![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgWXYzaaTrQmwlCJhBvnAefht6IwAeeseIQuRR1Ytbh4NO5QMjIe-Kzlf6kf37Hmoj8jJfbDDeehwbvm5MiMYnNkpjsf_iIRl0GHdCO5Zh39btQhUl5iFQ4YxqG2htXCoPkowaxz0HwMGo/s640/MASHINDANO+YA+MAGARI+PIX+NO+111.jpg)
Juma Mtanda, Morogoro
Makamu wa rais wa chama cha mbio za magari Tanzania (AAT), Satinder Singh Birdi amewataka waandaaji wa mashindano ya mbio za magari mwaka 2018 kuchezesha mbio hizo kwenye eneo la barabara zenye usalama zaidi kama chama cha mchezo huo duniani kilivyoagiza.
Akizungunza na gazeti hili mjini hapa, Birdi alisema kuwa chama cha dunia cha mbio za magari kinawataka waandaaji wa mbio za magari kuchezesha katika eneo la barabara binafsi au zilizotengwa kwa mchezo huo ili kuondokana kabisa kutumia barabara za umma lengo likiwa kuepukana na changamoto za mwingiliano.
Birdi alisema kuwa kuanzia sasa waandaaji wote wanapaswa kufuata na kuiga mfano wa mashindano ya mzunguko wa saba wa mbio za magari ya Mount Uluguru Morogoro 2017 ambazo zimechezeshwa kwenye eneo binafsi la barabara za mashamba ya Mtibwa wilayani Mvomero.
“Chama cha dunia cha mbio za magari kinatutaka michezo yetu kuchezwa kwenye eneo la barabara zilizo salama na klabu ya Mount Uluguru Rally 2017 wameonyesha njia na mfano wa kuigwa kwa kuchezesha mbio za magari kwenye eneo la barabara za mashamba ya Mtiwa na mwaka 2018 waandaaji wote wanapaswa kuiga mfano huo.”alisema Biridi.
Birdi alisema kuwa michezo wa mbio za magari ni mchezo wa hatari hivyo kuepukana na barabara za umma kutapunguza changamoto nyingi kwa madereva, mashabiki na watumiaji wa barabara hizo za umma ukiwemo mwingiliano wakati mashindano yakiendelea ambao husababisha usumbufu.
Katika mashindano ya mbio za magari ya Mount Uluguru Morogoro 2017 ya mzunguko wa saba yalihitishwa mkoani Morogoro desemba 16 na 17 mwaka huu kwa klabu ya Birdi Rally kutwaa ubingwa wa mbio hizo za kilometa 164.
Mwenyekiti wa klabu ya chama cha mbio za magari Mount Uluguru Morogoro, Dk Mossi Makau alisema kufanyika kwa mchezo huo kwenye eneo binafsi la barabara za mashamba ya Mtibwa kumepunguza changamoto nyingi za mwingiliano kwenye barabara za michezo.
Dk Makau alisema kuwa moja ya faida kubwa kuchezesha michezo kwenye eneo hilo la barabara za Mtibwa, madereva kuwa huru na kuelekeza akili kwenye mashindano pekee tofauti na changamoto za mwingiliano kwenye barabara za umma.
“Tumefanikiwa kuchezesha mbio hizi za Mount Uluguru Morogoro 2017 kwa 100%, kwanza tumefanikiwa kuwatengea sehemu maalumu mashabiki na yenye usalama ili kuona vizuri mbio hizi pia madereva walielekeza akili mashindanoni na hakukuwa na mwingiliano kutokana na eneo la barabara ya mashindano kufungwa na kuzuia baiskeli, pikipiki na magari ya watu binafsi kuingia.”alisema Dk Makau.
Mratibu wa mbio hizo, Faheem Aloo alisema kuwa mbio za Mount Uluguru Rally Morogoro 2017 zimefanyika kwa siku mbili ikihusisha mbio za kilometa 1.55 na kilometa 164.
Aloo alisema kuwa katika mbio za kwanza zilifanyika uwanja wa Tumbaku Manispaaa ya Morogoro, klabu ya Mkwawa Rally chini ya dereva, Ahmed Huwel na msaidizi wake, Gavin Lawrence walimaliza mbio hizo kwa muda wa dakika 1:54 wakitumia gari aina ya Ford Proto zikishirikisha klabu 15.
Kwa upande wa mbio za kilometa 164 zilizofanyika eneo la barabara za mashamba ya Mtibwa wilayani Mvomero, dereva machachari wa klabu ya Birdi Rally ya Dar es Salaam, Randeep Birdi na msaidizi wake, Zubeyr Piredina walishinda taji la mbio hizo baada ya kutumia muda wa saa 1:06:04 kwa kumaliza mbio hizo kwa mizunguko sita za kilometa za kilometa 164 wakiwa na gari aina ya Mitsubishi Evolution 9.
Aloo alisema kuwa katika mbio hizo klabu 16 ziliingia kwenye kinyang’anyiro cha kusaka ubingwa lakini gari sita zilishindwa kuendelea na mashindano kutokana na hitilafu katika upande wa gia boksi na injini.
“Madereva sita wameshindwa kuendelea na mbio baada ya gari zao kupata matatizo kwenye gia boksi na injini na kati yao ilipinduka na kubakia gari 10 zilizoendelea na mashindano na kumaliza na kupatiwa zawadi ya vikombe kulingana na nafasi zao.”alisema Aloo.
Mmoja wa mashabiki wa mbio hizo, Aziz Msuya alisema kuwa kuharibika kwa magari ya Ahmed Huwel wa klabu ya Mkwawa Rally Iringa, Jamal Khan wa klabu ya Kobil Rally ya Dar es Salaam kumewakosesha furaha sehemu ya mashabiki wengi na kukosa uhondo na ujuzi wao katika kutimua vumbi.
0 comments:
Post a Comment