MAKOSA DHIDI YA BINADAMU YAONGEZEKA YAMO YA KUBAKA, KULAWITI NA KUNAJISI TANZANIA
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limesema makosa dhidi ya binadamu yanayojumuisha mauaji, kubaka, kulawiti, kunajisi, wizi na kutupa watoto na usafirishaji binadamu yameongezeka nchini.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz amesema kuanzia Januari hadi Novemba mwaka 2016 yaliripotiwa makosa 11,513 kulinganisha na 11,620 katika kipindi kama hicho mwaka huu ambayo ni ongezeko la makosa 107 sawa na asilimia 0.9.
Amesema kati ya Januari na Novemba 2016 makosa makubwa ya jinai yalikuwa 68,204 ikilinganishwa na makosa 61,794 yaliyoripotiwa katika kipindi hicho mwaka 2017 ikiwa ni pungufu ya makosa 6,410 ambayo ni sawa na asilimia 9.4.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Desemba 20,2017 kuhusu hali ya usalama na amani nchini amesema ambayo yanaonekana kuongezeka ni makosa ya kubaka na kunajisi ambayo.
“Mwaka jana wakati kama huu makosa ya kubaka yaliyoripotiwa yalikuwa 6,985 lakini mwaka huu yameongezeka na kufikia 7,460 sawa na ongezeko la asilimia 6.8 huku mkosa ya kunajisi yakiongezeka kutoka 16 hadi 25 sawa na asilimia 56.3,” amesema Boaz.
Kuhusu makosa ya usalama barabarani amesema kwa mwaka 2016 yaliripotiwa makosa 1861 tofauti na mwaka 2017 yameripotiwa makosa 1526 hivyo yamepungua kwa asilimia 18.0.
Amewataka wananchi wote kuchukua tahadhari kipindi hiki cha sikukuu na kujiepusha na matukio ya uvunjifu wa amani huku akisema jeshi hilo limejipanga kukabilina na matukio hayo.
“Jeshi la polisi tumepanga mikakati madhubuti kukabiliana na matishio ya amani na utulivu pamoja na kudhibiti vyanzo vyote vya ajali nchini ...Tumejipanga kudhibiti vitendo vyote vya uhalifu vitakavyojitokeza katika kipindi hiki,” amesema Boaz.Mwananchi
0 comments:
Post a Comment