DEREVA WA TUNDU LISSU ANA MAJIBU KWA JESHI LA POLISI
Jeshi la Polisi nchini limesema bado linamhitaji dereva wa Mbunge wa singida Mashariki, Tundu Lissu, ili aweze kutoa majibu ya maswali mengi juu ya tukio la mbunge huyo kupigwa risasi mjini Dodoma Septemba 7, mwaka huu.
Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Simon Sirro amesema hayo leo Jumatano mkoani Mtwara, wakati akizungumza na waandishi wa habari na kuongeza kuwa upelelezi wa tukio hilo bado unaendelea ili kukamilisha uchunguzi.
“Chadema (Chama cha Demokrasia na Maendeleo), wanasema yule dereva anapatiwa matibabu ya kisaikolojia nchini Kenya, wakati kila siku kwenye mitandao tunaona picha zake anawaka tu hii inatupa wasiwasi kwa kuwa majibu ya maswali mengi tuliyo nayo anayo yeye, kwa sababu haiwezekani aendelee kupiga picha na kung’aa vile lakini wanasema ameathirika kisaikolojia, ” amesema IGP Sirro.
Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, alisema dereva huyo yuko nchini Kenya anapatiwa matibabu ya kisaikolojia baada ya kushuhudia tukio hilo la Lissu kushambuliwa kwa risasi wakiwa pamoja kwenye gari.
Lissu bado anatibiwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya baada ya shambulio hilo.
0 comments:
Post a Comment