14 ZATINGA 16 BORA MASHINDANO YA RWAKATARE CUP 2017 KILOMBERO
Mchungaji Dk Getruda Rwakatare akipiga mpira na kufunga bao wakati akizindua mashindano ya Rwakatare CUP 2017 uwanja wa Lukolonga Mngeta wilaya ya Kilomero Morogoro hivi karibuni/Picha na Juma Mtanda.
Juma Mtanda, Morogoro.
Jumla ya timu 14 zimefuzu na kutinga hatua ya 16 bora ya mashindano ya soka ya Rwakatare Cup 2017 baada ya kufanya vizuri katika michezo iliyokuwa ikipigwa kwenye vituo saba vya mashindano hayo kwa kusaka timu mbili za kuingia kucheza fainali hizo zinazofanyika katika wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro.
Mashindano hayo yameshirikisha jumla ya timu 80 na kugawanywa katika vituo saba huku kila kituo kikitoa washindi wawili wataoingia kwenye hatua ya michezo ya 16 bora na timu mbili zikiingia kwa njia ya upendeleo ambapo fainali yake itachezwa kwenye uwanja wa shule ya msingi Mchombe kijiji cha Mngeta mkoani hapa.
Akizungumza na MTANDA BLOG mjini hapa, Msimamizi mkuu wa kituo cha Mngeta, Supertus Duma alisema kuwa timu 14 zimefuzu na kutinga hatua ya 16 bora baada ya kushika nafasi ya kwanza na pili katika ligi ya kusaka wawakilishi wa kutinga hatua hiyo kutoka kwenye vituo sita huku kituo cha Mang’ula kikisubiriwa kutoa wawakilishi wake.
Vituo hivyo ni pamoja na Namawala, Mlimba, Mkamba, Ifakara, Mang’ula, Mngeta na Chita.
Duma alitaja timu zilizotinga hatua ya 16 bora kuwa ni pamoja na Teachers FC, Street Boys FC na Mlimba City FC kutoka kituo cha Mlimba wakati kituo cha Mngeta ni City Boys FC, Super Mahakama FC na Mngeta Rangers FC zilipenya huku kituo cha Chita ikitoa timu za Express FC na JKT Chita FC.
Nyingine ni Kidatu Kijiweni FC, Serengeti Boys kutoka kituo cha Mkamba, timu za Mlabani FC na Shupavu FC zikikata tiketi kutoka kituo cha Ifakara wakati katika kituo cha Namawala ni Idete FC na Namawala FC.
“Timu 14 tayari zimefuzu na kuingia kwenye hatua ya michezo ya 16 bora ya Rwakatare Cup 2017 baada ya vituo sita kumaliza michezo ya kusaka timu mbili za kuingia hatua hii ya 16 bora na tumebakiwa na kituo kimoja tu cha Mang’ula ambacho mpaka sasa tunatarajia kupata wawakilishi wao septemba 20 ambao wapo hatua ya michezo ya nusu fainali.”alisema Duma.
Duma alisema kuwa kituo cha Mang’ula ndicho kinachasubiriwa ili kupata wawakilishi wao wa kuungana na timu za vituo 14 kisha kamati ya mashindano itakaa na kutoa siku 10 za maandalizi kwa timu zote zilizofuzu kukusanya nguvu mpya kabla ya kupanga ratiba ya hatua hiyo ya 16 bora itayoanza kwa mtoano ili kupata timu nane zitakazo kutinga robo fainali, nusu fainali na fainali yenyewe.
Timu zilizoingia hatua ya nusu fainali kituo hicho cha Mang’ula ni Mbasa FC, Mwaya B FC, Toto Boys Kiswanya FC na Mkula FC wataochuana ili kupata timu mbili za kuingia kwenye hatua ya 16.
0 comments:
Post a Comment