WAKULIMA WATATU WASHAMBULIWA NA KUUAWAW BAADA YA MIFUGO KUKAMATWA NA KUTOZWA FAINI MOROGORO
Morogoro. Wakulima watatu wakazi wa Kata ya Kolero wilayani Morogoro wameuawa kwa kupigwa walipokamata mifugo iliyokuwa inalishwa kwenye mazao yao.
Diwani wa Kata ya Kolero, Eligius Mbena amesema Alhamisi Septemba 28 ng’ombe zaidi ya 140 waliingizwa kwenye mashamba ya wakulima katika Kijiji cha Kidodi na kula mazao.
Ng’ombe hao ambao inadaiwa ni mali ya mfugaji mmoja inaelezwa wameharibu zaidi ya eka tano za mazao ya mahindi, kunde na mbogamboga yaliyokuwa yakikaribia kukomaa.
Diwani huyo amesema baada ya wakulima kuona kundi la ng’ombe waliamua kuwasiliana na mtendaji wa kata ambaye alituma mgambo na kwa kushirikiana na wananchi waliondoa mifugo hiyo na kuipeleka ofisi ya kata.
“Baada ya mgambo kufika wale vijana waliokuwa wakilinda ng’ombe walikimbia ndipo wananchi na mgambo walipowaswaga ng’ombe hadi ofisi ya Kata ya Kolero kwa hatua zaidi,” amesema.
Amesema kwa utaratibu waliojiwekea, ng’ombe wanapokamatwa kwenye mashamba hutozwa faini ya Sh10,000 kwa kila mmoja. Mbena amesema mtendaji ndivyo alivyofanya kwa mifugo hiyo iliyokamatwa.
Amesema baada ya mhusika kulipa faini na kukabidhiwa ng’ombe wake, wananchi waliondoka na wakiwa njiani walishambuliwa.
Amewataja waliouawa kuwa ni Richard Edward, Riziki Juma na Antoni Matei ambao ni wakulima na wakazi wa Kata ya Kolero.
“Ninachosikitika ni kwamba, taarifa za mauaji haya tumezitoa katika mamlaka zote za wilaya na mkoa tangu Alhamisi Septemba 28 lakini hadi leo Jumamosi hakuna hatua iliyochukuliwa japo mwenye mifugo tunamjua na tumewatajia polisi,” amesema Mbena.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo alisema hawezi kuzungumzia lolote kwa kuwa masuala ya mauaji yanahusu Jeshi la Polisi na si ofisi yake.
“Msemaji wa matukio yote ya mauaji ni RPC si mimi,” alisema Chonjo.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leons Rwegasira alisema wamepata taarifa hizo na wametuma timu kufuatilia.
“Tuna taarifa kwamba kuna watu wameuawa Kolero lakini bado hatujapata kwa usahihi kwa kuwa timu yetu ndiyo imekwenda huko,” amesema.Mwananchi
0 comments:
Post a Comment