RAIS MAGUFULI AMWAGIA SI ALIYEKUWA MBUNGE WA KIGOMA KUSINI DAVID KAFULILA
Rais John Pombe Magufuli amempongeza aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila kwa kuliibua sakata la mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kueleza waliombeza na kumuita tumbili watakuwa tumbili wao.
Akiwa anahutubia wananchi wa Nguruka wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, Rais Magufuli alisema: “Kabla sijamaliza napenda kumpongeza Kafulila ambaye alijitolea kuibua sakata la IPTL, wengine wakamwita tumbili kwa kumbeza sasa wao ndio watakuwa tumbili,’’amesema.
Magufuli alisema: “Aliyemwita Kafulila tumbili yeye ndiye tumbili , Kafulila katetee wanyonge hadi wakudhihaki, ila wao ndio tumbili wewe ni mtu safi.
Akiwa bungeni mwaka 2014 ,aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema alizua tafrani akiwa bungeni kutokana na kitendo chake cha kutaka kumpiga Mbunge wa Kigoma Kusini, Kafulila wakati huo akiwa NCCR Mageuzi.
Sakata hilo lilitokea baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu kuahirisha kikao cha Bunge, ikiwa ni muda mfupi baada ya Werema na Kafulila kurushiana maneno bungeni ambako Jaji Werema alichukia baada ya Kafulila kumwita mwizi.
Ilivyokuwa
Hali ilianza kuchafuka wakati Jaji Werema alipokuwa akijibu mwongozo uliombwa na Kafulila kuhusu fedha za akaunti ya Escrow.
Katika mwongozo huo, Kafulila alisema Wizara ya Nishati na Madini kupitia Waziri wake, Profesa Sospeter Muhongo alizungumza uongo mara mbili bungeni kuhusiana na fedha za Akaunti ya Escrow.
“Alisema uongo mbele ya Waziri Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika maeneo mawili, kwamba uamuzi wa kutoa fedha za Escrow kwa IPTL ulikuwa wa Mahakama na Serikali isingeweza kwenda kinyume...” alisema.
Alisema katika hukumu hiyo ya Septemba, 2013 , hakuna mstari hata mmoja unaosema kuwa fedha za Escrow wapewe Kampuni ya IPTL.
“Profesa Muhongo aliliambia Bunge kuwa Serikali ililipa fedha hizo ili kuondokana na kesi hiyo lakini ninazo nyaraka za Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kuteua kampuni mbili za uwakili kwenda kuiwakilisha katika kesi nchini Uingereza,” alisema Kafulila.
Alisema kwamba aliomba mwongozo sababu huo umekuwa mwendelezo wa kuzungumza uongo bungeni... “Naibu Waziri (Nishati na Madini - Stephen Masele), alizungumza uongo bungeni tukaambiwa kuwa wamekutana katika sherehe za kuzaliwa yakaisha, haiwezekani, Bunge ni sehemu ya kuisimamia Serikali.
“Haiwezekani Bunge ling’olewe meno liwe ni chombo ambacho mtu anaweza kuzungumza uongo bila kuchukuliwa hatua kwenye jambo hili ambalo linaligharimu taifa mabilioni ya fedha.”
Baada ya madai hayo, Jaji Werema alisimama na kusema: “Bunge hili liliamua mambo mawili, kwanza kulikuwa na suala la rushwa na CAG apewe kazi ya kuchunguza na kutoa taarifa bungeni. La pili kuna watu walitoa vipeperushi humu bungeni, miongoni mwao ni huyu anayetoa maneno machafu (Kafulila),” alisema Werema na kumfanya John Mnyika (aliyekuwa Mbunge wa Ubungo-Chadema), kuomba mwongozo uliokataliwa na Mwenyekiti Zungu.
Hata hivyo, Mnyika na Kafulila waliendelea kuomba mwongozo, lakini Zungu aliwataka wamsikilize Jaji Werema kwa sababu naye alimsikiliza Kafulila. Werema aliendelea: “Suala la Escrow ni suala linalotokana na wanahisa wawili ambao ni IPTL na Mechmar… Pesa ya Serikali haikai kwenye Escrow.”
Hata hivyo, alikatishwa na kelele za Mnyika ambaye alitaka mwenyekiti kumpa nafasi ya kutoa taarifa. “Sasa kama unataka kuleta mambo ya nje ndani ya Bunge ningojee pale nje,” Jaji Werema alisema wakati wabunge hao walipokuwa waking’ang’ania kutoa taarifa.
Alisema ugomvi huo ulitokana na wanahisa wawili hao kila mmoja akitaka IPTL ifilisiwe ili waachane. Alisema Serikali iliingia katika mgogoro huo kwa sababu ya mikataba ya udhamini na kwamba wakati wanagombana iliamua kufungua akaunti ya Escrow.
Hata hivyo, kuliibuka maneno tena kutoka upande wa Kafulila na Jaji Werema alitaka kusikilizwa hata kama yeye ni mtuhumiwa katika suala hilo.
“…Wanyankole wanasema tumbili hawezi kuamua masuala ya misituni… sikiliza tumbili, sikiliza ‘please’ (tafadhali),” alisema Werema.
Sentensi hiyo iliamsha kelele kutoka upinzani na Kafulila alisikika akimwita Werema mwizi.
Hata hivyo, Zungu alizuia vurumai hizo kwa kumtaka Jaji Werema kukaa na kisha kuwataka wabunge hao wawili kupeleka ushahidi wao Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (Takukuru).
Mara tu baada ya Zungu kuahirisha Bunge, Jaji Werema alisimama na kumfuata Kafulila lakini kabla hajamfikia, mawaziri walimzuia na kumsindikiza hadi nje.Mwananchi
0 comments:
Post a Comment