BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KIFO CHA KIUNGO MSHAMBULIAJI WA SIMBA,PATRICK MAFISANGO AACHA SIMANZI.

GARI ALILOPATA NALO AJALI HADI KUPELEKEA KIFO KWAKE KIUNGO MSHAMBULIAJI WA KLABU YA SIMBA PATRICK MUTESA MAFISANGO MAJIRA YA SAA 8:45 USIKU MEI 17 ENEO LA CHANG'OMBE JIJINI DAR ES SALAAM.
                                                          
          BEKI WA SIMBA JUMA NYOSO PAMOJA NA HOHN BOKO WAKIWA WAMEBEBA JENEZA LENYE MWILI WA KIUNGO MSHAMBULIAJI WA KLABU HIYO YA SIMBA PATRICK MAFISANGO VIWANJA VYA TCC CLUB KWA AJILI YA KUAAGA KABLA YA KWENDA NCHINI KONGO DRC AMBAPO ATAZIKWA KIPENZI CHETU.
                                      
PATRICK MUTESA MAFISANGO ENZI ZA UHAI WAKE.

SIMANZI, huzuni na vilio viliwatawala wanamichezo nchini baada ya kupata taarifa za kifo cha kiungo wa kimataifa wa Rwanda na Simba, Patrick Mutesa Mafisango (32) aliyefariki dunia jana alfajiri kwa ajali ya gari.

Mafisango anatarajiwa kuagwa leo kwenye Uwanja TCC Sigara Chang'ombe jijini Dar es Salaam kabla ya kesho kusafirishwa kuelekea nyumbani kwao DR Congo kwa mazishi .


Msemaji wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema taratibu za kuuaga mwili wa marehemu zitaanza saa nne asubuhi mpaka saa 10 jioni.

Mafisango alipata mauti hayo eneo la Veta Chang'ombe usiku wa kumkia jana saa 8.45 alipokuwa akiendesha gari akitokea Maisha Club akiwa na wenzake wanne na alipofika maeneo ya Veta wakati akijaribu kumkwepa mwendesha baiskeli ya miguu mitatu 'Guta' gari lilimshinda na kugonga mti uliosababisha gari yake kuingia mtaroni na mauti kumkuta hapo hapo.

Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo mtoto wa dada yake Orly Ilemba (24) aliyekuwamo katika gari hilo alisema jana wakati wanavuka mataa ya Veta, marehemu alikuwa katika mwendo kasi mara mbele akakutana na Guta na katika jitihada za kulikwepa akagonga mti na gari kupinduka na kutumbukia mtaroni na mauti kumkuta hapo hapo.

"Tulitoka salama Maisha Club tunarudi nyumbani marehemu alikuwa akiendesha gari katika mwendo wa kasi, tulipovuka mataa ya Veta wakati akiwa 'spidi' tuliona guta kwa mbele yetu pamoja na pikipiki sasa wakati marehemu anakwepa kwa bahati mbaya aligonga mti na gari ikadumbukia ndani ya mtaro huku nikishuhudia kichwa cha ndugu yangu kikigeukia chini kwenye sehemu ya breki na miguu kuja juu kumbe tayari alishafariki......ndipo tukaanza taratibu za kumkimbiza hospitali," alisema Ilemba.

Aliongeza kuwa,"ndani ya gari hiyo aina ya Gx100 tulikuwa watu jumla ya watano mimi, Gaspar Karemera, Bozy na mwanamke mmoja ambaye yeye hatukumfahamu jina lake mara moja akiwa amekaa mbele na marehemu ambaye mpaka sasa bado yupo hospitali akiendelea na matibabu baada ya kuumia sana maeneo ya kichwani,"alisema Ilemba.

Akithibitisha kifo cha mchezaji huyo, Mkuu wa Trafiki katika mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Prackson Lugazia alisema ajali hiyo ilitokea wakati Mafisango aliyekuwa akiendesha gari aina ya GX 100 akitoka Maisha Club akiwa na familia yake akijaribu kumkwepa mwendesha Guta.

Alisema hali hiyo ilisababisha gari hilo kuacha njia na kuingia mtaroni na kugonga miti mitatu kisha kugeuka na kuangalia lilikokuwa likitoka na baadaye kupinduka.

"Baada ya kupata taarifa za ajali hiyo majira ya saa 10 asubuhi tulifika eneo la tukio haraka iwezekanavyo, lakini hatukukuta mtu yeyote zaidi ya gari lililokuwa limepinduka,"alisema Lugazia.

Alisema,"kufatia hali hiyo ndipo tulipoanza taratibu za kumtafuta marehemu na tulianzia hospitali ya Amana, tulikwenda hospitali ya Mwananyamala na baadaye Muhimbili ambako tuliukuta mwili wake pamoja mwanamke mmoja ambaye alikuwa na majeraha mbalimbali sehemu za mwili wake," alisema Lugazia.

Akizungumza jana alfajiri jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alisema,"ni kweli Mafisango hatunaye tena, kwa sasa siwezi kuzungumza chochote huyu ni mchezaji wa timu ya Taifa ya Rwanda, ndiyo nafanya mawasiliano na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na lile la Rwanda (FERWAFA) kuangalia namna ya kuusafirisha mwili wake."

Mafisango amefariki akiwa amemaliza mkataba wake na Simba na alitarajiwa kusaini mkataba mpya juzi na leo alitarajiwa kwenda Rwanda tayari kujiunga na kikosi cha timu hiyo 'Amavubi' kinachojiandaa kwa ajili ya mechi za mchujo za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2014, zitakazochezwa mwezi ujao.

Kocha wa timu ya Taifa ya Rwanda, Sredojevich Millutin 'Micho' akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu alisema,"nimeshtuka sana, siamini Mafisango amefariki, niliongea naye jana (juzi) na nimemtumia tiketi ya ndege kwa ajili ya kujiunga na timu na nilikuwa namsisitiza asichelewe na alinihakikishia Ijumaa (leo) atakuja."

"Ukiniambia amefariki sikuelewi hapa nilipo nimechanganyikiwa, kuna vikao vinaendelea (jana), nitakupigia baadaye,"alisema Micho huku sauti yake ikionekana kuwa na majonzi.

Wakati huohuo; Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa Simba na timu ya Taifa ya Rwanda (Amavubi), Patrick Mafisango kilichotokea leo (jana) alfajiri kwa ajali ya gari Dar es Salaam.

TFF ilisema msiba huo ni mkubwa kwa familia ya mpira wa miguu kwani Mafisango kwa kipindi chote alichocheza mpira hapa nchini akiwa na timu za Azam na baadaye Simba, aliifanya kazi yake (kucheza mpira) kwa bidii.

Kifo chake ni pigo kubwa sio tu kwa familia yake na timu alizochezea, bali Ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kati ambapo changamoto za Mafisango zilikuwa dhahiri uwanjani.

BOBAN:
 
Rafiki mkubwa wa Mafisango kiungo Haruna Moshi 'Boban' alikuwa kwenye majonzi makubwa huku machozi yakimtoka bila kuzungumza lolote.

Wakizungumzia ukaribu wa mchezaji huyo na marehemu baadhi ya wachezaji wa Simba walidai Boban ndiye alikuwa rafiki mkubwa wa Mafisango na walikuwa kila mara wakiongozana pamoja katika starehe na hata wakiwa kambini.

"Boban ndio alikuwa mtu wa kwanza kusambaza habari za kifo cha Mafisango kwetu na hata aliposikia taarifa hizo alichofanya alikwenda moja kwa moja Muhimbili kwenye chumba cha maiti na kuomba kuonyeshwa mwili wa marehemu na baada ya hapo hakuzungumza lolote mpaka hapa mnavyomuona,"alisema Juma Jabu.

Mafisango alijiunga na Simba akitokea Azam Fc, mwaka jana alizaliwa Machi 7, mwaka 1987, nchini Rwanda na alikuwa akiichezea timu ya Taifa ya nchi hiyo kabla ya kusimamishwa kwa muda mrefu kutokana na utovu wa nidhamu na amerudishwa kundini na kocha Micho, lakini hata hivyo hajaweza kuitumikia timu hiyo ya Taifa lake.

Mchezaji huyo atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika timu ya Simba msimu huu uliomalizika hivi juzi na kung'aa zaidi katika Ligi hiyo kwa kupachika mabao na kutoa pasi za mwisho, ambapo Mechi ya mwisho ya Mafisango ilikuwa ni kati ya Simba dhidi ya Al Ahly Shandy Jumapili katika hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho, ambayo Simba ilitolewa kwa penati 9-8, kufuatia sare ya jumla ya mabao 3-3.

Wakati mechi ya kwanza kati ya Simba na Wasudan hao iliyochezwa hapa nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa, Mafisango aliifungia timu yake bao moja kati ya matatu yaliyoiwezesha Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 katika mchezo huo.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

1 comments:

Anonymous said...

Mbele yake nyuma yetu sisi..Marehemu Mutesa Mafisango.Alazwe pema peponi yeye alikua kipenzi chetu.