BREAKING NEWS !! WASHTAKIWA 44 KATI YA 57 KESI YA KUCHOMA MOTO MALINYI WAACHIWA HURU MOROGORO
Morogoro. Washtakiwa 44 kati ya 57 wa kesi ya kuchoma moto ofisi ya Serikali ya kijiji cha Sofi wilayani Malinyi mkoani Morogoro wamefutiwa mashtaka na kuwa huru, huku wabunge wa Chadema Suzan Kiwanga (Mlimba) na Peter Lijualikali wa Kilombero na wenzao 11, ikielezwa watasomewa maelezo ya awali Aprili 24, 2018.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa Serikali, Sunday Hyera uliwasilisha ombi la kuwafutia mashtaka washtakiwa hao 44 kwa kile walichodai kuwa hawana ushahidi wa nguvu utakaowatia hatiani washtakiwa hao.
Hakimu aliyesikiliza kesi hiyo, Ivan Msack ameridhia ombi la kuwafutia mashtaka washtakiwa hao na hivyo kuhairisha kesi hadi Aprili 24 ambako washtakiwa 13, wakiwemo wabunge hao kesi yao itaanza kusikilizwa kwa maelezo ya awali.
Nje ya mahakama mmoja wa mawakili wanaowatetea washtakiwa hao, Fredy Kalonga amedai kuwa kwa sasa wanajiandaa kukabiliana na ushahidi utakaotolewa na upande wa mashtaka dhidi ya wabunge hao na wengine 11.
Miongoni mwa waliofutiwa mashtaka ni pamoja na diwani wa Mkula, Clement Mjami aliyedai Jamhuri imeonyesha udhaifu mkubwa kwa kukosa ushahidi dhidi yake.Mwananchi
0 comments:
Post a Comment