RAIS Dk. John Magufuli, amesema kuwa suala la maendeleo halina itikadi kwani yanayofanywa na Serikali yake hata mtoto wa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) atanufaika nayo.
Kutokana hali hiyo alisema bado ataendelea kuwafanyia kazi Watanzania, huku akipambana na watu wanaohujumu rasilimali za Taifa.
Kauli hiyo aliitoa jana mjini Itigi Manyoni mkoani Singida, ambapo alisema hatobagua vyama ila kwa sasa Tanzania inahitaji maendeleo ya kweli na si maneno.
Kiongozi huyo wa nchi alisema anashangazwa na baadhi ya watu kupiga kelele wakiwa jijini Dar es Salaam wakati majimbo yao hayana watu wa kuwasemea kwa kukosa maji, umeme na huduma za afya.
“Ukiona makelele yanapigwa ujue ni rushwa waliyopewa na hao watu..kama ni mmoja, wawili watatu ninawaambia wawekeni kiporo ili muwamwage katika uchaguzi ujao.
“Maendeleo ni ya wote awe mtoto wa nani au mtoto wa nani hata mtoto wa Tundu Lissu. Mna matatizo mengi mahosipitali na mengine lakini hamna wa kuwasemea badala yake wanazungumzia ya Dar es Salaam. Acha mkome si mlichagua wenyewe!
“Kosea njia usikikosee kuoa mke, usije pia kukosea kuchagua na kukosea madhara yake ni makubwa. Mwaka 2020 ikifika msikosee tena,” alisema Rais Magufuli.
Pamoja na hali hiyo alisema kama kuna tochi inawaka basi ina betri “Ukiona mtu anapiga kelele ujue kuna kitu amemeza na sio kingine bali ni rushwa, ukiona tochi inawaka ujue kuna betri,” alisema.
Alisema kuhusu ujenzi wa barabara hiyo itatumia na watu wote wakiwemo wanachama wa Chadema, ACT-Wazalendo jambo ambalo siku zote husimamia dhana maendeleo hayana chama.
Hali Serikali
Alisema ndani ya Serikali kuliwa na watu watumbuaji kwa kuwa na safari kila kukicha ikiwemo kufanya semina kila mahali ikiwemo nchi za Ulaya huku Watanzania wakiendelea kuumia kwa kukosa maendeleo.
“Nimeamua kuanza na watu wa juu na ninawatumbua kweli kweli kazi ni ngumu unaweza kutumbua ukakutana na usaha ukakurukia kwenye macho.
“Niombeeni nitumbue salama nisije kutumbua watu ambao hawatakiwi kutumbuliwa,” alisema.
Rasirimali
Alisema kwa muda mrefu Tanzania imeibiwa na wawekezaji kwenye sekta ya madini na amedhamiria kuhakikisha anajenga nchi ya viwanda.
“Ninataka kujenga Tanzania mpya kwani mimi nashindwa nini kuwambia tugawane, hata kiingereza najua ningewaambia ‘give me some ten percent’. Leo mabilioni yale kama ningechukua ningejenga viwanda vyangu Ulaya ningekuwa nasafiri kwenda kuangalia viwanda vyangu, ningejenga hata mahoteli Marekani.
“Wapo Watanzania wamewekeza nchi za nje kwa kujenga mahoteli hata wazazi wao hawana nyumba za kuishi saa nyingine mali zao zitapotea huko huko baada ya wao kufa, huo ndio ukweli.
“…mimi nimezaliwa hapa (Tanzania) nitafia hapa na nitazikwa hapa kwa sababu tumeumbwa maisha yetu na muda wake. Lakini ninataka niwatendee haki Watanzania bila kuwadanganya nitawaeleza ukweli. Unapokuwa Rais unajua siri nyingi nami nimeumbwa kwa ajili ya kuwatetea na ndio maana ninausema ukweli hadharani na sitaacha,” alisema Rais Magufuli.
Akizungumzia historia ya Mkoa wa Singida, alisema anaifahamu tangu akiwa Waziri wa Ujenzi ambapo mkoa huo ulikuwa na kilometa tatu tu za lami na hadi sasa ina kilometa 495 za barabara za lami.
Alisema ni vyema Watanzania wakawa na utaratibu wa kukumbuka walikotoka kwa kukumbuka historia ambapo yeye anaifahamu vizuri Singida enzi za Rais Benjamin Mkapa na Rais Dk. Jakaya Kikwete ambao alishiriki nao kujenga mkoa huo.
“Historia ya maisha yetu, mapambano yetu…tusiyapuuze na tuwe wepesi wa kukumbuka tulikotoka na mahala tuendako hii itasaidia kujenga mazingira mazuri kwa vijana wetu wanaozaliwa sasa,” alisema Magufuli.
Alisema wakati huo kutoka Mkoa wa Dodoma kwenda Manyoni ilikuwa ni shida ambapo barabara zilikuwa mbovu kiasi cha kusababisha abiria kulala njiani huku wagonjwa wakifia njiani.
“Wapo ambao ndugu zao walikufa au kulala njiani lakini cha ajabu leo hii wamesahau ndio maana ninasema tuwe wepesi wa kukumbuka historia ya maisha yetu,”alisema Magufuli.
Alisema katika ziara yake aliyoanzia Biharamulo amezindua mradi wa ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilometa 707 ambazo zitagharimu Sh bilioni 860 zitakazotolewa na Serikali kuu kwa asilimia 100 .
“ Katika fedha hizi hakuna hata senti ya mfadhili , niliamini mkinipa kazi hii nitafanya kwa moyo wote nimeamua pia hata vile vipande vingine vilivyobaki navyo vitengenezwe kwa lami ambavyo ni vya kutoka Itigi hadi Tabora,”alisema Magufuli.
Alisisitiza anafanya hivyo ili wananchi wapate unafuu wa safari na kuondokana na vumbi kama ilivyo hivi sasa.
“ Haiwezekani mtu akatoka Dar es Salaam akapata lami akifika Itigi hadi Tabora apate vumbi afike amechakaa na mchumba wake au mkewe sikubali hali hii hivyo hata kile kipande cha Chaya hadi Nyahua cha kilometa 85 nazo zitengenezwe kwa kiwango cha laimi,”alisema Magufuli.
Alisema ametoa mwezi mmoja na nusu kwa viongozi wa mkoa huo kuhakikisha kunafanyika matengenezo kwa kiwango cha lami.
MRADI WA UMEME
Magufuli alisema katika kuhakikisha Tanzania ya viwanda inafanikiwa wameamua kuweka umeme katika vijiji mbalimbali hapa nchini.
Alisema hauwezi kukamilisha ndoto za uchumi wa viwanda kama hakuna umeme wa uhakika kwani hata kiwanda kidogo cha kutengeneza makopo au kuchomelea vyuma nacho kinahitaji umeme pia.
Aliongeza kuwa katika kutekekeza mkakati huo anafanya kila jitihada fedha zinazokusngwa badala ya kutumika ovyo na wakubwa zinatumika kujenga uchumi wa wananchi wa kawaida.
“Tumeanza mwanzo mzuri kwani hadi sasa Tanzania ni miongoni mwa nchi chache Afrika zinazofanya vizuri kwa kusambaza umeme kwa wananchi wake kwa asilimia 45 wakati nchi nyingine zimefikisha asilimia 2.7,”alisema Magufuli.
Alisema lengo kuu la Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika ambapo katika mradi wa umeme vijijini utasaidia kuongeza hadi kufikia asilimia 50 ya wananchi wake.
“Katika kutekeleza adhima yetu ya Tanzania ya viwanda tutajitahidi kuongeza vyanzo vya uzalishaji vya umeme ambapo bwawa la kuzalisha umeme ambapo kwa sasa tuna megawati 1,460 na tukiongeza na bwawa litaongeza megawati 2,100 ambao utaunganishwa moja kwa moja kwenda mkoani Singida na maeneo mengine ili wananchi wapate umeme wa uhakika,”alisema Magufuli.
Alisema serikali imejipanga kuongeza vyanzo vya umeme ili angalau kufikia asilimia 56 ya wanufaika wa umeme.
Magufuli alisema awali alikuta makusanyo ya mapato kwa mwezi ni Sh bilioni 800 lakini kwa sasa baada ya utumbuaji na kuwabana wale wakwepa kodi kwa sasa imefika hadi Sh trilioni 1.3 kwa mwezi.
Rais alirejea kauli yake akisema kamwe Serikali haitatoa chakula kwa mkoa utakaokumbwa na baa la njaa na badala yake viongozi wa mkoa huo watawajibishwa.
“Wilaya ikiwa na njaa nitajua wewe mkuu wa mkoa hufai, mkuu wa wilaya hufai. Mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya atakayeshindwa kuwahamasisha watu wake wafanye kazi, hafai kuwa kiongozi,” alisema.
Amewataka wakuu wa mikoa kuwaondoa katika nafasi zao makatibu tarafa ambao hawahamasishi kilimo.
“Ikiwezekana na wewe mkuu wa wilaya au mkoa kama unakaa kijijini au ni katibu kata onyesha mfano wako wa kazi. Ukiwa diwani, hivyo hivyo, ukiwa mbunge hivyo hivyo.
Ndiyo maana ninatimiza wajibu wangu wa kuhamasisha watu, chapa kazi, hapa kazi tu,” alisema.Mtanzania
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment