Na Luqman Maloto
Watu wa soka wana misemo yenye kufurahisha. Manchester United iliwafunga mahasimu wao wa Jiji la Manchester, klabu ya Manchester City magoli 3-2 katika mchezo wa mzunguko wa pili, Ligi Kuu ya England. Ni mchezo uliofanyika siku tatu kabla ya City kuivaa Liverpool, mechi ya pili ya robo fainali, Klabu Bingwa Ulaya.
Manchester City imekuwa na msimu mzuri sana 2017-2018. Timu yake ni bora mno kiasi cha kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu ya England ikiwa imesaliwa na michezo mitano. Hivyo, mashabiki wa United baada ya kuifunga City, walianzisha ucheshi wa kuitania Liverpool kuwa wao walichokifanya kilikuwa kutibua mzinga wa nyuki, hivyo cha moto wangekipata.
Walimaanisha kwamba kitendo cha wao kuifunga City, hasira zote zingeishia kwa Liverpool. Hata hivyo, ulikuwa utani wa soka. Liverpool ilishinda mchezo wa marudiano kwa mabao 2-1, ikiwa ni nyongeza baada ya mechi ya awali kushinda 3-0, hivyo Liverpool wametinga nusu fainali Klabu Bingwa Ulaya kwa jumla ya magoli 5-1 dhidi ya City.
Nilivutiwa na utani huo wa kuchokoza mzinga wa nyuki. Nauleta katika kumtafsiri mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye.
Tangu Machi 2017 alipovuliwa uwaziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ni kama Serikali ilichokoza mzinga wa nyuki, maana Nape amekuwa moto hasa. Amekuwa na hoja nzito dhidi ya Serikali kuliko wabunge wengi wa upinzani.
Hadi sasa, imethibitika kuwa Nape ni mbunge mwenye kusoma nyaraka nyingi za Serikali zenye kuwasilishwa bungeni. Na taarifa anazopata katika kusoma kwake, amekuwa akizitumia kujenga hoja zenye uzani mkubwa dhidi ya Serikali, hivyo kutimiza mantiki halisi ya kuwa mjumbe wa chombo cha uwakilishi wa wananchi.
Namna anavyojenga hoja kipindi hiki akiwa mbunge wa kawaida baada ya kuvuliwa uwaziri, inamfanya Nape athibitishe sura nne za kisiasa na kiuongozi. Anzia alipokuwa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) na uhusika wake, baadaye katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, akawa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, halafu sasa hivi mbunge tu.
Nape wa UVCCM
Nape alijipambanua mno mwaka 2008 wakati wa mchakato wa uchaguzi wa mwenyekiti wa Umoja wa Vijana CCM (UVCCM).
Kipindi hicho mwenyekiti aliyekuwa Dk Emmanuel Nchimbi aliyekuwa akimaliza muda wake, hivyo kuacha vijana wapya kuwania nafasi hiyo.
Mwenyekiti wa UVCCM pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, kwa hiyo anaingia kwenye vikao vyote muhimu vya uamuzi vya chama. Pamoja na Nape, vijana wengine wa CCM wakati huo waliojitosa kuwania uenyekiti wa UVCCM walikuwa Jerry Silaa, Hamad Masauni, Issa Haji Ussi, Anthony Mtaka, Said Mtanda, Haule Pangisa na Samuel Marero.
Wengine walikuwa Stephen Deya, Geofrey Mwankenja, David Manoti, Mussa Mnyeti, Edson Lubua, Mwamini Lusingu, Asmah Kalokola, Marco Zablon Allute, Harold Adamson, Adila Hilal Vuai, Ashura Ismail, Rashid Masalaka na Raha Ahamada.
Baadaye katika kupitisha majina ya wagombea, ilibainishwa kuwa ilikuwa zamu ya Zanzibar kuongoza UVCCM. Hiyo ilitokana na ukweli kwamba wenyeviti wa UVCCM waliopishana walikuwa wanatoka Tanzania Bara. Maana Nchimbi alipokea uongozi kutoka kwa Dk Didas Masaburi. Uchaguzi ulifanyika na Masauni alichaguliwa kuwa mwenyekiti, huku makamu wake akiwa Benno Malisa.
Baadaye Masauni alilazimishwa kujiuzulu uenyekiti baada ya kubainika kuwa alighushi umri. Hata hivyo, mapema kabisa liliibuka sekeseke la kumkata Nape ambaye alijitokeza na kusema:
“Kati ya wagombea wote zaidi ya 29, nimekuwa mjumbe wa Nec kwa miaka sita, mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM miaka sita na katibu msaidizi wa Idara ya Siasa, Makao Makuu ya chama. Najua kanuni, sheria na katiba ya Umoja wa Vijana CCM (UVCCM).”
Baadaye Nape akatuhumiwa kuwachafua vigogo, hasa aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa. Nape alisema Lowassa ambaye alikuwa mwenyekiti wa bodi ya UVCCM, aliiongoza jumuiya hiyo kuingia mkataba wa kifisadi katika ubia wa kujenga jengo la makao makuu ya CCM, lililopo Upanga jijini Dar es Salaam.
Kashfa hiyo pia ilimtikisa Nchimbi ambaye ndiye alikuwa mwenyekiti kipindi mkataba huo unasainiwa.
Kutokana na tuhuma hizo alizozitoa, Baraza Kuu la UVCCM, lilimfuta uanachama Nape.
Kama si aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Jakaya Kikwete kumkingia kifua, Nape angepoteza uanachama CCM tangu mwaka 2008. Mwaka 2010, Nape aliomba ridhaa ya CCM kuwa mgombea ubunge jimbo la Ubungo, lakini alishindwa. Kisha Kikwete alimteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Masasi.
Nape Katibu wa Itikadi
Nape kama mkuu wa wilaya hakujipambanua sana ukizingatia ni nafasi ambayo aliihudumia kwa muda mfupi. Aprili 2011 aliteuliwa kuwa katibu wa Itikadi na Uenezi CCM. Ni kipindi ambacho Nape alijiweka wazi kama mtetezi kindakindaki wa chama. Alifanya kazi kubwa kuijenga na kuitetea CCM.
Kwa vile Nape hakuwa na majukumu mengine, aliweza kuambatana na aliyekuwa katibu mkuu, Wilson Mukama kufanya kazi kubwa ya uenezi wa chama.
Mukama alimpompisha Abdulrahman Kinana, kazi kubwa mno ilifanyika. Nape alizunguka na Kinana nchi nzima kuhakikisha CCM inakuwa hai na yenye nguvu kushinda Uchaguzi Mkuu 2015.
Ni kipindi ambacho Nape aliweza kusimama na Kinana, kisha kuwashambulia mawaziri wa Serikali ya CCM kwa kuwaita mizigo. Shabaha ilikuwa kujenga hali ya kuaminika kwa chama, ili baadhi ya makosa ya viongozi serikalini yasichukuliwe kuwa kasoro zitokanazo na CCM.
Kimsingi Nape aliibeba CCM mabegani kwake na hakutaka kuambiwa kitu. Wabunge wa upinzani na hata wa CCM walipotaka kugusa masilahi ya chama, hakusubiri pakuche; aliwajibu.
Kipindi Lowassa alipokuwa mbunge wa Monduli, aliwahi kusema bungeni kuwa “Serikali haichukui maamuzi magumu”, Nape akamjibu: “Maamuzi magumu yanachukuliwa. Hata Lowassa kufukuzwa uwaziri mkuu yalikuwa maamuzi magumu.”
Nape alipokuwa waziri
Machi 23, mwaka jana, saa chache tangu alipovuliwa uwaziri, Nape alitaka kufanya mkutano na waandishi wa habari, lakini alizuiwa.
Kuna mtu ambaye inaamika ni ofisa wa polisi, alimtishia bostola akimlazimisha aingie kwenye gari aondoke eneo la Hoteli ya Protea, Oysterbay, Dar es Salaam, alipopanga kuzungumza na waandishi wa habari.
Tukio hilo la kutishiwa bastola lilisababisha Nape awe mbogo. Alihoji: “Unajua nimepambana kiasi gani kuipigania nchi hii? Ona mkono wangu ulivyoharibika. Nimelala porini miezi 28 kupigana kuirudisha CCM madarakarani.
Halafu anakuja mtu ananionyesha bastola.” Maneno hayo ya Nape yaliakisi kazi kubwa aliyoifanya na Kinana kuipa uhai CCM mpaka kushinda Uchaguzi Mkuu 2015.
Nape aliondolewa uwaziri siku moja baada ya kupokea ripoti ya kamati aliyoiunda kuchunguza sakata la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kudaiwa kuvamia kituo cha Clouds TV na kulazimisha kurushwa hewani kwa kipindi ambacho maudhui yake yalikataliwa na watayarishaji wa kipindi pamoja na uongozi runinga hiyo.
Kabla ya Nape kupokea ripoti hiyo, Tayari Rais John Magufuli alikuwa ameshatoa kauli ya kumtetea Makonda, kwamba asingefanya chochote. Zaidi, alimtaka afanye kazi.
Na wakati Rais Magufuli anatoa kauli hiyo, tayari Nape alikuwa ameshaunda kamati. Vilevile Nape aliporuhusu ripoti ya kamati isomwe mbele ya vyombo vya habari na kumtia hatiani Makonda kwa uvamizi, Rais Magufuli alikuwa aneshasema Makonda aachwe.
Pamoja na Nape kuondolewa uwaziri, amebaki na heshima kuwa alijaribu kufanya jambo la kutetea uhuru wa vyombo vya habari. Na siku alipotolewa bastola baada ya kuondolewa uwaziri, Nape alisema: “Mimi ni mwanahabari. Nisipopigania uhuru wa hawa wanahabari nipiganie uhuru wa akina nani wengine?”
Hata hivyo, Nape alipokuwa waziri alishutumiwa kwa kitendo chake cha kulazimisha kupeleka bungeni muswada wa Huduma za Habari 2016 na baadaye kupitishwa kuwa Sheria ya Huduma za Habari 2016.
Wadau wa habari waliomba sana ufanyiwe marekebisho, maana unakandamiza mno tasnia ya habari. Tuhuma nyingine ya Nape ni kufuta matangazo ya moja kwa moja ya televisheni katika vipindi vya Bunge.
Kimsingi Nape akiwa waziri, kabla ya kuibuka kwa sakata la Makonda na Clouds TV, alijipambanua kuwa mwenye kuilinda Serikali kama ambavyo aliipigania CCM. Na baada ya kuondoka kwenye uwaziri, Nape amekuwa shubiri kwa mawaziri na Serikali kwa jumla kutokana na hoja zake.
Hata hivyo, haiwezi kusahaulika kuwa Januari na Februari mwaka jana, Makonda alipoanzisha mpango wa kuwaita watu mbalimbali Kituo Kikuu cha Polisi (Central), Dar es Salaam, kwa tuhuma za kuhusika na dawa za kulevya, alipowaita wasanii kwa mara ya kwanza, Nape kama waziri mwenye dhamana ya sanaa, aliupinga utaratibu uliotumika, kwamba uliwaharibia biashara wasanii.
Nape mpya bungeni
Hivi karibuni Nape alipokuwa akichangia hotuba ya Waziri Mkuu, alikosoa mwenendo wa Serikali kuwa inakwenda kinyume na ilani ya CCM.
Alisema watu wa Lindi na Mtwara waliingia gharama kubwa, ikiwemo kuvunjiwa nyumba zao ili kuruhusu mradi wa uvunaji wa gesi asilia, lakini anashangaa kuona suala la gesi linatelekezwa.
Alikosoa mradi wa umeme wa maji kwenye Mto wa Rufiji wa Stiegler’s Gorge kuwa haupo kwenye ilani ya CCM. Akasema, mambo ambayo yamo kwenye ilani, yaliyoombewa kura na wananchi wakakubali kuichagua CCM yanaachwa, yanaingizwa ambayo hayamo.
Alikumbusha kwamba wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu 2015, CCM ilinadi uchumi wa gesi, lakini sasa nchi inarejea katika umeme wa maji.
Hiyo si mara ya kwanza kwa Nape kuikosoa Stiegler’s Gorge. Novemba mwaka jana, Nape alizungumza bungeni kuhusu kasoro ya Serikali kutoishirikisha sekta binafsi katika miradi inayoweza kujiendesha kibiashara, badala ya kuendelea kukopa, kitu ambacho alionya kwamba kitakuja kusababisha athari kubwa kwa nchi.
Jambo la kwanza Nape alisema Serikali inakopa fedha nyingi kwa ajili ya miradi mikubwa ambayo ukamilikaji wake unachukua muda mrefu, wakati mikopo husika marejesho yake yanafanyika ndani ya muda mfupi. Kutokana na hali hiyo, alitahadharisha kwamba marejesho yataathiri miradi mingine.
Nape alisema kwa vile miradi itachelewa kukamilika, wakati wa marejesho ya mikopo, itabidi kuchukua fedha kwenye miradi ya huduma kama elimu, afya na kadhalika ili kuwalipa wadeni wa nchi. Katika hili Nape alisema anatilia shaka uzalendo wa wachumi ambao wanamshauri Rais Magufuli.
Upande wa pili, Nape alionya kuwa nchi inapiga hatua kwenda kuwa isiyokopesheka ikiwa itakopa kwa ajili ya miradi miwili tu; wa kwanza ni ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge) dola 15 bilioni (Sh33.8 trilioni) na wa ufuaji umeme wa Stiegler’s Gorge megawati 2,100 dola 5 bilioni (Sh11.27).
Jumla dola 20 bilioni (Sh45 trilioni). Nape alisema taarifa mya zinaeleza Deni la Taifa limefikia dola 26 bilioni (Sh58.6 bilioni) sawa na asilimia 32 ya uhimilivu wa deni. Kwamba ili Tanzania ifikie kikomo cha kukopeshwa, deni lake linapaswa kufikia dola 45 bilioni (Sh101.4 trilioni).
Kutokana na hoja hiyo ya Nape, endapo Serikali itaongeza mkopo kwa miradi miwili tu ya standard gauge na Stiegler’s Gorge, deni litafikia dola 46 bilioni (Sh103.7 trilioni), yaani ongezeko la Sh2.3 trilioni kutoka kwenye kiwango chake cha mwisho cha kukopa. Mpaka hapo unaweza kumuona Nape mpya.
Sawa na ule utani kwamba mzinga wa nyuki umechokozwa, sasa mawaziri wanamkoma bungeni. Hata hivyo, huyo ndiye Nape anayebadilika kutoka UVCCM, Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kisha sasa mbunge.
0 comments:
Post a Comment