CHAI YA RANGI YAUA MUME, MKE KIJIJI CHA BAGA
WATU wawili wa familia moja, mke na mume wakazi wa Kijiji cha Baga, wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, wamefariki dunia baada ya kunywa chai ya rangi inayodhaniwa kuwa na sumu.
Mbali ya hilo, mpwa wao amenusurika katika tukio hilo ambalo limeacha maswali mengi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba, alithibitisha kutokea tukio hilo.
Alisema lilitokea Juni 19, mwaka huu saa saba mchana wakati familia hiyo ilipoandaa kinywaji hicho.
Aliwataja waliofariki wakati wakipatiwa matibabu katika Zahanati ya Baga kuwa ni Rajabu Ally (73) na Amina Rajabu (62).
Kamanda Wakulyamba alisema katika tukio hilo, mpwa wao Adam Saidi (12), mwanafunzi wa darasa la tatu Shule ya Msingi Mashine, alinusurika kifo.
Alisema miili ya marehemu imefanyiwa uchunguzi wa awali na kukabidhiwa ndugu kwa taratibu za mazishi, huku Jeshi la Polisi likiendelea na upelelezi wa tukio hilo.
“Katika tukio hilo ambalo limepoteza watu wa familia moja, mpwa wao alinusurika baada ya kunywa chai idhaniwayo kuwa ni yenye sumu, tunaendelea na upelelezi wa tukio hili,” alisema Kamanda Wakulyamba.Mtanzania
0 comments:
Post a Comment