BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

SAKATA LA Sh1.5 TRILION ZAWAHENYESHA VIONGOZI WA SERIKALI RAIS DK MAGUFULI NA SIASA

Dar/Dodoma. Wakati Rais John Magufuli akimuuliza CAG na katibu mkuu wa Wizara ya Fedha swali kuhusu madai ya kuwapo kwa fedha ambazo hazikukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na hivyo kuibua mjadala, Serikali imelazimika kutoa tamko bungeni mjini Dodoma kuhusu sakata hilo.

Matukio hayo mawili yalitokea jana Ikulu jijini Dar es Salaam ambako Rais alikuwa akiwaapisha majaji wapya na Dodoma ambako Bunge lilipangua ratiba yake kumuwezesha Naibu Waziri wa Fedha, Dk Ashatu Kijaji kutoa ufafanuzi wa Sh1.51 trilioni ambazo ni tofauti kati ya fedha zilizokusanywa na zilizotumika mwaka wa fedha wa 2016/17 na baadaye kukaguliwa na CAG.

Matukio hayo yamekuja baada ya wiki nzima ya kujadili ripoti ya ukaguzi ya CAG iliyowasilishwa bungeni Aprili 11 huku suala hilo likitawala mjadala huo uliodumu kwa takriban siku tisa kutokana na wabunge kuhoji matumizi yake na sababu za kutokaguliwa.

Suala hilo liliibuliwa na mbunge wa Kigoma Mjini na kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ambaye chama chake pia kimemuandikia Spika kikitaka aunde kamati kuhoji, lakini katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alimjibu kuwa hakuna fedha iliyoibwa wala kiasi hicho kutajwa kwenye ripoti.

Zitto aliibua hoja yake kutoka ukurasa wa 34 wa ripoti ya CAG ya ukaguzi wa fedha za Serikali Kuu kwa mwaka unaoishia Juni 30, 2017 ambayo inaonyesha kuwa kati ya Sh25,307.48 bilioni zilizokusanywa, Sh23,792.30 bilioni zilitolewa kwa ajili ya mishahara ya watumishi, matumizi mengine, matumizi ya maendeleo na fedha kwa ajili ya kulipa madeni yatokanayo na amana za Serikali pamoja na riba.

Jana, baada ya hafla ya kuwaapisha majaji kuisha kwa hotuba za viongozi, Rais Magufuli alionekana kama hakutaka kuzungumza, lakini wakati waalikwa wakiwa wanasubiri asimame, alielekea sehemu ya kutolea hotuba na kueleza kuwa alipanga kutozungumza, lakini alikuwa na machache ya kusema.

Baada ya kuzungumzia masuala ya Mahakama na umuhimu wa kutenda haki, Rais aligeukia suala la uvumi wa mitandaoni na ndipo alipogusia sakata hilo.

“Kuna ugonjwa tumeupata Tanzania wa kufikiri kila kinachoandikwa kwenye mitandao ni cha ukweli. Sifahamu ugonjwa umetoka wapi, lakini ni kwa sababu hii mitandao hatui-control sisi,” alisema Rais.

“Wako huko wenye mitandao yao, interest yao ni kutengeneza business. They don’t care consequence (lengo lao ni kufanya biashara, hawajali athari) mtakazopata. Ndiyo maana ukienda nchi kama China, sina uhakika kama wana Google na WhatsApp za aina hii kama tulizonazo sisi.

“Ndiyo maana kila mmoja anapojifikiria ana-post chochote. Nilikuwa nasomasoma baadhi ya mambo mengine wanasema Serikali imeiba Sh1.5 trilioni. Siku moja nikampigia CAG kwamba mbona kwenye ripoti yako uliyonisomea CAG hukunieleza huu wizi wa Sh1.5 trilioni?

“Kwa sababu ungenisomea hapa, siku hiyohiyo ningefukuza watu. Kama nimefukuza wakurugenzi watatu siku hiyohiyo kwa sababu ya hati chafu, hawa wa Sh1.5 trilioni uliwaficha wapi?”

Alisema amejaribu kusoma kwenye ripoti ya CAG, lakini hakuona mahali palipoandikwa fedha hizo zimeibiwa na akampigia Profesa Assad kumuulizia na baadaye katibu wa Wizara ya Fedha, Dotto James ambao pia walimwambia hakuna kitu hicho.

“Hakuna Sh1.5 trilioni iliyoibwa na Serikali lakini kwa sababu ya uhuru wa mtu kuandika chochote. Nami nika-check tu nikasema aah! Hata ndege tuliambiwa ni mbovu, ni kawaida ya uhuru huu,” alisema.

JPM amuuliza CAG, katibu
Baadaye aliwauliza Profesa Assad na Dotto waliokuwapo katika hafla hiyo.

“Na bahati nzuri CAG yupo hapa. Kwenye ripoti yako kuna hela tumeibiwa Sh1.5 trilioni, sema kabisa bwana, tumeibiwa Sh1.5 trilioni?” alihoji.

“Hakuna mambo ya namna hiyo Mheshimiwa Rais,” alijibu Profesa Assad.

Rais Magufuli akamshukuru na kumuuliza Dotto. “Basi bwana asante, kaa au katibu mkuu kuna fedha Sh1.5 trilioni zimeibwa?” alimuuliza.

Dotto: “Hapana Mheshimiwa Rais.”
Dk Magufuli: “Unasema?”
Dotto: “Hapana, Hazina tupo salama.”

Rais Magufuli alisema watu wamekuwa wakiandika na kuzungumza bila aibu na kwamba hata hawamuogopi Mungu, na kwa sababu ya mitandao wanapost chochote.

“Kwenye ripoti hakuna. Yaani mimi ningepata wa aina hiyo hata angekuwa waziri siku hiyohiyo angeondoka. Natafuta hela halafu ziwe zinaibiwa!” alisema.

Alisema anafahamu ripoti ya CAG huwa inajadiliwa kwenye PAC (Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali), hivyo wabunge watajadili.

“Kwa sababu hapa nazungumza na wanasheria ifike mahali sasa tuwe tunazitumia sheria zetu. Ukishapotosha umma wa Watanzania 55 milioni madhara yake ni makubwa mno. We may take it simple (tunaweza kuchukulia kirahisi), lakini madhara yake ni makubwa,” alisema.

“Ni matumaini yangu katika sheria hizi, DPP yupo, naibu yupo, solicitor general yupo, Dk tena umesomea hayahaya, naibu wake yupo tena mpiganaji mzuri wa haki za binadamu. Nafikiri atasimamia hata haki za Watanzania wengine, zikiwamo za Serikali.

“Majaji nanyi mpo nina uhakika kesi kama hizi zikija mtazishughulikia harakaharaka. Ni lazima tutangulize kwanza masilahi ya nchi yetu, inawezekana wapo watu wanakuchukia wewe jaji mkuu au wanamchukia waziri au labda wananichukia mimi, lakini chuki tusiielekeze kwa Watanzania. Nchi hii ikiharibika hakuna atakayebaki salama. Tunaweza kufikiri tupo pembeni lakini madhara yake ni makubwa.”

Kauli ya Serikali
Mjini Dodoma ambako wabunge, hasa wa upinzani wamekuwa wakihoji matumizi ya fedha hizo, Dk Kijaji alitoa tamko la Serikali kuhusu sakata hilo, akisema katika kipindi cha mwaka 2012/13 hadi 2016/17, wizara hiyo ilikuwa kwenye kipindi cha mpito cha miaka mitano ya utekelezaji wa mpango mkakati wa kuandaa hesabu za Serikali kwa kutumia mfumo wa viwango vya kimataifa vya uhasibu katika sekta ya umma (IPSAS Accrual).

Alisema katika kipindi hicho, Serikali iliendelea kukusanya taarifa kwa kutumia mfumo huo ili kuwezesha kutambua kikamilifu hesabu za mali, madeni na mapato yanayotokana na kodi.

Alisema IPSAS Accrual ni mfumo wa kiuhasibu ambao hutambua mapato baada ya muamala husika kukamilika na si wakati fedha taslimu inapopokewa; na matumizi yanatambuliwa wakati muamala wa matumizi umekamilika na si wakati fedha inalipwa.

“Mfumo huu ni mzuri na una faida nyingi,” alisema.

Dk Kijaji alisema matokeo ya utekelezaji wa mpango mkakati wa uandaaji wa hesabu kwa mfumo wa IPSAS Accrual umeiwezesha Serikali na taasisi zake kutoa taarifa za kina na zinazoonyesha uwazi na uwajibikaji wa taasisi husika, hususan katika usimamizi wa mali na madeni ya taasisi.

“Kuongezeka kwa uwazi, kumewawezesha watumiaji wa hesabu kupata taarifa zinazowasaidia kufanya uamuzi sahihi na kwa wakati,” alisema.

Dk Kijaji alisema kutokana na matumizi ya mfumo huo wa viwango vya kimataifa vya uhasibu katika sekta ya umma, hakuna fedha taslimu Sh1.51 trilioni iliyopotea au kutumika kwenye matumizi ambayo hayakuidhinishwa na Bunge.

“Hivyo basi, madai ya baadhi ya watu wasiolitakia mema Taifa letu na Serikali yetu ya Awamu ya Tano hayana msingi wowote wenye mantiki,” alisema.

Naibu waziri alisema taarifa ya CAG imeeleza jumla ya mapato yote ya Serikali kwa mwaka 2016/17 yalikuwa Sh25.3 trilioni ambazo zinajumuisha mapato ya kodi; mapato yasiyo ya kodi; mikopo ya ndani na nje; na misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo.

Alisema kuanzia mwaka 2016/17, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilianza rasmi kuyatambua mapato kwa mfumo wa IPSAS Accrual.

“Hivyo basi, kati ya mapato haya ya Sh25.3 trilioni, yalikuwamo pia mapato tarajiwa (receivables) kama mapato ya kodi yenye jumla ya Sh687.3 bilioni na mapato ya kodi yaliyokusanywa kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya jumla ya Sh203.92 bilioni (transfer to Zanzibar)” alisema.

Dk Kijaji alisema katika uandishi wa taarifa ya ukaguzi, CAG alitumia taarifa za hesabu na nyaraka mbalimbali zikiwamo taarifa za utekelezaji wa bajeti na hadi kufikia Juni 30, 2017; mapato yalikuwa jumla ya Sh25.3 trilioni na matumizi yalikuwa Sh23.79 trilioni.

“Matumizi haya hayakujumuisha Sh697.85 bilioni zilizotumika kulipa dhamana na hati fungani za Serikali zilizoiva,” alisema.

Dk Kijaji alisema matumizi hayo yalikuwa hayajafanyiwa uhamisho (re-allocation) wakati ukaguzi unakamilika.

“Hivyo basi, baada ya kufanya uhamisho, jumla ya matumizi yote kwa kutumia ridhaa za matumizi (exchequer issues) yalikuwa Sh24.4 trilioni,” alisema Dk Kijaji.

Alisema baada ya kupunguza mapato ya Zanzibar ya Sh203.92 bilioni na mapato tarajiwa ya Sh687.3 bilioni; mapato halisi kwa mwaka 2016/17 yalikuwa Sh24.41 trilioni.

Dk Kijaji alisema baada ya kujumlisha matumizi ya dhamana na hati fungani zilizoiva za kiasi cha Sh697.85 bilioni kwenye matumizi ya Sh23.79 trilioni yaliyoonyeshwa katika taarifa ya CAG, ridhaa za matumizi zilizotolewa zilikuwa Sh24.49 trilioni na kuleta ziada ya matumizi ya Sh79.07 bilioni ikilinganishwa na mapato.

Alisema kwa mchanganuo huo, ni dhahiri kuwa kwa mwaka 2016/17 matumizi ya Serikali yalikuwa makubwa kuliko mapato kwa Sh79.09 bilioni ambazo ni overdraft kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

“Utaratibu wa kutoa fedha zaidi ya mapato (overdraft facility) uko kwa mujibu wa kifungu cha 34 cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006,” alisema.

Dk Kijaji alisema Serikali ipo makini na haiwezi kuruhusu upotevu wa aina yoyote wa fedha za umma.

“Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuona kwamba, kila mapato yanayokusanywa yanatumika ipasavyo na kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania,” alisema.

Dk Kijaji alitoa kauli ya Serikali bungeni baada ya Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kukatiza kipindi cha maswali na majibu.

Maswali sita yalikuwa yameshajibiwa na kusalia mawili ndipo alipotoa muda Serikali kutoa kauli hiyo.

Uamuzi huo ulitokana na mwongozo ulioombwa na mbunge wa viti maalumu (Chadema), Susan Lyimo aliyesema kipindi cha maswali na majibu kwa mujibu wa kanuni za Bunge wakati wa mkutano wa bajeti kinatakiwa kuwa dakika 60, hivyo kuhoji ni kanuni gani imetumika kukatisha maswali mawili yaliyosalia.

Akijibu huo mwongozo, Dk Tulia alisema hakuna kanuni iliyovunjwa na kwamba, maswali yaliyosalia yatapangiwa siku nyingine.

ACT, CUF, Chadema walonga
Lakini kauli hiyo haikukubaliwa na ACT Wazalendo ambayo jana jioni ilitoa taarifa ikisema maelezo hayo ni kama yaliyotolewa na Polepole ambayo tayari jana yamejibiwa na katibu mwenezi Taifa wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Zitto inasema chama chake kinaendelea kumsihi Spika wa Bunge aruhusu ukaguzi maalumu wa matumizi ya Sh1.5 trilioni kupitia Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).

Mapema wiki hii, Polepole aliitisha mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia hoja ya Zitto kuhusu fedha hizo na kushauri akamatwe na mamlaka husika kwa kile alichodai ni upotoshaji.

Kama alivyoeleza Dk Kijaji, katibu huyo wa uenezi wa CCM alisema kuna fedha tarajiwa ambazo ndizo ripoti ya CAG inaonyesha hazikukaguliwa.

Naye mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema hakuna namna Serikali itakwepa kulitolea ufafanuzi suala la fedha hizo. 


Pia mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro alisema chama hicho kinamtaka Spika aunde kamati ya kuchunguza suala hilo au aziachie kamati husika za chombo hicho kulishughulikia./Mwananchi
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: