Dar/Iringa. Chanzo cha vifo vya pacha walioungana Maria na Consolata Mwakikuti ni kusinyaa kwa mapafu hivyo kusababisha kufeli kwa upumuaji wao.
Hayo yalielezwa jana na Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Ndani wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Pauline Chale ambaye alibainisha kwamba madaktari walifahamu kuwa ugonjwa huo ungekuwa na madhara kwao.
“Kiutaalamu tulijua kwamba ipo siku presha ya mapafu itapanda na kusababisha shinikizo la moyo na mapafu ambapo hiyo ndiyo iliyosababisha kifo chao,” alisema Dk Chale ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na mapafu.
Alisema walipowapokea Februari 3 katika kitengo cha wagonjwa mahututi (ICU), Mwaisela walikofikishwa kutokana na tatizo la kupumua lililoambatana na maambukizi ya bakteria katika mfumo wa upumuaji, jopo la madaktari lilifanya kazi mbili kubwa; kuchunguza nini kilichokuwa kinasababisha homa ya mapafu na kwa nini inashindwa kupona.
“Tulianza kuchukua sampuli ya makohozi kutambua aina gani ya bakteria wanaoleta tatizo la maambukizi na kubaini ni ‘Klebsiella Pneumoniae’. Ilitusaidia kujua na kuchagua aina sahihi ya dawa, walitibiwa kwa dawa stahiki na maambukizi ya mapafu tulijiridhisha yamekwisha.”
Sababu ya upumuaji hafifu
Dk Chale alisema ili kubaini kwa nini pacha hao walikuwa na upumuaji hafifu, waliamua kufanya vipimo vya mapafu kupitia kipimo cha CT Scan ya kifua iliyoonyesha umbo la nje la kifua chao na mfumo wa njia za hewa na mapafu yenyewe ambacho kilionyesha wote wawili walizaliwa pia na ulemavu wa kifua na uti wao wa mgongo.
“Hiyo shepu ya kifua ilichangia na ushindwaji wa kupumua ambao kwao lilikuwa ni tatizo endelevu na kadri walivyokuwa wanazidi kukua, upumuaji wao ulikuwa unazidi kuwa hafifu,” alisema.
Alisema katika uchunguzi huo walibaini hata ukubwa wa mapafu ulikuwa mdogo uliobana hasa kwa Maria ambaye alikuwa chini ya mwenzake.
“Maria alikuwa na mapafu madogo sana na hata kiwango cha oksijeni kilichoingia kwenye kifua chake kilikuwa kidogo, hivyo vyote vilichangia kuendelea kusinyaa kwa mapafu yao,” alisema Dk Chale.
Alisema kutokana na hali hiyo, Muhimbili ilizungumza na familia ambayo ilitaja matatizo ambayo walizaliwa nayo tangu wakiwa wadogo. “Kwa sababu maambukizi ya mapafu yalikwishapona, tukajiridhisha wanaweza kuwachukua na kuendelea kuwatunza nyumbani, lakini inabidi wawe na vifaa maalumu vya kuweza kupumua.”
Alisema Aprili 30 waliwaruhusu lakini kutokana na maandalizi ya jinsi ya kuwafikisha Hospitali ya Mkoa wa Iringa waliondoka Mei 17 wakiongozana na muuguzi aliyebobea kuhudumia wagonjwa mahututi na daktari aliyebobea katika magonjwa ya dharura.
Dk Chale alisema kwa kipindi chote walichokuwa Iringa walikuwa wakiwasiliana na daktari bingwa, Dk Faith Kundy ambaye aliwapatia maendeleo yao.
“Daktari bingwa Dk Faith alishanipigia simu nikamwelekeza jinsi ya kufanya na aliweza kutatua kila tatizo lililotokea, lakini saa 72 kabla ya kifo chao hakukuwa na mawasiliano yoyote na kifo cha namna hiyo kinakuwa ni ghafla huwezi kujua kitakuwaje, tulijua ikifika hatua hiyo ingekuwa ni ghafla,” alisema.
Walikuwa wadadisi katika tiba
Moja ya vitu ambavyo viliwafanya madaktari wawe makini ni jinsi Maria na Consolata walivyokuwa wakifuatilia na kutaka kujua kila kitu ikiwamo kwa nini walimeza dawa ya aina fulani na kwa sababu gani.
Dk Chale alisema haikuwa kazi kubwa kuwaelewesha katika matibabu yao kwani wao pia walikuwa na juhudi kujua kuhusu afya zao. “Kwa kipindi chote walihitaji kujua matibabu yao yanakwendaje, kabla ya kufanyiwa tiba fulani kutokana na upeo waliokuwa nao walihoji na hata wakati mwingine kuomba ushauri pia nini wafanye kuepuka madhara zaidi ya kifua,” alisema.
Walichagua pa kuzikwa
Pacha hao ambao walifariki dunia Jumapili usiku mjini Iringa, watazikwa kesho kwenye makaburi ya Tosamaganga.
Akizungumzia mazishi hayo, Mkuu wa Shirika la Maria Consolata, Jane Nugi alisema uamuzi huo umefikiwa kutokana na matakwa ya pacha hao ambao katika uhai wao walichagua kuzikwa kwenye eneo wanalozikwa viongozi wa madhehebu ya Katoliki na kwamba msiba wao upo kwenye nyumba ya shirika hilo Kihesa, Iringa kwa kuwa ndio nyumbani kwao. “Wakati wakiumwa walisema wangetamani kuhifadhiwa tunakohifadhiwa sisi hivyo watazikwa kwenye makaburi ya Tosamaganga,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alisema jana kuwa pacha hao wanaandaliwa jeneza moja lenye mfumo wa watu wawili, misalaba miwili na kwamba watazikwa katika kaburi moja.
Kuhusu ratiba, Kasesela alisema wataagwa kesho katika viwanja vya Rucu ambako pia kutakuwa na ibada maalumu itakayoanza saa nne ikisimamiwa na maaskofu, Tarcisius Ngalalekumtwa wa Jimbo la Iringa na Alfred Maluma wa Jimbo Katoliki Njombe.
Makamu Mkuu wa Rucu, Pius Mgeni alisema, “Tumeshaanza maandalizi ya ujenzi wa jukwaa kwa ajili ya kuwaaga.”
Mlezi wa wanafunzi wa Ruco, Martha Magembe alisema walilazimika kuunda zamu za kulala na kushinda hospitali na pacha hao baada ya walezi waliokuwa nao Muhimbili kutakiwa kupumzika.
Walivyokabidhiwa kwa masista
Alisema walikabidhiwa watoto hao na wazazi wao mara tu walipozaliwa katika hali hiyo. Kuhusu hilo, familia ya watoto hao jana ilizungumzia ilivyoshiriki kuwalea licha ya kuwa walikuwa chini ya uangalizi wa masista.
Mama mkubwa wa pacha hao, Anna Mushumbusi alisema tangu walipozaliwa walikuwa karibu nao wakifuatilia maendeleo yao lakini hawakuweza kuwachukua kulingana na hali waliyokuwa nayo.
Kaka yao wa kwanza, David Mwakikuti alisema baada ya wazazi wao kufariki walichukuliwa na ndugu upande wa mama na kwenda kulelewa Bukoba. “Tulilelewa vizuri na kwa upendo ndio maana leo hii wote tumesomeshwa, wajomba na shangazi zetu hawakutuacha kabisa,” alisema.
Maria na Consolata ni wazaliwa watatu wakiongozwa na kaka yao David, dada yao Editha na mdogo wao wa mwisho Jackline.
David alisema wakati Maria na Consolata wakisoma Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Ruaha (Rucu), Editha anasoma Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut) na Jackline anajiandaa kuanza masomo ya sekondari.
David ambaye alisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kozi ya takwimu, anafanya kazi katika shirika linalojishughulisha na masuala ya kijamii la OM lilipo Dar es Salaam.
“Hatukuwa na uwezo wa mawasiliano zaidi lakini tulikuwa tukiwaomba walezi wetu na kuja kuwatembelea ndugu zetu ambao kwa wakati wote walikuwa wanalelewa na Shirika la Maria Consolata,” alisema.
David alisema mara ya mwisho kukutana na Maria na Consolata ni wakati wakiwa wamelazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Nakumbuka wakati nilipoonana na wadogo zangu waliniambia katika maisha yangu nijitahidi kuwasaidia wengine wasiojiweza hata kama nilichonacho ni kidogo, kiukweli ninayo mengi ya kujifunza kutoka kwa ndugu zangu,” alisema.
Alisema wamemfundisha kupigania ndoto zake bila kujali vikwazo vinavyoweza kumsimamisha.
Mama mkubwa, Anna alisema walikuwa wakifuatilia malezi na makuzi yao tangu walipozaliwa.
“Taarifa ya kuzaliwa kwao tuliipata siku za saba baadaye, wakati huo hakukuwa na mawasiliano kama haya ya sasa kwa hiyo niliondoka Dar es Salaam na kwenda Makete.”
Alisema alipofika na kuuliza mipango, aliambiwa tayari watoto walikuwa wamekabidhiwa kwa masista wa Shirika la Maria Consolata kulingana na hali zao.
“Tuliheshimu ridhaa ya wazazi wao waliyoitoa kuwa watoto watakuwa chini ya masista, kazi yetu ilikuwa kuja kuwaona kila tunapopata nafasi,” alisema.
Siri ya majina ya Maria na Consolata
Wengi wamekuwa na maswali kuhusu majina ya Maria na Consolata yanayofanana na shirika lililowalea. Sista Jane alisema baada ya kuzaliwa, wazazi wao waliamua kuwakabidhi kwao kulingana na hali waliyokuwa nayo na hivyo kutakiwa kuwapatia majina.
“Baba yao mzazi Mwakikuti aliposhauriwa kuwabatiza baada ya kuzaliwa kutokana na hali waliyokuwa nayo aliomba masista watoe majina hivyo yule aliyekuwepo akawaita Maria na Consolata,” alisema.
Sista Jane alisema waliwalea watoto hao katika mazingira ya kiimani wamjue Mungu na kuwafundisha upendo.
Alisema walipomaliza darasa la saba katika Shule ya Msingi ya Ikonda, wilayani Makete waliwapeka Kilolo katika shule yao ya Maria Consolata walikohitimu kidato cha nne.
Alisema wakiwa huko waliwajengea nyumba na kuwaandalia mazingira mazuri ya kuishi huku wakiwa chini ya uangalizi wa viongozi wa Maria Consolata.
Alisema hadi wanamaliza kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Udzungwa mpaka wanaingia Rucu walikuwa karibu nao kwa kila hatua.
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / kitaifa /
slider
/ SIMULIZI ILIYOJAA SIMANZII NA MACHUNGU KWA MARIA NA CONSOLATA KUTOKA HOSPITALI YA MUHIMBILI
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment