YADAI INAONGOZWA NA JAJI ASIYE NA SIFA,
KATIBU MKUU WA CHADEMA DK SLAA.
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeipinga tume ya
kuchunguza mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa Channel Ten, Daudi Mwangosi,
iliyoundwa na Waziri wa Mambo wa Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, kwa
maelezo kuwa inaongozwa na jaji asiye na sifa.
Kimesema kuwa Jaji huyo mstaafu, Stephen Ihema, anafahamika ni mtu
asiyejua kazi, kwani ameshindwa kutoa hukumu katika kesi zaidi ya 300.
Akizungumza na waandishi jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa
Masuala ya Sheria, Katiba na Haki za Binadamu wa chama hicho, Tundu
Lissu, alisema kutokana na Jaji Ihema kutoweza kazi, hata Jaji Bernard
Luanda alipata kumkosoa kwa kutoa waraka kwa majaji wote mwaka 2005.
“Kama mnafuatilia taarifa za hivi karibuni, Ihema ni mmoja wa majaji
waliopo kinyume cha sheria na Katiba. Aliteuliwa kuwa jaji enzi za
Benjamin Mkapa, ilipofika mwaka 2003 kwa sababu hakuwa anajua sheria,”
alisema.
Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki, aliongeza kuwa Ihema
hajui kazi ya ujaji na kwamba alisharundika zaidi ya kesi 300 ambazo
anashindwa kuziandikia hukumu. Na kuwa mtu ambaye anajulikana kutokuwa
na uwezo wowote wa kufanya kazi ya kisheria.
“Ndugu zangu na hili naomba nirudie maana wasiseme tumeanza maneno
yetu, mwaka 2003 kabla mimi sijawa mbunge kuna mtu anaitwa Joram Alute,
ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Singida kwa sababu ya ubovu wa Jaji
Ihema, Joram alimwandikia Rais Mkapa barua ya kumuomba kumuondoa Jaji
Ihema Mahakama Kuu, kwa sababu hakuwa na uwezo wowote wa kufanya kazi ya
ujaji.
Miaka karibu 10 wana CCM, Joram Alute, si CHADEMA, alisema hawezi
kazi, aidha ni mvivu au hajui namna ya kuandika hukumu, hafai kuwa
jaji,” alisema Lissu.
Aliongeza kuwa mwaka 2005 Jaji Ihema alikuwa amemaliza mkataba wa
kwanza na kupewa mwingine wa kazi ya ujaji, hali ambayo ilimfanya Jaji
Bernard Luanda (sasa Jaji wa Mahakama ya Rufaa), baada ya kuandikiwa na
Jaji Manento kuwa Ihema amepewa mkataba wa ujaji, aliandika waraka
uliosambazwa kwa majaji wote kuwa Ihema si jaji kwa mujibu wa Katiba.
Alisema kwa mujibu wa sheria za nchi, majaji wanateuliwa, hivyo Jaji Ihema kupewa mkataba ni kinyume cha sheria na katiba.
Lissu alieleza kuwa hata alipopelekwa Tume ya Maadili ya Viongozi wa
Umma, tume hiyo ilikuwa ni ya kuficha uchafu na madhambi ya viongozi,
kwani ilikuwa kimya kwa miaka yote huku viongozi wakishiriki kufilisi
taifa.
Alisema kutokana na maelezo hayo ni dhahiri kuwa Ihema hana uwezo na
pia maadili yake ni ya mashaka, kwani hilo linafahamika ndani ya
mahakama.
Pamoja na hilo, alisema tume hiyo imeundwa kwa lengo la kurekebisha
mambo baada ya Jeshi la Polisi kukamatwa mchana kweupe wakifanya mauaji.
“Ni tume ambayo lengo lake si kuchunguza mauaji, ni kuondoa hii picha
ya mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi hadhaharani…hii ndivyo
tunavyoiangalia.
Kwa kuwa si tume ya kuchunguza mauaji sisi kama chama hatutaiunga
mkono na tutawashauri wananchi wa Tanzania, wawe wanachama wetu, wasiwe
wanachama wetu, wasiiunge mkono,” alisema.
Nchimbi akosolewa
Lissu alisema kwa mujibu wa sheria ya kuunda tume za uchunguzi mwaka
1962 sura ya 29, anayepaswa kuunda tume ni Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na kutoa hadidu rejea na kwamba kulingana na utaratibu huo
si jukumu la waziri kuunda tume.
Alisema tume za aina hiyo zinatoa ripoti kwa rais au zinaweza kutoa
taarifa hadharani endapo rais ataelekeza hivyo katika hadidu rejea.
“Hivyo kwa matukio makubwa ya kitaifa yanayotokea, kisheria ni jukumu
la rais, si jukumu la waziri ambaye anawasimamia watuhumiwa wa hicho
kinachotakiwa kuchunguzwa.
Kwa hiyo katika upeo huo wa kisheria, Waziri Nchimbi hana mamlaka ya kuunda tume ya kuchunguza mauaji hayo,” alisema.
Lissu alifafanua kuwa walioua ni polisi ambao inawezekana waliamriwa
waue na wakubwa zao kisiasa (waziri) au kiutendaji (IGP na maofisa
wengine wa jeshi), hivyo kama unachunguza mauaji yaliyofanyika waziwazi,
inawezekana yamefanywa kwa amri za kisiasa au kiutendaji.
Hivyo alihoji kama tume hiyo ina uwezo wa kumhoji waziri au IGP na
kusema kuwa: “Tume hii ni danganya toto, ya kitchen party, pengine na ya
marafiki, ili kuondoa picha mbaya kwa Jeshi la Polisi,” alisema.
Wajumbe wake waguswa
Lissu alisema Naibu Kamishna wa Polisi, Isaya Mungulu, kutoka makao
makuu hana uwezo kwa kumuita waziri au IGP kwa ajili ya kumhoji
kuhusiana na mauaji hayo.
Kuhusu mtaalamu wa mabomu, Wema Wapo, kutoka Jeshi la Ulinzi wa
Wananchi wa Tanzania (JWTZ) alihoji kuwa anakwenda kuchunguza kitu gani
kisichojulikana, kwani katika picha muuaji anajulikana.
“Inaonekana ni bomu la machozi ambalo alipigwa nalo, ambalo
limemchanachana. Sasa ni kitu gani kisichojulikana. Sasa unaita mtaalamu
achunguze mlipuko upi ambao haujulikani?” alihoji.
Kwa upande wa Theopili Makunga kutoka Jukwaa la Wahariri (TEF) na Pili
Mtambalike kutoka Baraza la Habari Tanzania (MCT), alisema hao ni
waandishi wa habari na kuhoji iwapo wana utaalamu wa kuchunguza vifo.
“Hii ni tume ya marafiki, yenye lengo la kukosha mauaji yaliyofanywa
na marafiki, kwa vyovyote vile hii si tume halali ya kuchunguza mauaji
ya Mwangosi,” alisema Lissu.
Hadidu rejea zapingwa
Lissu alihoji ni mtu gani asiyefahamu chanzo cha mauaji hayo, kwani
vyombo vya habari vimemuonyesha kupitia picha, hivyo kuhoji tume hiyo
inakwenda kuchunguza kitu gani.
Kuhusu swali kama kweli kuna uhasama kati ya polisi mkoani Iringa na
waandishi, alihoji iwapo tume hiyo inakwenda kuchunguza mauaji ama
uhasama.
Kwa upande wa swali kama nguvu iliyotumika na polisi ilikuwa sahihi,
alisema kuwa hilo ni suala la kisheria na pia kunahitajika ushahidi.
“Kuhusu swali linalohoji mahusiano kati ya polisi na vyama vya siasa.
Hili liko wazi kabisa kwa sababu sijawahi kusikia Jeshi la Polisi
limevunja mikutano ya CCM, kwa hiyo hapa wanakwenda kuichunguza
CHADEMA,” alisema.
Aliongeza kuwa iwapo wanataka kuchunguza suala hilo kwa nini Mungulu
yupo kwenye tume hiyo na hakuna mtu wa CHADEMA wala Msajili wa Vyama vya
Siasa au mwakilishi wake.
“Hii si tume ya kuchunguza mauaji, ni ya kufunika mauaji haya…hatuwezi kukubaliana na tume hii,” alisema.
Mbali na hilo, alisema kuna haja ya kuchunguza matukio mbalimbali ya
mauaji yaliyotokea hivi karibuni likiwemo la Morogoro, Arusha, Igunga na
Arumeru Mashariki.
“Matukio yote haya hayajachunguzwa inavyostahili. Hatutaki mambo yaishe hivi hivi,” alisema.
Mapendekezo yao
Kutokana na hali hiyo, alisema chama hicho kinamtaka Rais Jakaya
Kikwete kuunda tume ya uchunguzi wa mauaji ambayo itaongozwa na majaji
waadilifu na kwamba itakuwa bora iwapo watatoka Mahakama ya Rufaa na
Mahakama Kuu, ambao watafanya uchunguzi wa wazi.
“Katika tume hiyo mashahidi watakuwa wakiitwa hadharani. Tume za aina
hii hazipo, lakini kwa mujibu wa sheria Rais anaweza kuunda tume hiyo.
Hatutaki uchunguzi wa kificho ambao unaonesha polisi hawakukosea,”
alisema.
Alieleza kuwa tume hiyo itakuwa na mamlaka ya kumuita mtu yeyote
isipokuwa rais.
Na kwamba kwa kuwa muuaji anajulikana, chama hicho
kinataka askari wote waliohusika wakamatwe na kufunguliwa kesi ya
mauaji.
“Tunajua si wote walioua, ila katika sheria kuna kitu kinaitwa common
intension, mmoja ameua, lakini alioshirikiana nao wanahusika.
Hili
linawezekana kwa kuwa kuna ushahidi,” alisema.
Alisema iwapo rais hataunda tume hiyo, kuna njia nyingi za kuendelea
na suala hilo, na kusema hilo chama kinapaswa kutoa kauli.
Wataka Nchimbi ajiuzulu
Katika hatua nyingine, Lissu alisema kutokana na tukio hilo, Waziri
Nchimbi anapaswa kuwajibika kisiasa kwa kujiuzulu, kwani hawezi
kuendelea kuwa waziri na kuheshimika kutokana na tukio hilo.
“Kama ana chembe ya uadilifu afuate nyayo za Mwinyi (Ali Hassan
Mwinyi) miaka 36 iliyopita ambaye alijiuzulu uwaziri.
Nchimbi hawezi
kuwa waziri na kuendelea kuheshimika kama anaongoza jeshi la wauaji.
Akishindwa kujiuzulu rais amfukuze kazi,” alisema.
Alieleza kuwa mauaji ya aina hiyo ni ya kisiasa na kuongeza kuwa jeshi hilo limekuwa likifanya kazi kwa niaba ya CCM.
Tendwa aibuka
Mauaji ya Daudi Mwangosi, anayedaiwa kuuawa kwa bomu na askari polisi
mkoani Iringa, yamemuibua Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John
Tendwa, ambaye ametishia kuvifuta vyama vinavyojihusisha na siasa za
vurugu.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Tendwa ambaye
alitumia muda mwingi kuwatisha CHADEMA pia amelionya Jeshi la Polisi na
kulitaka lifanye kazi zake kwa wajibu wa sheria za nchi.
Tendwa ambaye ofisi yake imekuwa ikilalamikiwa na vyama vya upinzani
kuwa inashindwa kutekeleza wajibu wake kutokana na kuegemea upande wa
Chama tawala cha CCM, alisema kuwa demokrasia ya sasa imekua na
kusababisha vifo vya raia wasio na hatia.
Alisema hawezi kuvumilia siasa za vu
rugu zinazohatarisha amani ya
taifa lililopata uhuru wake miaka 50 iliyopita kwa kisingizio cha
operesheni za ukombozi.
Tendwa alisema haoni haja ya CHADEMA kuendelea na operesheni yao ya
Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) wakati huu ambao si kipindi cha uchaguzi,
hivyo kutishia kukifuta chama hicho alichodai mikutano yake imekuwa
ikizusha vurugu.
Aliainisha kuwa kuanzia mwaka jana hadi sasa mauaji kadhaa ya raia
yametokea katika mikutano ya kisiasa katika mikoa ya Arusha, Singida,
Morogoro na Iringa na kwamba hali hiyo haiwezekani kusema taifa ni huru.
Alisema kuwa Agosti 10 mwaka huu, mkutano wa vyama vya siasa na Jeshi
la Polisi ulifanyika na kuzungumzia masuala mbalimbali likiwamo la amani
nchini, kufanyika kwa mikutano ya vyama, wajibu wa vyama vya siasa kwa
kufuata sheria za nchi na wajibu wa Jeshi la Polisi nchini.
Tendwa aliongeza kuwa kutokana na kuwapo kwa sheria ya mikutano ya
vyama vya siasa nchini, ikitokea chama chochote cha siasa kitaleta chuki
na uvunjifu wa amani kitapaswa kufutwa.
“Kutokana na hali tuliyoifikia kwa sasa inatisha, hivyo vyama vya siasa viondoe uchochezi,” aliongeza.
Pia amelitaka Jeshi la Polisi kutimiza wajibu wake wa kulinda raia
pamoja na mali zao na kuwataka wavitumie vyombo vyao kwa ustaarabu.
DCI asuswa Iringa
Jeshi la Polisi nchini limeanza kuonja shuluba ya matukio yao
kususiwa na waandishi wa habari, ambapo jana Mkurugenzi wa Makosa ya
Jinai nchini, DCI Robert Manumba, alikuwa wa kwanza kukumbwa na adha
hiyo mkoani Iringa.
Waandishi wa habari wameazimia kutoripoti taarifa zozote za jeshi hilo
hadi hapo wale waliohusika katika kusababisha kifo cha mwanahabari,
Daudi Mwangosi, watakapokuwa wamekamatwa na kuchukuliwa hatua.
Manumba ambaye jana alikuwa akitaka kutoa taarifa za awali juu ya
uchunguzi wa kifo cha Mwangosi, alijikuta katika wakati mgumu baada ya
wanahabari hao kugoma kabisa kwenda kumsikiliza.
Pia waandishi hao wamekosoa tume iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, wakisema haijakidhi haja wala
kuzingatia uwiano, kwa kile walichoeleza kuwa hakuna hata klabu moja ya
waandishi wa habari iliyoshirikishwa.
Awali waandishi hao walitoa masharti kwa DCI wakitaka awepo peke yake
katika chumba cha mikutano lakini Manumba alijitetea kuwa tamko
alilotaka kutoa ni lazima na maofisa hao walisikie.
“Jamani punguzeni jazba juu ya hili, ninajua mna mchango mkubwa katika
maendeleo ya taifa hili na suala hili limemgusa kila mmoja, hasa ninyi
waandishi wa habari, hivyo naomba mnisikilize na mjue tunataka kuwaambia
nini,” alisema DCI Manumba bila mafanikio.
Wakati huo huo, waandishi wa habari mkoani hapa, walisema wakati tume
iliyoundwa na Dk. Nchimbi haijaanza kazi yake rasmi ni vema Kamanda wa
Polisi mkoani humo akaachia madaraka yake kwa muda ili kupisha uchunguzi
huru.
Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa, Frank
Leonard, alisema mbali na kumtaka Kamuhanda kujiuzulu pia ni wakati
muafaka kwa tume iliyoundwa ikawahusisha na viongozi wa klabu ya
waandishi.
TUCTA yamlilia Mwangosi
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (Tucta), limemlia
aliyekuwa mwandishi wa kituo cha runinga cha Channel Ten, marehemu Daudi
Mwangosi, likisema alikuwa ni mchapa kazi.
Katibu Mkuu wa Tucta, Hezron Kaaya, alisema kuwa ni jambo la
kusikitisha na kushangaza kwa mwandishi kuuawa wakati akitekeleza
majukumu yake.
“Kwa kweli Tucta kati ya mambo ambayo yametuuma na kutusikitisha ni
kifo cha Mwangosi kinachoripotiwa kufanywa na Jeshi la Polisi, hasa
kitendo cha kusambaratishwa mwili wake, kwani hata mnyama anapouawa
katika mawindo huwa hauawi kwa namna ile,” alisema.
Kaaya aliongeza kuwa ni jambo la kusikitisha kwa kuwa kifo kile
kitachukua muda mrefu kwa Watanzania kukisahau kwani hakuwa na kosa
lolote alilolifanya mpaka kuuawa namna ile.
Aliongeza kuwa kwa hali ilivyo sasa taifa linaelekea pabaya, kwa
sababu haki ya mnyonge haizingatiwi tena na wenye nguvu, akitoa mfano
kuwa wanyonge wanapodai haki yao jibu rahisi ni kusambaratishwa kwa
mabomu na virungu vya polisi.
Alisema endapo hali hiyo itaachwa iendelee hivyo, kunaweza kutokea
maafa makubwa kwa wananchi waliochoka kuonewa na kudhulumiwa haki zao.
Kaaya alibainisha kuwa Watanzania wengi wameuawa katika matukio ya
kisiasa na hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa kukomesha hali hiyo
isiendelee kutokea, badala yake zinaundwa tume ambazo hata hivyo
hazijulikani zinakoishia zaidi ya kutumia fedha za walala hoi.
0 comments:
Post a Comment