BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

ELIMU BURE IMEKWAMA KUTOKANA NA CHANGAMOTO TANZANIA

 
MPANGO wa Serikali kutoa elimu bure kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ulioanza kutekelezwa mwanzoni mwa mwaka jana, umeshindwa kufanikiwa kutokana na changamoto mbalimbali. 

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya HakiElimu kuhusu utekelezaji wa mpango wa elimu bure, umebaini sababu kadhaa ikiwamo fedha za ruzuku kutofika shuleni kwa wakati na kutozingatia idadi ya wanafunzi kama ilivyotarajiwa. 

Akizindua utafiti huo Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa HakiElimu, John Kalage, alisema uchambuzi wa matokeo unaonyesha kuwa baadhi ya shule zenye wanafunzi wachache zinapata fedha zaidi kuliko shule zenye wanafunzi wengi. 

Akitolea mfano alisema Shule ya Msingi Mulemba iliyopo Muleba mkoani Kagera yenye wanafunzi 828, ilipokea Sh 3,918,000 ilhali Shule ya Ilolo iliyopo Mpwapwa mkoani Dodoma yenye wanafunzi 874, ilipokea Sh 3,400,000. 

Alifafanua kuwa kabla ya utekelezaji wa mpango wa elimu bure uliowaelekeza wazazi kutotoa michango mingine ya shule na kupiga marufuku masomo ya ziada katika waraka wa elimu namba tano wa mwaka juzi, pia shule za msingi zilipaswa kupata kiasi cha Sh 10,000 na sekondari Sh 25,000 kwa kila mwanafunzi kwa mwaka kwa uendeshaji wa shule, ununuzi wa vitabu, vifaa vya mitihani na ukarabati. 

“Asilimia 40 ya ruzuku kwa shule za msingi na asilimia 50 kwa shule za sekondari inapaswa kubaki Tawala za Mikoa kwa ununuzi wa vitabu, asilimia 60 kwa shule za msingi na asilimia 50 kwa shule za sekondari, inayobaki kupelekwa moja kwa moja shuleni kugharamia ukaratabi, vifaa, mitihani, utawala na michezo. 

 “Utafiti unaonyesha kuwa katika kipindi cha Januari hadi Juni, mwaka jana, Serikali ilipaswa kupeleka kiasi cha shilingi 3,000 kwa mwanafunzi wa shule ya msingi, lakini ilipeleka wastani wa shilingi 2,700 ambayo ni sawa na asilimia 93 na kupeleka ruzuku kwa sekondari kwa wastani wa asilimia 100,’’ alisema. 

Kalage alisema shule zenye wanafunzi wachache kati ya 200 hadi 300 zinapata wastani wa Sh 100,000 hadi 150,000 kwa mwezi na haziwezi kutatua matatizo ya msingi ikizingatiwa ruzuku zinatumwa shuleni kila mwezi, huku walimu wakishindwa kutatua changamoto hiyo. 

Pia alisema ruzuku zinazopelekwa shuleni hazikidhi mahitaji ya shule na hiyo imedhihirika kutoka kwa walimu wakuu 95, kwamba fedha wanazozipata hazitoshi kukidhi mahitaji mbalimbali. 

Kalage alisema hata baada ya kuanza kutekelezwa kwa mpango wa elimu bure, wazazi bado waliendelea kubanwa kwa kuchangishwa gharama mbalimbali za uendeshaji wa shule kwa watoto. 

Alizitaja gharama hizo kuwa ni pamoja na zile za kulipa walinzi, kujenga madarasa na kulipa wapishi na hiyo ilitegemea na wazazi wenyewe kwa kuwa wengine wanachanga na wengine hawachangi.

“Hii inahusishwa moja kwa moja na matokeo ya utafiti kuhusu uelewa wa wazazi kwenye namna ya elimu bila malipo, kwa sababu asilimia 51.3 ya wazazi wanaelewa kuwa elimu bila malipo maana yake wazazi kutochangia gharama zozote za elimu ya watoto wao katika shule za umma,’’ alieleza. 

Kalage aliendelea kusema kuwa mpango wa elimu bure umesababisha ongezeko la wanafunzi wa darasa la kwanza hasa kwa shule za msingi ambapo kuna ongezeko la asilimia 43 na asilimia 10 kwa shule za sekondari. 

Pia alisema elimu bure imesababisha walimu kuelemewa kwa kuwa awali ilikuwa kwa wastani mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 45, lakini kwa sasa mmoja anafundisha wanafunzi 164.  
 
MAONI YA WADAU WA ELIMU
Mchambuzi wa masuala ya kijamii, Jenerali Ulimwengu, akichangia katika uzinduzi wa utafiri huo, alisema kuwa huwezi ukatenganisha suala la elimu na siasa kwa kuwa chimbuko la elimu bure lilianzia katika kampeni za siasa. 

Alisema anashangaa Rais Dk. John Magufuli kukataza kuendelea na mikutano ya siasa hadi hapo mwaka 2020 wakati ingekuwa muda mwafaka kuweza kuendelea kukosoa kutoa mawazo na kuchangia hilo. 

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Bashiru Ally, alisema elimu ni gharama, hivyo kila mwanachi mwenye uwezo kwa kushirikiana na Serikali anatakiwa kuwekeza katika elimu.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: