
MARAIS wa Sudan na Sudan Kusini wameanzisha mazungumzo kumaliza
uhasama kati ya nchi zao. Katika mazungumzo ambayo yanafanyika nchini
Ethiopia, unatafutwa muafaka juu ya masuala nyeti kama vile mafuta na
mpaka.
Rais Omar al-Bashir wa Sudan na mwenzake wa Sudan Kusini, Salva Kiir,
wamekutana usiku wa kuamikia leo katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis
Ababa, Mazungumzo yao ya muda wa masaa mawili yameanzisha mchakato wa
kutafuta suluhu kwa matatizo katika uhusiano wa nchi hizo jirani, ambazo
hadi Julai mwaka jana zilikuwa nchi moja.
Msemaji wa serikali ya Sudan Kusini, Atif Kiir, amesema bado zipo
tofauti kati ya pande mbili zinazozungumza, ila akaelezea imani kwamba
pengo lililopo litapungua hadi kufikia makubaliano.
Rais Al-Bashir wa Sudan na Salva Kiir wa Sudan Kusini
Marais al-Bashir na Salva Kiir walizungumza hadi usiku wa manane, na
ripoti za waandishi zinasema walitoka ndani ya chumba cha mkutano
wakionekana wachangamfu.
Mazungumzo yao yanaendelea leo hii, pengine
chini ya upatanishi wa waziri mkuu mpya wa Ethiopia, Hailemariam
Desalegn.
Badr el-din Abdullah, msemaji wa serikali ya Khartoum pia anakubaliana
na mwenzake wa Sudan Kusini kwamba bado yapo mambo ambayo hayajaafikiwa,
na kuongeza kuwa masuala ya kiusalama ndiyo changamoto kubwa iliyopo.
Balozi wa Sudan Kusini mjini Khartoum, Mayen Dut Wol, amesema bila
kupata maelewano juu ya masuala hayo ya kiusalama, itakuwa vigumu
kuyatekeleza mengine yatakayoafikiwa.
''Bila kufikia maelewano juu ya masuala ya kiusalama na mpaka, nina
uhakika kwamba hata tukisaini makubaliano juu ya mafuta na mengine ya
kiuchumi, utekelezaji wake utakuwa mgumu sana.'' Amesema Wol.
Abyei bado kikwazo
Kila upande unadai kuwa eneo la Abyei lenye mafuta ni lake
Umiliki wa jimbo linalozozaniwa la Abyei, na kutenga eneo lisilo na
shughuli zozote za kijeshi kati ya Sudan na Sudan Kusini, ni miongoni
mwa mada ngumu katika mkutano huo.
Eneo hilo, linaweza kuukatiza msaada
kwa waasi wa katika majimbo ya Kordofan Kusini na Blue Nile, ambao Sudan
inadai wanaungwa mkono na serikali ya mjini Juba.
Mikondo kadhaa ya mazungumzo kati ya nchi hizo mbili imekwishaambulia
patupu, lakini sasa, kukutana ana kwa ana kwa marais wawili, na mbinyo
wa Umoja wa Mataifa ambao unaambatana na kitisho cha kuziwekea nchi hizo
vikwazo iwapo zitashindwa kuelewana, vimetoa matumaini mapya ya
mafanikio.
Muda wa mwisho uliowekwa na Umoja wa Mataifa kwa marais wa nchi hizo
kuelewana juu ya masuala ambayo hayakupatiwa ufumbuzi wakati Sudan
ilipopata Uhuru wake Julai mwaka jana, ulimalizika Jumamosi iliyopita.
Muda huo uliwekwa baada ya makabiliano makali baina ya nchi hizo, baada
ya jeshi la Sudan Kusini kulikalia kwa muda eneo lenye kuzalisha mafuta
la Heglig, na Sudan kujibu kwa mashambulizi ya ndege za kivita.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amewatolea wito marais
Al-Bashir na Kiir kumaliza tofauti zao, ili mkutano huu wa kilele uweke
kikomo kwenye kipindi cha mizozo.

0 comments:
Post a Comment