TUNDU LISSU AGANDA CHUMBA CHA MAHAKAMA AKIOGOPA KIVULI CHA POLISI
MWANASHERIA Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu jana alikataa kuondoka chumba cha Mahakama ya Wilaya ya Dodoma, akidai kuwa ana taarifa ya kutakiwa kukamatwa na Polisi ili kupelekwa jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo lililotokea mahakamani hapo jana, lilileta taharuki na kufanya watu wajae mahakamani. Hali hiyo ilitokea mara baada ya kuahirishwa kwa kesi ya Chama cha Walimu Manispaa ya Dodoma (CWT) iliyokuwa inahusu mgogoro wa viongozi wa chama hicho wanaodaiwa kufanya matumizi mabaya ya mali za chama hicho.
Katika kesi hiyo, Lissu alikuwa ni Wakili wa Utetezi upande wa Viongozi wapya. Akizungumza baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo hadi Septemba 27, mwaka huu, Lissu alisema amepata taarifa za kutaka kukamatwa kupitia ujumbe mfupi aliotumiwa na Mkewe toka Dar es salaam ambapo asubuhi askari walifika nyumbani kwake na kujulishwa kuwa yupo Dodoma.
“Sitatoka Mahakamani hapa kama wao wana uwezo na wanafanya kazi kwa maelekezo waje wanikamatie hapa mahakamani, sitoki nitaendelea kunywa maji yangu haya yatanipa nguvu ya kukaa hadi jioni,” alisema Lissu.
Lissu alisema aliamua kubaki mahakamani baada ya kudokezwa kuwa kuna gari linamsubiri nje ya mahakama kupelekwa Dar es Salaam.
Katika mazingira ya mahakama kulikuwa na watu walioonekana kusubiri wakiwa katika mavazi ya kiraia huku gari la Polisi likiwa limeegshwa jirani na lango la kuingilia viwanja vya Mahakama hiyo.
Alipoulizwa anahisi nini chanzo cha kutaka kukamatwa kwake, Lissu alisema anahisi kauli zake za karibuni dhidi ya Rais John Magufuli kuhusu utendaji wake.
Kutokana na Lissu kugomea kutoka mahakamani, alizua taharuki na kusababisha watu kurundikana mahakamani hapo huku gari linalodhaniwa ndilo limeegeshwa kumsubiri likiondolewa mahali lilipokuwepo.
Lissu hadi saa kumi kasoro jioni alikuwa bado ndani ya mahakama hiyo huku akidai kuwa anaandika ujumbe mfupi wa kuwajulisha watu wengine.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alisema anamshangaa Lissu na kwamba Polisi hawana mpango wa kumkamata na wakitaka kumkamata hata mahakamani ndani, wana uwezo wa kumtoa.
“Kama anaogopa polisi, kwanini anazungumza maneno yasiyofaa mbele ya jamii?,” alihoji Mambosasa. Kamanda Mambosasa alimtaka Lissu kutoka, kwani hawana mpango naye na wanashangaa alipozitoa hizo taarifa.
0 comments:
Post a Comment