Upinzani ulitaka uchaguzi huo uahirishwe.
Nchini Angola, vituo vya kupigia kura vimefunguliwa kwa
uchaguzi mkuu ambapo watu wapatao millioni tisa wanatarjiwa kupiga kura.
Chama tawala cha MPLA ndicho kinachopewa nafasi kubwa zaidi ya
kushinda.
Hii ni mara ya tatu kwa uchaguzi mkuu kufanyika Angola tangu nchi hiyo
ilipojipatia uhuru kutoka kwa watawala wa kikoloni mwaka 1975.
Mara ya
mwisho, uchaguzi ulifanyika mwaka 2008 na kabla ya hapo mwaka 1992
ambapo matokeo ya uchaguzi yalizua mgogoro ulioitumbukiza Angola katika
awamu ya pili ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu hadi mwaka
2002.
Katika uchaguzi wa mwaka huu, zaidi ya shule na vyuo 10,000
viligeuzwa kuwa vituo vya kupigia kura. Vituo hivyo vilifunguliwa saa
moja asubuhi na vitafungwa saa 12 jioni.
Rais Jose Eduardo dos Santos wa Angola.
CHAMA tawala cha Ukombozi wa Angola - MPLA, ndicho kinachopewa nafasi
kubwa zaidi ya kuushinda uchaguzi wa leo.
Rais dos Santos, ambaye
amekuwa madarakani kwa karibu miaka 33 sasa, ataongezewa miaka mingine
mitano ya kuiongoza nchi yake. Alipokuwa akitoa hotuba ya kufunga
kampeni siku ya Jumatano, dos Santos alionyesha kuwa mwenye kujiamini:
"Ujenzi wa nchi yetu unaendelea. Kwa namna hiyo tunachangia vikubwa
katika kuboresha hali ya maisha ya raia wa Angola," alisema dos Santos.
"Maendeleo yanaletwa na mimi. Upinzani unakosoa tu na kutoa vitisho.
Lakini sisi wa MPLA tunafanya kazi kwa ajili ya maslahi ya taifa letu."
Upinzani ulitaka uchaguzi uahirishwe.
Mwanamke mmoja akiwa katika kituo cha kupigia kura.
VYAMA vya upinzani nchini humo bado havijawa na nguvu ya kuwa
kitisho kwa MPLA. Chama kikuu cha upinzani, UNITA, kilipigana vita na
utawala hadi pale kiongozi wake Jonas Savimbi alipouliwa na wanajeshi
mwaka 2002.
Mwenyekiti wa chama hicho, Isaias Samakuva, ameishutumu tume
ya uchaguzi kwa kufanya makosa na kuvunja sheria katika kuuandaa
uchaguzi wa leo. "Tulitaka uchaguzi uahirishwe.
Ni bora kusubiri kwa
mwezi mmoja hadi pale ambapo taratibu zote zitafuatwa kulingana na
sheria. Lakini hatua hiyo haijachukuliwa," alisema Samakuva.
Tume ya uchaguzi ya Angola inatakiwa kutoa matokeo ya uchaguzi katika
siku saba zijazo. Hata hivyo, matokeo ya awali yanaweza hata kutolewa
mwishoni mwa wiki hii.
Zaidi ya waangalizi 97,000 kutoka vyama 9
vinavyoshiriki kwenye uchaguzi huu watasimamia shughuli zote za upigaji
kura.
Angola ni moja ya nchi za Afrika ambazo uchumi wao unakua kwa kasi.
Ukuaji huo kwa Angola unatokana na mauzo ya mafuta. Hata hivyo, sehemu
kubwa ya vijana hawana ajira na ujenzi wa miundombinu nje ya mji mkuu
Luanda, unaendelea kwa kiwango kidogo sana.
0 comments:
Post a Comment