuthaminiwa na ndio maana hata Sheria ya Huduma ya Habari ya Mwaka 2016, aliisaini katika kipindi kifupi tu tangu ipitishwe na Bunge.
Alisema Rais Magufuli ana nia njema na watanzania na ndio maana utawala wake umejikita zaidi katika eneo la uwajibikaji na kuwahamasisha wanahabari na Watanzania kuunga mkono jitihada hizo ili kuifanya Tanzania iwe eneo bora la kuishi.
Awali, wakati akiwasilisha taarifa ya ripoti hiyo kabla ya kumkabidhi Waziri, Katibu wa timu hiyo ya dharura, Deodatus Balile alibainisha kuwa utafiti uliofanywa na timu hiyo umebaini kuhusika kwa RC Makonda katika kuvamia akiwa na askari wenye silaha kituo cha televisheni cha Clouds na kuwatishia.
Alisema kupitia mahojiano na vielelezo vya mikanda ya video za usalama (CCTV), timu ilibaini kuwa kiongozi huyo pamoja na kuvamia ofisi hizo, pia aliwalazimisha wafanyakazi wa kituo hicho kumpatia habari ambayo haijakamilika, jambo ambalo ni kinyume cha sheria zote zinazosimamia vyombo vya habari nchini.
“Pia tumegundua kuwa baada ya kuingia na askari, aliwatishia watangazaji wa kipindi cha SHILAWADU na wengine waliokuwepo kazini usiku huo, kuwa atawafunga jela kwa muda wa miezi sita kwa kitendo cha kukaidi kutoa habari yake, ikiwa ni pamoja na kuwakagua kama wanatumia dawa za kulevya wakiwemo wafadhili wa kipindi hicho,” alifafanua Balile.
Alisema kutokana na vitisho hivyo, wengi wa wafanyakazi wa chombo hicho cha habari walijikuta wakilia na wengine wakiwa na hali mbaya hasa baada ya kiongozi huyo wakati akiondoka eneo hilo kuwasisitiza kuwa endapo taarifa za uvamizi wake zitatoka nje ya redio hiyo watakiona cha mtema kuni.
Alisema wamependekeza kuwa RC Makonda akiombe radhi Clouds na vyombo vyote vya habari, kwa kitendo chake cha kuvunja sheria za usalama na maadili kwa vyombo vya habari, lakini pia walimuomba Waziri Nape, kuwasilisha malalamiko ya vyombo vya habari nchini dhidi ya Makonda kwa mamlaka ya uteuzi nchini ili ichukue hatua stahiki.
Aidha, wameitaka Clouds kuzingatia taratibu, sheria na kanuni ilizojiwekea na kuhakikisha mtu ambaye hahusiki na si mfanyakazi wa chombo hicho, hajihusishi kwa namna yoyote na shughuli za uhariri wa vipindi vya chombo hicho.
Pia Katibu huyo alisema timu yao imependekeza vyombo vya dola vichunguze kwa kina tukio hilo, hasa kitendo cha askari kutumika wakiwa na silaha kutishia raia.
Balile pia alieleza kuwa pamoja na kwamba ripoti hiyo imekamilika, lakini haikupata upande wa Makonda wa kujieleza baada ya kiongozi huyo kushindwa kutumia fursa hiyo ya kujieleza katika muda wote aliotafutwa na kamati hiyo.
“Siku ya kwanza ya kuanza kazi hii, tulikamilika kila kitu cha upande wa Clouds, tulihoji wafanyakazi na kupitia mikanda ya CCTV na kupata ukweli wa tukio. Lakini kwa upande wa RC Makonda haikuwa hivyo, kila tulipompigia hakupokea simu wala kujibu ujumbe tuliokuwa tunamtumia,” alisema Balile.
Alisema ilibidi watumie wasaidizi wake kwa kuwasiliana nao ambao waliwataka wajumbe wa timu hiyo kwenda kumuona kiongozi huyo ofisini kwake.
Alisema walifika ofisini kwake saa tano asubuhi na kuambiwa wasubiri kwa kuwa Makonda alikuwa na ugeni wa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene.
Alieleza kuwa ilipofika saa sita na nusu waliambiwa waingie ofisini kwake tayari kwa mahojiano na kuelekezwa kutumia njia ya kupanda ngazi, hata hivyo walipoingia ofisini kiongozi huyo hakuwepo na baadaye waliambiwa ametokea mlango wa nyuma na ameenda kwenye jengo la Machinga Complex.
“Wakati tukiendelea kumsubiri, majira ya saa tisa mchana, alikuja mhudumu na kutujulisha kuwa Makonda hawezi kuja kwa kuwa amepata kazi nyingine. Hata hivyo, kamati imejiridhisha kuwa ameamua kwa hiari yake kutotumia fursa ya kuhojiwa,” alisema Balile.
Alisisitiza kuwa pamoja na hayo, kamati hiyo imejiridhisha kupitia vielelezo ilivyo navyo kuwa kiongozi huyo alifanya uvamizi huo katika chombo cha habari na kutoa vitisho kwa kutumia silaha, kinyume cha sheria za nchi, maadili ya viongozi na Katiba.
Nape aliunda timu hiyo ya watu watano kuchunguza suala la kilichotokea Clouds Media Groups, Ijumaa iliyopita ambako Makonda anadaiwa alivamia kituo hicho akishinikiza kurushwa hewani kwa habari iliyokuwa inamhusu mwanamke aliyedaiwa kuzaa na Askofu wa Kanisa la Uzima na Ufufuo, Josephat Gwajima.
Waliounda timu hiyo ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Dk Abbas Hassan, Mwakilishi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mabel Masasi, Mhariri Mwandamizi kutoka Kampuni ya The Guardian, Jesse Kwayu, Balile ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Mkurugenzi wa Kampuni ya Jamhuri na Mkurugenzi Mtendaji wa Upendo Media na Katibu Msaidizi wa TEF, Neng’ida Johanes.
Katika hatua nyingine, TEF kwa kushirikiana na Klabu ya Waandishi wa Habari Dar es Salaam (DCPC), wamelaani vitendo vya viongozi na wanasiasa wanaotumia vyombo vya habari nchini kwa manufaa yao binafsi na kukandamiza uhuru wa vyombo hivyo.
Aidha, wametangaza rasmi azma yake ya kutoandika au kutangaza habari zote zinazomhusisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutokana na kitendo chake cha kuvamia chombo cha habari cha Clouds Media huku akiwa ameambatana na askari wenye silaha.
Katibu wa jukwaa hilo, Neville Meena alisema jukwaa hilo, lina wajibu wa kuchukua hatua pale linapoona haki na uhuru wa vyombo vya habari nchini unakiukwa.
Wakati huo huo, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), mbali ya kulaani uvamizi huo unaodaiwa kufanywa na Makonda katika kituo cha Clouds, tume hiyo kupitia kwa Mwenyekiti wake, Bahame Nyanduga imeshauri Makonda akiri kuwa kitendo alichofanya ni uvunjifu wa haki za msingi za waandishi wa habari na uhuru wa vyombo vya habari.
Lakini kitendo cha kuvamia kituo cha runinga na redio cha Clouds Media Group kwa kutumia askari wa Jeshi la Polisi kwa maslahi binafsi ni kitendo kisichoendana na utawala wa sheria, amelidhalilisha Jeshi la Polisi, kwa hiyo ni budi awaombe radhi Watanzania.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment