BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KIPIGO CHA BAO 2-1 CHAWAKOSESHA MAWENZA MARKET FC DONGE LA SH800,000 KUTOKA KWA ABOOD

Mbunge wa jimbo la Morogoro Mjini, Abdullaziz Abood akizungumza na wachezaji wa klabu ya Mawenzi Market FC kabla ya kuingia kipindi cha pili wakati wa ligi daraja la kwanza Tanzania bara dhidi ya KMC FC ya Kinondoni Dar es Salaam uwanja wa jamhuri Morogoro. Picha na Juma Mtanda.

Juma Mtanda, Morogoro.
Klabu ya Mawenzi Market FC imeanza vibaya ligi daraja la kwanza Tanzania bara kwa kipigo huku wachezaji wakikosa kupata zawadi ya sh800,000 kutoka kwa mbunge wa jimbo la Morogoro Mjini baada ya kutandikwa bao 2-1 na KMC FC katika mchezo mkali wa ufunguzi wa ligi hiyo uliopigwa uwanja wa jamhuri mkoani hapa.

KMC FC yenye maskani yake wilaya ya Kinondoni katika jiji la Dar es Salaam iliitambia Mawenzi Market ya Morogoro kwa mkongwe, Stephen Mwasika kufungua akaunti ya mabao kwa kupachika bao la kwanza dakika ya nne kufuatia kupokea pasi ya, Augustino Samson na Cliff Anthony akihitimisha kwa kufunga bao la pili na ushindi dakika ya 84.

Bao la Mawenzi Market FC lilipatikana dakika ya 51 lililofungwa na, Maulid Iddy na kufanya mchezo huo kumalizika kwa KMC FC kuibuka na ushindi wa bao 2-1.

Baada ya kumalizika kwa kipindi cha kwanza huku KMC FC ikiingiza kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wakiongoza kwa bao 1-0, kulimlazimu Mbunge wa jimbo la Morogoro Mjini, Abdullaziz Abood kuongea na wachezaji wa Mawenzi Market FC kuwataka waibuke na ushindi katika mchezo na kutoa zawadi ya sh800,000.

Chezeni kwa kujituma ili kusawazisha bao lao kisha msake bao la ushindi na kama mkiibuka na ushindi nitatoa sh800,000 kama zawadi kwa wachezaji, alisema Abood muda mfupi kabla ya kuanza kipindi cha pili.

Baada ya mapumziko, Abood alienda jukwaa la kusini, jukwaa linalopendwa na Mwanamuziki Afande Sele na kuwaomba mashabiki hao kuipa sapoti klabu ya Mawenzi Market FC kama njia ya kuwapa hamasa wachezaji katika uwanja wao wa nyumbani na wafanye vizuri kwenye michezo yao.

Mchezaji wa KMC FC, Cliff Anthony ndiye aliyetibua dili la wachezaji wa Mawenzi Market FC la kuambulia japo ya nusu ya fedha hizo kutoka kwa Abood baada ya kufunga bao la pili dakika ya 84 baada ya kupokea pasi ya Stephen Mwasika na kujaza mpira kimiani.

Baada ya dakika 90 na mwamuzi wa kati, Ahmed Seif kutoka Pwani kupuliza filimbi ya kumaliza mchezo huo, mashabiki wa Mawenzi Market FC walishindwa kuamini matokeo hayo na kurusha lawama kwa benchi la ufundi kwa kushindwa kuwaingiza wachezaji wenye kasi.

Kocha msaidizi wa Mawenzi Market FC, Mohamed Diego alisema kuwa kipigo hicho kimetokana na ugeni katika ligi daraja la kwanza na kuahidi kufanya kupata matokeo mazuri katika mchezo ujao dhidi ya Polisi Tanzani SC.

Kwa upande wa mkuu wa KMC FC, Fred Felix Minziro alisema kuwa amefurahishwa na vijana wake kuibuka na ushindi licha ya Mawenzi Market FC kuonyesha upinzani mkubwa na kutandaza soka la kuelewana.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: