BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

Utiaji Saini Ujenzi Wa Barabara Zanzibar


Na: Nafisa Madai-Maelezo Zanzíbar

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imetiliana saini Ujenzi wa Barabara mbili za Koani-Jumbi,Jendele ,Cheju hadi Kaebona na barabara ya Kizimbani-Kiboje kwa kiwango cha lami ambao utagharimu shilingi bilioni 14.833.

Hayo yamefahamika wakati wa utiaji saini wa makubaliano ya ujenzi huo kati ya Wizara ya Mawasiliano na Miundombinu na Kampuni ya M/S db Shapriya + Co.Ltd yaliyofanyika Ukumbi wa Hoteli ya Bwawani mjini Unguja.

Makubaliano hayo yametiwa saini na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Miundombinu Dk Vuai Lila kwa niaba ya Serikali ambapo kwa upande wa Kampuni hiyo iliwakilishwa na Fundi Mkuu Sathish Babu.

Akizungumza mara baada ya utiaji saini katika hafla hiyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, Dk Vuai Lila, alisema fedha hizo zimetolewa na Benki ya Maendeleo ya Kiarabu kwa Maendeleo ya nchi za Afrika (BADEA), ambayo imetoa dola za marekani milioni 8 wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa dola za kimarekani milioni 2.36.

Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa BADEA itachangia shilingi bilioni 11.454 ikiwa ni sawa na asilimia 72.22, ambapo Serikali itachangia shilingi bilioni 3.379 sawa na asilimia 22.78.
Aidha amesema zaidi ya shilingi milioni 900, atalipwa msimamizi wa mradi huo na BADEA, ambapo Serikali italipa shilingi milioni 500 ikiwa ni fidia ya mazao na nyumba katika maeneo yatakayopita barabara hizo.
Dk.Lila amesema mradi huo utaanza wakati wowote kuanzia sasa ambapo unatarajiwa kukamilika baada ya miezi 17.

Amesema ujenzi wa barabara hizo utaimarisha miundombinu ambayo ni chachu ya maendeleo na kuwakwamua wananchi wa maeneo hayo kiuchumi ili kuondokana na umasikini.

Amewataka viongozi na wananchi wanaaoishi karibu na sehemu zitakazopita barabara kuzidisha ushirikiano ili kuleta ufanisi katika ujenzi huo.

"Mradi huu ni muhimu kwani utasaidia sana kusukuma maendeleo ya nchi yetu hivyo tunaomba kuweko mashirikiano ili uweze kukamilika kama ulivyokusudiwa", alisema Dk Lila.

Nae Mkandarasi Paul Bird, kutoka Kampuni ya DB Shapriya + Co.Ltd, aliihakikishia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutekeleza ujenzi huo kwa wakati sambamba na kujenga kwa kiwango kinachokubaliwa.

"Naahidi kuwa mradi huu utakwenda kama ulivyopangwa hivyo nataka mashirikiano kwa wananchi na hata viongozi wa sehemu utakaopita mradi huo", amesema Bird.

Kwa upande wake Diwani wa Koani Shaaban Jabu Kitwana, ameahidi kutoa mashirikiano ya karibu ili kuona kuwa hakuna vikwazo vitakavyotokea katika kipindi chote cha kazi hiyo.

Aidha Kitwana aliishukuru Serikali kusikia kilio chao cha siku nyingi kwa kuwa itasaidia sana kuleta maenedeleo katika vijiji husika vya mradi huo wa barabara.

IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: