LIONEL MESSI ANASURIKA KUFUNGWA CHA MIEZI 12 JELA
Nyota wa soka duniani Lionel Messi huenda akaamua kulipa faini kukwepa kifungo cha miezi 21 jela ambacho alihukumiwa na mahakama Uhispania kwa kosa la ulaghai wakati wa kulipa kodi, taarifa Uhispania zinasema.
Mwendesha mashtaka wa serikali nchini Uhispania anatarajiwa kubadilisha kifungo hicho kuwa faini ya €255,000 ($285,000; £224,000), ambayo ni sawa na €400 kwa kila siku ambayo angekaa gerezani.
Uamuzi wa mwisho kuhusu kulipwa kwa faini utatolewa na mahakama.
Messi, pamoja na babake Jorge, walipatikana na hatia ya kuilaghai Uhispania jumla ya €4.1m kati ya 2007 na 2009.
Mahakama mjini Barcelona iligundua kwamba walitumia maeneo salama kwa ulipaji kodi Belize na Uruguay ili kukwepa kulipa kodi.
Kando na huku hiyo ya kifungo jela, nyota huyo wa klabu ya Barcelona pia alitozwa faini ya €2m na babake €1.5m.
Walijitolea kulipa €5m "kama malipo ya kufidia", kiasi ambacho ni sawa na kiasi cha kodi ambayo anadaiwa kukwepa kulipa pamoja na riba, Agosti mwaka 2013.
Rufaa ya Messi dhidi ya hukumu hiyo ilikataliwa na Mahakama ya Juu nchini Uhispania mwezi jana, ingawa muda wa babake kusalia gerezani ulipunguzwa kwa sababu alikuwa amelipa kiasi fulani cha kodi.
Hata hivyo, Messi hajawahi kutarajiwa kwenda jela, kwani chini ya mfumo wa mahakama nchini Uhispania, kifungo cha chini ya miaka miwili jela kinaweza kutumikiwa kama kifungo cha nje.
Ufanisi wa Lionel Messi na masikitiko
Alifikisha magoli 500 akiwa na Barcelona Aprili 2017
Mshindi wa tuzo ya mchezaji bora duniani ya Fifa, Ballon d'Or, mara tano ambayo ni rekodi.
Alichaguliwa mchezaji bora zaidi wa Uefa barani Ulaya mara tatu
Ameshinda Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya akiwa na FC Barcelona mara nne.
Ameshinda ligi Uhispania mara nane akiwa na FC Barcelona
Anashikilia rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi La Liga
Alishinda dhahabu ya Olimpiki akiwa na Argentina mwaka 2008
Anaongoza ufungaji mabao Argentina akiwa na mabao 55 timu ya taifa
masikitiko:
Juni 16 2016: Aliangika daluga zake timu ya taifa Argentina baada ya kushindwa kufunga penalti fainali ya Copa America dhidi ya Chile (alibadilisha uamuzi huo baadaye) ilikuwa mara ya nne kwa Argentina kushindwa katika fainali kubwa katika miaka tisa walishindwa pia:
Copa America (2015) dhidi Chile (mikwaju ya penalti); Kombe la Dunia 2014 dhidi ya Ujerumani; Copa America (2007) dhidi ya Brazil
Messi hayko peke yake katika matatizo kuhusu kodi Uhispania. Mshindani wake Cristiano Ronaldo pia huenda akashtakiwa. Ronaldo anadaiwa kufanya ulaghai wa jumla ya €15m(£13m) katika ulipaji ushuru kati ya 2011 na 2014.
José Mourinho naye anadaiwa kulaghai maafisa wa kodi €3.3m (£2.9m; $3.6m) alipokuwa meneja wa Real Madrid kati ya 2011 na 2012
0 comments:
Post a Comment