HAWA NDIO MADAKTARI 10 WALIOTUMIA SAA 10 DODOMA KUOKOA UHAI WA TUNDU LISSU BAADA YA KUPIGWA RISASI
Jumla ya madaktari bingwa 10 walitumia saa 10 kwa ajili ya kunusuru maisha ya Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu akiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma hadi Uwanja wa Ndege kabla ya kusafirishwa Nairobi.
Muda huo ulijumuisha tangu Lissu alipopigwa risasi saa 7:30 mchana Septemba 7, 2017 akiwa nyumbani kwake mtaa wa Area D mjini hadi aliposafirishwa kwenda Nairobi nchini Kenya saa 6:17 usiku.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk James Kiologwe akizungumza na Mwananchi amesema lilikuwa tukio lenye changamoto zake.
“Nina timu nzuri kwa maana nina uongozi mzuri wa hospitali ya mkoa lakini nina madaktari na watoa huduma ambao wana ‘commitment’ ya hali ya ajabu,” amesema.
Amesema wakati tukio hilo linatokea yeye alikuwa mbali kidogo na hospitali lakini baada ya kupata taarifa na kufika alikuta tayari Lissu ameshaanza kuhudumiwa.
“Tulikuwa na timu ya zaidi ya watu 20 ambao walishiriki kwa njia mbalimbali. Unajua kuna ushiriki wa moja kwa moja na usio wa moja kwa moja. Kwenye macho ya watu huwa anaonekana daktari pekee lakini ukweli ni kwamba hawezi kufanya kazi pekee yake lazima wawepo watu wengine,”amesema.
Amesema kati ya timu hiyo 10 walikuwa ni madaktari bingwa katika fani mbalimbali walikuwa kazini wakati huo ambao Lissu anafikishwa hospitalini baada ya kuumia.
Pia katika timu hiyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya ambaye ni mtaalam bingwa wa usingizi alishiriki hadi saa 6.17 usiku Uwanja wa Ndege wa Dodoma kabla ya Lissu kwenda jijini Nairobi nchini Kenya.
Hata hivyo, amesema walikuwa na vitendea kazi vya kutosha na ndio maana walisema kuwa wanaweza kumhudumia mgonjwa huyo.
“Jambo hilo halikuwa na nia ya kuwatuliza watu hapana, bali lilikuwa linamaanisha kuwa uwezo tunao kweli,”amesema“Ni kweli tukio kama lile lilikuwa na changamoto zake. Changamoto ya kwanza ni tukio ambalo limewagusa watu wengi sana kisaikolojia.
Watu wengine wangependa kumuona mgonjwa kwa hiyo mwananchi anaweza kukimbia kuja kumuona,” amesema.
Hata hivyo, amesema hawakuweza kuwaruhusu kwa sababu za kiutaratibu ambapo kwa muda huo madaktari wanahitaji zaidi kuokoa maisha ya mgonjwa.
“Suala la kumuona na kujua ameumiaje wakati huo hauwezi kumsaidia kwa wakati huo halikuwa muhimu. Niwashukuru sana wananchi wa Dodoma pamoja na viongozi walikuwa ni wasikivu unapowapa maelekezo walikuwa wanatekeleza,”amesema.
Amesema walipata ushirikiano wa hali ya juu kutoka kwa watu mbalimbali wakati wa tukio hilo jambo ambalo liliwasaidia katika utekelezaji wa kazi hiyo.Mwananchi.
0 comments:
Post a Comment