Mbunge wa Kilombero Peter Lijualikali akidhibitiwa na askari hivi karibuni katika moja ya matukio yaliyosababisha kushtakiwa na kukaa rumande, juzi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilibadilisha kifungo chake cha miezi sita na kumwachia huru. Picha na Juma Mtanda.
Uamuzi wa Mahakama Kuu wa kutengua hukumu ya Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali ni mwendeleo wa kutenguliwa hukumu zinazofanywa na mahakama za chini hasa kwa kesi za kisiasa.
Pamoja na kutenguliwa hukumu hizo, majaji wamekuwa wakitoa maoni ya kulaumu kinachofanywa na mahakimu na wanasheria hasa wa Serikali kwa kutotenda haki.
Miongoni mwa kesi iliyotajwa na majaji kwamba ni kunajisi taaluma ya sheria ni iliyohusu dhamana ya Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema.
Lema, ambaye alikaa mahabusu takriban miezi minne baada ya Serikali kukata rufaa kupinga dhamana yake, alikamatwa Novemba 2016 akiwa bungeni Dodoma kwa tuhuma kuwa alitoa maneno ya uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli.
Hata hivyo, pamoja na hakimu kuweka wazi dhamana yake, haikuwa rahisi kwake baada ya Serikali kuizuia kwa madai kuwa ilikata rufaa na baadaye kufuatiwa na sarakasi zilizosababisha akae mahabusu kwa zaidi ya miezi minne.
Lakini, siku ya kusikiliza uamuzi dhidi pingamizi la dhamana, mawakili wa Serikali waliondoa rufaa yao, kitu kilichosababisha majaji kukemea uchezeaji wa sheria ulioonyeshwa na ofisi ya Mwendesha Mashitaka wa Serikali (DPP).
Jaji Bernard Luanda aliyekuwa mwenyekiti wa jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa alikuja mbogo kwa kusema;
“Tunaomba ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali muwe makini sana maana mnatufanya wanasheria wote hatuna akili na mnachafua Mahakama, kwa hali ya kawaida mtu mumshikilie kwa misingi ya kisheria, lakini katika kesi hii tumepitia jalada hatujaona kitu chochote cha kumshikilia Lema hadi leo na imetushtua sana,” alisema Jaji Luanda.
Juzi, Jaji Ama-Isaria Munisi wa Mahakama Kuu wakati akitoa uamuzi wa kutengua hukumu ya Lijualikali alionyesha kushangazwa na hukumu hiyo kwa kuwa hati ya mashtaka ilikuwa na kasoro na mrufani alikuwa mjumbe halali wa kikao alichotaka kuhudhuria.
Lijualikali ni miongoni mwa wanasiasa wengi waliohukumiwa kwa makosa mbalimbali na baadaye kuachiwa huru, baada ya kuonekana hawakuwa na hatia au kunyimwa kwao dhamana kulitokana na kutozingatia utashi wa kisheria.
Mbunge huyo wa Kilombero alihukumiwa kwenda jela miezi sita, Januari 11, 2017, bila ya chaguo la kulipa faini baada ya kuonekana kuwa na hatia ya kuvamia mkutano ambao hakualikwa.
Hata hivyo, Jaji Munisi juzi alitengua hukumu hiyo baada ya kukubaliana na warufani kwamba hati ya mashtaka ilikuwa na upungufu. Katika kesi hiyo, Lijualikali aliwakilishwa na mawakili wawili, Tundu Lissu na Fred Kiwelo wakati Jamhuri iliwakikishwa na Faraja Nchimbi.
Wanasiasa wengine ambao uamuzi wa mahakama za awali ulitenguliwa na Mahakama Kuu ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Lindi, Suleiman Mathew pamoja na Katibu wa Tawi la Kata ya Nyangamala, Ismail Kupilila waliohukumiwa kifungo cha miezi minane gerezani kwa kosa la kufanya mkutano bila kibali Januari 2017.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Godfrey Mhina wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi.
Mathew na wenzake wametoka nje kwa dhamana kusubiri kusikilizwa kwa rufaa yao inayopinga hukumu iliyowatia hatiani mapema mwaka huu, baada ya kusikiliza mashahidi sita wa upande wa mashtaka na kujiridhisha kuwa ushahidi wao umethibitika bila kuacha shaka.
Hata hivyo, Mahakama Kuu Kanda ya Kusini iliwapa dhamana baada ya kukubaliana na maombi yao wakati rufaa yao ikisikilizwa.
Ingawa mahakama za juu kutengua uamuzi wa mahakama za chini ni jambo la kawaida katika mfumo wa utoaji haki, mlolongo wa matukio ya kesi hizo zinazohusu wanasiasa umeibua mjadala.
Akizungumzia hukumu hizo, mhadhiri wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Onesmo Kyauke alisema masuala ya kisheria ni ya majadiliano, hivyo ni kawaida hukumu kutofautiana kutoka mahakama moja na nyingine.
“Kuna kesi nyingi tu hukumu zinatofautiana, siyo za siasa tu. Zipo kesi za ujambazi, mauaji siwezi kusema ni kesi za siasa tu,” alisema Kyauke.
“Kuna matatizo mengi yanayosababisha kesi ihukumiwe kinyume. Kwa mfano mawakili wa Serikali wanakosea kuandaa mashitaka, wanashindwa kuonyesha element of the offence (makosa). Mfano unasema huyu amefanya kosa la armed robbery’ (unyang’anyi wa kutumia silaha), lakini hasemi nani alitishiwa na hiyo silaha,” alisema Dk Kyauke.
Hata hivyo, alisema kama mtu anaona amehukumiwa kimakosa na akashinda rufaa, anaweza kumshitaki aliyemshitaki lakini anatakiwa athibitishe kuwa kulikuwa na njama katika kesi hiyo.
“Ni sawa na mpira wa miguu, mtu anapewa kadi nyekundu, lakini bado waamuzi wengine watasema pale ilitakiwa itoke kadi ya njano. Wakati mwingine majaji wanatoa maamuzi tofauti kwa kesi moja. Utakuta kesi inasikilizwa na majaji watano, watatu wanaamua tofauti na wawili wakawa na uamuzi wao, lakini uamuzi wa wengi ndiyo unachukuliwa.”
Mratibu wa mtandao wa watetezi wa haki za binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Ole Nguruma alisema wakati mwingine uhuru wa mahakama unaingiliwa.
“Kuna uhuru wa mahakama na uhuru wa watendaji wa mahakama. Pamoja na uhuru huo, watendaji wa mahakama wana utashi wa kisiasa na wakati mwingine msukumo kutoka nje,” alisema Ole Nguruma..
“Watendaji wa mahakama wanapaswa kusimamia misingi ya kazi yao hata kama wataingiliwa na mihimili mingine. Wakati mwingine mahakimu wanashindwa kusimamia uhuru walionao. Kwa mfano kesi hii ya Lijualikali, inaonyesha hakimu hakuwa serious (makini).”
Hata hivyo, Jaji Mstaafu Ameir Manento alisema kutofautiana kimaamuzi kwa mahakama ndiyo uhuru wenyewe.
“Uamuzi wa mahakama ya chini kubadilishwa na mahakama ya juu ndiyo uhuru wenyewe wa mahakama. Inawezekana hakimu wa mahakama ya chini hana uwezo, ndiyo maana rufaa inapelekwa mahakama ya juu ili kuchuja ule uamuzi. “Ndiyo maana wameweka ngazi; mahakama ya mwanzo, mahakama ya wilaya, mahakama ya hakimu mkazi.
Ngazi zimewekwa ili kuchuja uamuzi ili haki itendeke. Huo ni mfumo wa kimataifa na hata kwenye mahakama za kodi uko hivyo,” alisema Jaji Manento.Mwananchi
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment