BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WILAYA YA UKEREWE ONDOENI AIBU YA WANAFUNZI KUPATA MIMBA MASHULENI

Inasikitisha, inauma. Kwa mtu yeyote makini na mpenda maendeleo, lazima aguswe anaposikia taarifa za hali ya ujauzito kwa wanafunzi wa kike wilayani Ukerewe.

Mimi sikusikia tu taarifa, lakini nimejionea mwenyewe mazingira ya kisiwa hiki kilichopo ziwa Victoria mkoani Mwanza.

Ukerewe iliyosifika kwa uchawi kama baadhi ya watu walivyodai miaka ya nyuma, leo inaingia katika orodha ya maeneo yanayoongoza kwa wanafunzi kujazwa mimba.

Ni jamaa, ndugu, marafiki wanaofanya haya. Wanajuana japo baadhi hawataki kutajana. Wakati Serikali ikijihimu kuboresha hali ya elimu ikiwamo kutoa bure fursa ya elimumsingi, baadhi ya wanufaika wanafifisha jitihada hizi.

Wanakubali au wanalazimishwa kupata ujauzito. Huu kwangu ni sawa na ubadhirifu wa fedha za Serikali inayotumia fedha nyingi kuwekeza katika elimu wilayani hapo.

Pengine una shauku ya kujua ukubwa wa tatizo; ni hivi taarifa za kiserikali zinaonyesha kuwa kutoka Januari hadi Septemba mwaka huu, wanafunzi 118 wamepata ujauzito. Kati yao 110 ni wanafunzi wa sekondari na nane kutoka shule za msingi.

Kwa taratibu za kielimu nchini, wanafunzi hawa wameshajifukuzisha shule. Kama walifikiri kuna watetezi wa kuwataka warudi shule, wajue wameula wa chuya!

Hii si taarifa ya kufurahisha ndio maana neno la kwanza katika makala haya niliandika; ‘inasikitisha’. Unaweza kujiuliza ni wataalamu wangapi nchi yetu itawakosa ikiwa wasichana hawa hawatopata tena fursa ya kujiendeleza kielimu

Wanafunzi 118 siyo idadi ndogo, humo kunaweza kuwapo wahandisi, walimu, wanasheria na wataalamu wengineo.

Kwa nini haya yatokee Ukerewe, eneo lenye baraka ya kuwa na viongozi na wasomi maarufu nchini? Hivi wasichana hawa wameshindwa kuwachukulia kina mzee Pius Msekwa, Balozi Getrude Mongella na wengineo kama viigizo vyao maishani na kuwa chachu ya kujikita katika elimu badala ya mapenzi?.


 Walipokuwa wakisoma, walimu hawakuwasimulia habari za watu hawa kama mbinu mojawapo ya kuwapa hamasa kuwa hata nao wanaweza kufika mbali kielimu na kimaisha?

Wazazi nyumbani hawawajui kilichowafikisha mbali wana-Ukerewe wenzao hawa?

Simuoni wa kumuokoa msichana wa Ukerewe zaidi ya mzazi, Je, tuwalaumu walimu? Tuilaumu Serikali kwa kutojenga mabweni? Kwa hali ya Ukerewe, hata kukiwa na mabweni mpaka chekechea, mimba hazitokosekana. Wana- Ukerewe wakumbuke kupanga ni kuchagua. Mnataka kuchagua nini kwa ajili ya maisha ya watoto wenu?

Nilipowauliza baadhi ya wananchi kuhusu uchawi kutamalaki kisiwani hapo, wapo waliosema hayo ni mambo ya zamani; wapo waliosema sio kweli. Lakini vipi taarifa kuhusu mimba kwa watoto wenu? Je, hizi nazo ni taarifa za kusingiziwa?

Wana-Ukerewe mnahitaji kubadilika hasa wakati huu ambao Serikali imeamua kwa dhati kuwekeza katika elimu. Nikiwa kisiwani hapo hivi karibuni, macho yangu yalishuhudia uwekezaji mkubwa wa miundombinu ikiwamo vyumba vya madarasa na mabweni katika shule kadhaa za sekondari na msingi.

Ni majengo ya kisasa yanayojengwa kupitia mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo (P4R), chini ya uratibu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Wana-Ukerewe mnataka nini kutoka serikalini? Kama Serikali inajiongeza kwa kiasi chake, nanyi jiongezeni ili mdhibiti mimba kwa watoto wenu.

Mimba 118 kwa miezi tisa pekee sio idadi ndogo. Lazima kazi ifanyike ili kuzifanya mimba hizi kuwa historia.

Inasikitisha kuwa hata vyombo vya dola vinapotaka kuchukua nafasi yake, wazazi ndio wanaoongoza kuwaficha wahusika na kukataa kutoa ushirikiano.

Wapo wazazi wanaowataja wahusika leo, lakini kesho wanaruka na hivyo kurudisha nyuma jitihada zinazofanywa na vyombo kama vile Jeshi la Polisi na Mahakama. Huku ni kupalilia vitendo vya mimba.

Ndiyo maana naunga mkono hatua za Serikali wilayani hapo kuwatia nguvuni wazazi wa wanafunzi wanaopata mimba.

Hata hivyo, nguvu za dola pekee hazitofua dafu katika mapambano haya ikiwa Wana- Ukerewe hamtokuwa tayari kuwalea na kuwalinda watoto wenu dhidi ya wanaume wakware.

Msione aibu, kaeni kitako na watoto wenu na waelezeni kinagaubaga kuhusu elimu ya makuzi, afya, stadi za maisha na kujitambua. Na huu usiwe wajibu wa kinamama pekee, bali uwe pia wajibu wa kinababa, jamaa na jamii ya Ukerewe kwa jumla.

Msitumie mila na desturi kama kikwazo cha kina baba kukaa na watoto wa kike kwa kisingizio kuwa elimu ya uzazi ni masuala ya aibu.

Ipi hasa ni aibu kati ya kukaa na mtoto wako huku ukimfunda kuhusu maisha na kuletewa mjukuu asiye na baba nyumbani?.Mwananchi
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: