JAHAZI LA MAWENZI MARKET LAENDELEA KUYUMBA LIGI DARAJA LA KWANZA MOROGORO
Mlinzi wa klabu ya Mawenzi Market FC, Abdallah Kulandana (chini) akichuana na mshambuliaji wa Polisi Tanzania SC, Hamad Kambanga wakati wa mchezo wa ligi daraja la kwanza Tanzania bara uliopigwa kwenye uwanja wa jamhuri Morogoro na Mawenzi Market FC kukubali kipigo cha bao 2-1.Picha na Juma Mtanda.
NA JUMA MTANDA, MOROGORO.
Jahazi la klabu ya Mawenzi Market FC limeendelea kukumbwa na mawimbi na kushindwa kuhimilia mikikimikiki ya ligi daraja la kwanza Tanzania bara baada ya kukubali kupokea vipigo viwili mfululizo kutoka kwa KMC FC na Polisi Tanzania SC katika uwanja wake wa nyumbani wa jamhuri mkoani Morogoro.
Mawenzi Market FC ilianza mchezo wa ufunguzi wa ligi hiyo kwa kutandikwa bao 2-1 kutoka kwa KMC FC ya Temeke jijini Dar es salaam kisha kupoteza mchezo mwingine dhidi ya Polisi Tanzania SC (Zamani Polisi Morogoro SC) na kujikuta ikiwasononesha mashabiki wake.
Katika mchezo wa jana (Juzi) Mawenzi Market FC ilishindwa kutumia vyema uwanja wake wa nyumbani kufuatia kukubali kipigo cha bao 2-1 kutoka kwa Polisi Tanzania baada ya mshambuliaji. Hamad Kambanga kuandika bao la kuongoza dakika ya nne na, Benedict Elias kufunga bao la pili na ushindi dakika ya 27.
Mshambuliaji wa Polisi Tanzania SC, Hamad Kambanga alikuwa mwiba mkali katika safu ya ulinzi ya Mawenzi Market FC kwa kutoa pasi ya bao la pili baada ya kuichambua ngome ya wapinzani wao kila wakati.
Hassan Mkota aliifungia bao la kufutia machozi Mawenzi Market FC dakika ya 40 huku kipindi cha pili wakitandaza soka la kushambulia na kutengeneza mashambulizi mengi lakini walishindwa kufumania nyavu.
Kutokana na vipigo hivyo, Mawenzi Market FC imejikuta ikipoteza mwelekeo na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne huku wenyewe wakifunga bao mbili huku wakishindwa kuvuna pointi yoyote.
Kocha msaidizi wa klabu ya Mawenzi Market FC, Mohamed Diego alisema kuwa wamekuwa wakifanya maandalizi mazuri lakini wamekuwa wakikosa bahati ya kuiuka na ushindi licha ya kuwa wageni katika ligi daraja la kwanza.
Kwa upande wa kocha mkuu wa Polisi Tanzania SC, John Tamba alisema kuwa benchi la ufundi wamefurahishwa na ushindi huo.
Tamba alisema kuwa Polisi Tanzania imevuna pointi nne katika michezo yake miwili huku wakitoa sare ya bao 1-1 dhidi ya JKT Mlale FC na kuisambaratisha Mawenzi Market FC bao 2-1.
0 comments:
Post a Comment