WAZIRI Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesifu ukuaji wa
demokrasia nchini mwake, na kusema kuwa chama chake kinachotawala
kilicho na misingi ya Uislamu, kimekuwa mfano wa kuingwa kwa nchi za
Kiislamu.
Akihutubia maelfu ya wajumbe na viongozi wa mikoa wakati wa mkutano
mkuu wa chama hicho siku ya Jumapili, Erdogan alisema zama za mapinduzi
ya kijeshi katika taifa hilo la watu milioni 75 zimekwisha.
Mkutano huo ulimchagua Racep Tayyip Erdogan kukiongoza chama cha
Justice and Development, maarufu kama AK Party kuwa kiongozi wake kwa
muhula mwingine wa miaka mitatu bila upinzani.
Huu ndiyo ulikuwa mkutano
wake wa mwisho kama waziri mkuu na kiongozi wa chama hicho kwa vile
sheria za chama hicho zinamzuia mtu kugombea uongozi kwa zaidi ya mihula
mitatu mfululizo.
Waziri Mkuu Tayyip Erdogan akisalimiwa na wafauasi wake wakati akiingia katika mkutano mkuu wa chama tawala nchini humo cha AK.
Waziri mkuu huyo ambaye anatizamiwa kugombea urais mwaka 2014, alisema
katika hotuba yake iliyokuwa inakatizwa na vifijo vya mara kwa mara,
kuwa huduma ni muhimu kuliko vyeo.
Matamshi hayo yalitafsiriwa na
wachambuzi kama dalili za wazi kuwa anataka kuwa rais wa kwanza
kuchaguliwa na umma chini ya marekebisho ya katiba ya mwaka 2007
yanayoweka mihula miwili ya miaka mitano kila mmoja.
"Shabaha yetu ni kusherehekea miaka mia moja tukiwa nchi ya Jamhuri
ifikapo mwaka 2023, na baada ya hapo tutajitahidi kuijenga Uturuki
kuelekea Jubili ya miaka alfu moja," alisema Erdogan.
Aahidi kushughulikia suala la Wakurdi
Katika hotuba yake iliyodumu kwa karibu saa mbili na nusu, na ambayo
ililenga kubainisha ajenda ya chama chake kwa kipindi cha miaka kumi
ijayo, Erdogan aliahidi kuirekebisha katiba ya Uturuki na kuanzisha
ukurasa mpya kuhusiana na jamii ya wakurdi milioni 15 wa Uturuki.
Viongozi mbalimbali wakiwemo rais wa Misri Mohammad Mursi, rais wa
Kyrgystan Almazbek Atambayev, rais wa jimbo huru la Wakurdi nchini Iraq,
Masoud Barzani na kiongozi wa Hamas Khaled Mashaal walikuwa miongoni
mwa wageni waalikwa.
Waziri mkuu Tayyip Erdogan na rais wa Misri Mohammed Mursi.
Rais Mursi ambaye alikuwa mgeni rasmi katika Mkutano huo alikisifu
chama cha hicho tawala kama chanzo cha hamasa kwa kanda.
"Nimekuja
kuonyesha si tu mapenzi yangu, heshima na uvutiwaji kwa njia ya ufanisi
iliyochukuliwa na Uturuki, lakini kufikisha pia salamu za raia wa Misri
na uvutiwaji wao kwa mafanikio mliyoyapata."
Chini ya uongozi wa Erdogan, chama cha AK kimefanikiwa kushinda
uchaguzi mara tatu mfululizo tangu mwaka 2002, na kuhitimisha historia
ya serikali dhaifu za muungano ambazo zilikuwa zikipinduliwa mara kwa
mara na wanajeshi.
Pato la mtu moja moja nalo limeongezeka mara karibu
mara tatu na Uturuki imerejesha ushawishi wake kama dola kubwa katika
kanda ya mashariki ya kati, huku wsahirika wake wakiutizama mchanganyiko
wa utulivu wa demokrasia na na utamaduni wa Kiislamu kama njia ya mfano
kwa kanda hiyo inayobadilikabadilika.
0 comments:
Post a Comment