BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

DAKTARI MKONGWE AFARIKI DUNIA AKIWA NA UMRI WA MIAKA 105

 
Daktari mkongwe wa Kijapani, Shigeaki Hinohara mwenye umri wa miaka 105 ambaye amekuwa akipigania afya ya wazee wenzake amefariki dunia Jumanne Julai 18, 2017 kutokana na mfumo wake wa upumuaji kushindwa kufanya kazi, Joseph Burra anaandika.

Ni mwasisi wa utaratibu wa kupima afya ya mwili mzima (full body medical checkup), harakati za kukabiliana na magonjwa yatokanayo ya mtindo wa maisha (vitambi, lehemu kwenye mishipa ya damu nk).

Pamoja na uzee wake alifanya kazi hadi mwanzoni mwa mwaka huu ikiwa ni miezi michache kabla ya kifo chake akiendelea kuwahudumia wagonjwa akiwa na afya njema kabisa.

Daktari Hinohara alizaliwa mwaka 1911 mkoani Yamaguchi magharibi mwa Japani na alianza kazi ya utabibu wa binadamu mwaka 1941 katika Hospitali ya Kimatifa ya St. Luke cha jijini Tokyo na pia alikuwa akifundisha katika chou
cha uuguzi cha St. Luke.

Baada ya vita Vikuu vya Pili vya Dunia alishiriki kuwatibu majeruhi wa wakati wa vita na wale walioathiriwa na na shambulio ya mabomu ya atomiki.

Dk. Hinohara alishiriki kuboresha hospitali hiyo na Chuo chake cha uuguzi kuwa ya hadhi ya kimataifa kutokana na umahiri wake uliochochewa na ari pamoja na ufahamu wa biashara alifanikiwa kubadilisha taasisi hiyo kuwa hospitali kubwa na chuo bora cha uuguzi nchini Japani.

Amewahi kuwa mwenyekiti wa bodi ya chuo hicho atakumbukwa kama mtu aliyekuwa tayari kujaribu mambo mapya siku zote. Hadi alipofikisha umri wa miaka 75 alikuwa ameshachapisha vitabu 75 kikiwemo kinachojulikana sana cha "Living Long, Living Good" ambacho kimeuza zaidi ya nakala milioni 1.2.

Kitabu hicho cha "Living Long, Living Good" yaani "Kuishi Maisha Marefu, Maisha mema" ambacho kimeuza zaidi ya nakala milioni 1.2 kilichapishwa mwaka 2001.

Kama mwasisi wa harakati za utetezi wa afya ya wazee, Daktari Hinohara amekuwa akiwatia moyo watu kuishi Maisha marefu ya afya na furaha kwa kuzingatia lishe bora na kuepuka aina ya vyakula vilivyo hatari kwa afya ya mwili.

Alihimiza mazoezi na kupima afya zao kila mara huku yeye mwenyewe kama tabibu akionesha mfano bora kwa hayo anayohubiri.

Kama sehemu ya juhudi zake za kukabiliana na magonjwa yatokanayo na mtindo wa maisha alianzisha utaratibu wa uchunguzi wa afya wa mwili mzima mnamo mwaka 1954 katika hospitali hiyo alikokuwa akifanyia kazi.

Ilikuwa hospitali binafsi ya kwanza kuanza kutoa huduma hiyo ya uchunguzi wa afya ya mwili mzima. Alihamasisha jamii akiwataka hasa wazee kushiriki kikamilifu katika mpango huo.

Daktari Hinohara akiendelea kufanya kazi yake ya kutibu watu hata baada ya kutimiza umri wa miaka 100, alipanua shughuli zake hadi kwenye nyanja zingine, Kwa mfano aliwahi kutunga mziki kwa ajili ya watoto akiegemea kwenye kitabu kimoja cha picha kutoka Marekani kinachoitwa "The Fall of
Freddie the Leaf".

Itakumbukwa pia mwaka 1970, Daktari Hinohara alikaa mateka siku nne baada ya ndege aliyopanda kutekwa na watu wenye misimamo mikali. Buriani, Hinohara!
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: