BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

ADAU WADAI KUNA KITU SAKATA LA TUNDU LISSU

Harakati za Chadema kukabiliana na mazingira ya kisiasa ya sasa inazidi kuipambanisha na vyombo vya dola, na wiki hii viongozi wake wa juu walikamatwa tena, huku wengine wakiendelea kuhojiwa vituo vya polisi.

Wiki ilimalizika kwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kukamatwa akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), akitaka kuelekea mjini Kigali, Rwanda kuhudhuria mkutano wa wanasheria wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mbali na Lissu ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu, katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji na viongozi wengine nane, wakiwamo wabunge wa majimbo na viti maalumu, walikamatwa wakiwa wilayani Nyasa mkoani Ruvuma wakituhumiwa kuandamana kinyume cha sheria.

Dk Mashinji, ambaye alikuwa mkoani Ruvuma kukagua shughuli za maendeleo ya Chadema katika Kanda ya Kusini, alikamatwa pamoja na Cecil Mwambe, ambaye ni mbunge wa Ndanda, Zubeda Sakuru (viti maalumu) na viongozi wengine wa mkoa na kanda hiyo.

Wakati viongozi hao wakikamatwa wiki hii, Edward Lowassa, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Alhamisi aliripoti tena kituo cha polisi ambao wanaendelea na uchunguzi kama kauli zake zina uchochezi.

Matukio hayo yametokea wiki moja baada ya viongozi wengine wa chama hicho kumaliza wiki iliyoishia Julai 8 wakiwa mahabusu. Halima Mdee, ambaye ni mbunge wa Kawe, alikamatwa Julai 7 kwa amri ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi aliyeagiza awekwe mahabusu kwa saa 48.

Ijumaa ya wiki hiyo, mwenyekiti wa Chadema mkoani Geita, Fabian Mahenge na katibu wake, Sudi Kanganyala na wengine walikamatwa wakati wakiwa katika kikao cha ndani.

Wengine ni Vitus Makange, ambaye ni mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Geita, Neema Chozaire (mwenyekiti wa Bavicha wa mkoa), Uhuru Selemani (kaimu mwenyekiti wa Wilaya ya Chato), Mangesai Rudonya (katibu) na Marko Maduka (diwani mstaafu).

Lakini, kukamatwa kwa Lissu ndio kumekuwa gumzo kubwa zaidi.

Ingawa Lissu si mgeni wa mapambano na vyombo vya dola, mazingira ya kukamatwa kwake safari hii yamepokelewa kwa hisia tofauti, huku uchunguzi wa polisi uliohusisha upekuzi nyumbani kwake, kuchukua kipimo cha mkojo na waandishi kuhojiwa ukiibua maswali.

Mapema wiki hii, Lissu, akiwa mkoani Dodoma, aliamua kutotoka ndani ya chumba cha mahakama baada ya kupata tetesi kuwa nje ya jengo hilo kulikuwa na askari waliotumwa kumkamata. Lakini, baada ya mahakama kufunga shughuli zake, kamanda wa polisi wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alienda mahakamani kumhakikishia kuwa hakuwa amepata maelekezo ya kumkamata na kumsihi aondoke.

Siku mbili baadaye, Lissu alikamatwa akiwa JNIA na kulazwa rumande ya Kituo Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam, kabla ya kupelekwa nyumbani kwake kwa ajili ya kupekuliwa na baadaye Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kuchukua kipimo cha mkojo.

Wakati hayo yakiendelea, polisi walikuwa wakiita waandishi wa habari walioandika habari za tukio lake kwa ajili ya mahojiano.

Kwa mujibu wa Alice, ambaye ni mke wa Lissu, mwanasheria huyo alikataa kutoa kipimo cha mkojo kwa maelezo kuwa tuhuma za uchochezi dhidi yake, hazina uhusiano na mkojo.

Mwanasheria wa Lissu katika shauri hilo, Fatuma Karume aliwaambia waandishi wa habari kuwa wanashangazwa na jinsi Jeshi la Polisi linavyoshughulikia suala la mnadhimu huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni baada ya kuwakatalia kumuona, kukataa kumtoa kwa dhamana na hata kutompeleka mahakamani kama sheria zinavyotaka.

“Hili linatushangaza sana kwa sababu ana haki ya kupata dhamana na kupelekwa mahakamani,” alisema binti huyo wa rais wa zamani wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.

Kitendo hicho kilimfanya Karume na wanasheria wenzake kupeleka ombi la dharura Mahakama Kuu kutaka Mkuu wa Jeshi la Polisi aeleze sababu za kumshikilia Lissu bila ya kumpeleka mahakamani baada ya saa 24 kupita kama sheria zinavyotaka.

Suala hilo pia lilizungumziwa na msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi Barnabas Mwakalukwa wakati alipotembelea ofisi za Mwananchi Communications Limited Ijumaa.

“Mhalifu hajitambulishi kwa chama na tuhuma za uhalifu haziangalii itikadi za chama fulani. Polisi inafanya kazi yake endapo itabaini mhalifu, atakamatwa saa na muda wowote bila kujali yeye ni nani,” alisema Mwakalukwa.

Suala la hekaheka za polisi na Lissu limeibua maswali kwa wanasiasa na wanasheria waliohojiwa na Mwananchi, na baadhi yao kuhisi na kudai kuwa kuna jambo zaidi.

“Kuna kila dalili zinazoonyesha kuwa Jeshi la Polisi linataka kumshtaki Lissu kwa makosa tofauti na uchochezi,” alisema Fatuma Karume alipoulizwa kuhusu sakata hilo jana.

Wakili huyo wa jijini Dar es Salaam alisema kitendo cha polisi kupekua nyumbani kwa Lissu na kuchukua CD sita zinazohusu utafiti aliofanya katika sakata la Mgodi wa Bulyanhulu mwaka1999, ni mkakati wa kutafuta kesi nyingine.

Alisema vitendo vingine vinavyoashiria kumfungulia mashtaka tofauti na ya uchochezi yaliyoelezwa awali ni kutaka kuchukua kipimo cha mkojo, kitu ambacho Lissu alikataa.

Naye mkurugenzi wa itifaki wa Chadema, John Mrema alisema hata kitendo cha kuwahoji waandishi wa habari walioripoti kauli za Lissu kinaonyesha kuwa kuna mkakati wa kutafuta kesi tofauti.

Lissu anatuhumiwa kutoa maneno ya uchochezi wakati alipozungumza na waandishi wa habari na kulaani vitendo vya ukandamizaji wa demokrasia, hasa kukamatwa mara kwa mara kwa viongozi na wanachama wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Pia, kitendo cha kumnyima dhamana na kutompeleka mahakamani baada ya muda wa saa 24 unaotambuliwa kisheria kupita, kumemtia wasiwasi Mrema.

“Lissu ndiyo kiongozi anayeongoza kwa kesi nyingi za uchochezi alizofunguliwa katika Mahakama ya Kisutu, kwa hiyo pengine anaonekana kuwa kikwazo kwa Serikali kwa kuzungumza sana na kufuatilia suala hili la ukandamizaji wa demokrasia,” alisema Mrema.

“Kwa hiyo wanatamani kumfunga bila hata kupitia mahakama lakini tunaamini haki itatendeka.”

Kaimu kamanda wa polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya alisema madai ya kuendelea kushikiliwa na polisi, kupimwa mkojo, kunyimwa dhamana ni sehemu ya upelelezi.

Kamanda Mkondya alisema wataendelea kumshikilia hadi uchunguzi wao utakapokamilika na suala la kupimwa mkojo litatolewa ufafanuzi baadaye.

Lakini, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alisema Jeshi la Polisi linatakiwa kuwa wazi katika kesi ya msingi inayomkabili Lissu kwa kuwa suala hilo linafuatiliwa kimataifa.

Mbunda, ambaye amejikita katika utawala bora, alisema vyombo vya dola na mahakama vimekuwa vikifanya kazi yake kwa mujibu wa sheria, hivyo si sahihi kwa polisi kuwajengea wananchi wasiwasi.

“Polisi inatakiwa kuonyesha weledi wa hali ya juu, kama ni uchochezi iweke wazi ili kuondoa wasiwasi wa kuwapo kwa figisufigisu. Kama ni ule mkutano wa waandishi ielezwe wazi kesi ya msingi itakuwa nini, wachambuzi na media zinafuatilia sana,” alisema.

Wakili wa Kujitegemea wa Mahakama Kuu, Onesmo Mpinzile alitofautiana na wadau wengine akisema dalili hizo zinaweza kuwa ni hofu ya wanasiasa ambayo haina ushahidi, akitoa mfano wa hoja za mbunge wa Ifakara (Chadema), Peter Lijualikali.

Mpinzile alisema polisi kupima mkojo ni kawaida na si kosa kwa kuwa inategemea uchunguzi unaofanyika unataka nini.

Hata hivyo, alisema kitendo cha kumnyima dhamana Lissu si sahihi kwa kuwa kisheria ni haki ya msingi kisheria kulingana na tuhuma dhidi yake. “Kwa nafasi ya Lissu kama mbunge na kiongozi wa Chama cha Wanasheria (TLS), alitakiwa kupewa dhamana. 


Labda polisi waende mahakamani kueleza ni kwa nini hawataki kutoa dhamana, kwamba pengine akiwa nje anaweza kuharibu uchunguzi au kuhofia usalama wake,” alisema.Mwananchi
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: