BAADA YA EDWARD LOWASSA KUHOJIWA KWA SAA 4, ATAKIWA KURIPOTI TENA MAKAO MAKUU YA POLISI
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa
WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amehojiwa kwa zaidi ya saa 4 na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa tuhuma za uchochezi.
Lowassa alihojiwa jana Dar es Salaam katika Makao Makuu ya Polisi kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 8:14 mchana, kwa kile alichodai kuwa ni kutokana na hotuba aliyoitoa Jumamosi katika Jimbo la Ukonga lililo chini ya Mbunge, Mwita Waitara.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mahojiano hayo, Lowassa alisema kuwa baada ya mahojiano hayo, anatakiwa kuripoti tena katika ofisi hizo kesho saa 6 mchana.
“Nawapongeza kwa kula sikukuu ya Idd pamoja na mimi kule polisi mlitegemea kupata chochote kutoka kwangu. Ukweli niliitwa kuhojiwa kuhusu hotuba niliyoitoa siku moja kabla ya Idd kwa Mbunge Waitara wa jimbo la Ukonga,” alisema Lowassa.
Aidha, alisema kuwa wapo katika utekelezaji wa ilani ya chama hicho na kwamba wanachama wake wawe na amani, kwani mambo yako safi na ameitwa kwa nia njema.
Akijibu swali kuhusu kufifishwa kwa upinzani, mgombea huyo wa urais katika uchaguzi uliopita, alisema katika mazingira ya sasa asingependa kujibu swali hilo, kwani si wakati muafaka na kwamba hawezi kuingiza mazingira ya kesi iliyopo na masuala hayo.
“Waandishi mmefanya kazi nzuri sana kwa kuandika habari nzuri na kuhabarisha umma, niwaombe muendelee kufanya kazi hiyo kwa weledi, pia tunashukuru ushirikiano uliooneshwa na Polisi,” alisisitiza Lowassa.
Kwa upande wake, Wakili wa Lowassa, Peter Kibatala alisema walipokea mwito kutoka kwa DCI ukimtaka aripoti saa 4 jana. Alisema kuwa Lowassa anadaiwa kutoa maneno ya kichochezi Juni 23, mwaka huu katika futari iliyoandaliwa na Waitara.
“Mahojiano yalikuwa marefu kwa sababu ni question statement na Polisi ndio wanajua wanachunguza nini, lakini mashitaka ni ya uchochezi,” alifafanua Wakili Kibatala. Naye Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alisema walioruhusiwa kuingia ndani kwenye mahojiano ni Lowassa na wanasheria wake na kwamba wao walikuwa nje kama watazamaji.
Alisema kama chama hawaoni kuwa ni jambo baya kuitwa kwa Lowassa kuhojiwa, bali kuweka mambo mabaya yatambuliwe na pande zote na kwamba wanayo mambo mengine ya kidemokrasia yanapaswa kufuatwa.
“Serikali kupitia kitengo cha upelelezi kinachukua muda mrefu tofauti na masuala ya kijinai yalivyowekwa kwa kuwa wameridhia mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu wanapaswa kuzingatia muda, hivyo wanapaswa kuzingatia,” alisema Dk Mashinji.
Hata hivyo, nje ya makao makuu ya Polisi ulinzi uliimarishwa, ambapo licha ya kuwepo kwa Polisi wenye bunduki pia yalionekana magari ya maji washawasha yakipita mara kadhaa huku waandishi wa habari wakitakiwa kukaa mbali na eneo hilo.
Lowassa alikuwa Waziri Mkuu wa Tanzania katika Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais mstaafu- Jakaya Kikwete.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment