KUATIA kitendo cha maadui wa Uislamu cha kumvunjia heshima
Mtume Mtukufu Muhammad SAW, Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa
Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ujumbe kwa taifa la Iran na umma mkubwa wa
Kiislamu akisema kuwa, siasa za kihasama za Wazayuni, Marekani na
vinara wengine wa ubeberu wa kimataifa ndizo zilizohusika na harakati
hiyo iliyojaa shari.
Ameweka wazi sababu za kinyongo cha Wazayuni dhidi ya Uislamu na
Qur'ani na akasisitiza kuwa, kama wanasiasa wa Marekani wanasema kweli
katika madai yao kwamba hawakuhusika katika jinai hii, basi wanapaswa
kuwapa adhabu inayonasibiana na jinai hii wale wote waliohusika na
uhalifu huo mkubwa na waliowasaidia kifedha ambao wamezitia simanzi na
maumivu nyoyo za mataifa ya Waislamu.
Ayatullah Khamenei amesema lau kama mabeberu wa kimataifa wasingeunga
mkono sehemu za kwanza za mnyororo huu muovu yaani Salman Rushdie,
mchora vikatuni wa Denmark na makasisi wa Kimarekani waliochoma moto
Qur'ani, na kuacha kuagiza makumi ya filamu zinazopiga vita Uislamu
kutoka kwenye makampuni ya wawekezaji wa Kizayuni basi hali isingefikia
kiwango hiki cha kutenda dhambi kubwa na isiyosameheka.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema Waislamu kote duniani
wanapaswa kuelewa kwamba, harakati hizi zilizofeli za maadui dhidi ya
mwamko wa Kiislamu ni kielelezo cha adhama na umuhimu wa mwamko huo na
bishara ya kustawi kwake zaidi.
0 comments:
Post a Comment