HALI ya wasi wasi yazuka katika mji mkuu wa Kenya Nairobi
kufuatia shambulio la bomu katika kanisa liliouwa mtoto mmoja na
kujeruhi wengine kadhaa na kusababisha ghasia za kulipiza kisasi dhidi
ya jamii ya Wasomali.
Makoti ya watoto na viatu vilivyorowa damu vilikuwa vimetapakaa kwenye
sakafu ya kanisa la Anglikana la Mtakatifu Polycarp.
Mkuu wa polisi wa
jiji la Nairobi Moses Nyakwama ameliambia shirika la habari la AFP
kwamba mtoto mmoja ameuwawa na wengine watatu walijeruhiwa vibaya na
kwamba wanashuku shambulio hilo limefanywa na watu wanaoliunga mkono
kundi la Al Shabaab.
Amesema hiyo ni mikiki ya mfa maji ambaye hawachi kutapatapa na kwamba
hivi karibuni polisi ya Kenya imewakamata watuhumiwa kadhaa kuhusiana na
maguruneti.
Janet Wanja aliyeshuhudia tukio hilo amesema alikuwa ndio
kwanza anaingia kanisani katika kanisa hilo lilioko eneo la Pangani
wakati mripuko ulipolitingisha jengo la kanisa.
Hali ilivyo baada ya mripuko kanisani.
Amesema "Nimesikia sauti kubwa ya mripuko na baadae vilio vya watoto,
nilichanganyikiwa kwa kile nilichokishuhudia, watoto wakiwa na majeraha
na damu ikiwa imetapakaa kila mahala".
Wanja anauliza kwa nini
wanashambulia kanisa?
Wilfred Mbithi mkuu wa operesheni za polisi mjini Nairobi amekaririwa
akisema baadhi ya mashahidi wamewaambia kwamba waliwaona wanaume wawili
wenye asili ya Kisomali wakikimbilia nyuma ya kanisa ambapo ndiko
kulikotokea mripuko huo.
Wakati ikutuhumiwa kwamba watu hao ndio
waliolirusha guruneti hilo kanisani,polisi pia inachunguza uwezekano
kwamba mripuko huo umesababishwa na bomu ambalo lilikuwa limetegwa
kanisani humo na mapema.
Afisa wa kanisa Livingstone Muiruri amesema watoto tisa wamejeruhiwa
katika mripuko huo na kwamba watoto waliokuwa wakihudhuria misa walikuwa
na umri wa kati ya miaka sita na kumi.
Baada ya shambulio hilo watu
wenye hasira wanaofikia 100 waliwavurumishia mawe Wasomali,majengo na
magari yanayomilikiwa na jamii hiyo lakini hakuna mtu aliyeripotiwa
kujeruhiwa katika purukushani hizo zilizotokea katika kiunga cha
Pangani.
Polisi ya Kenya iliwatawanya watu hao wakati Wasomali wakikimbilia usalama wao kwa kujifungia majumbani mwao.
Pangani imepakana na mtaa wa Eastleigh uliopachikwa jina la "Mogadishu
ndogo" kutokana na wakaazi wake wengi kuwa ni wakimbizi wa Somali au
Wakenya wenye asili ya Somali.
Baadae hapo jana polisi wawili wa Kenya
waliuwawa kwa kupigwa risasi katika mji wa kaskazini wa Garissa ulioko
karibu na mpaka na Somalia.
Majeshi ya Kenya nchini Somalia.
Herman Ndiemma naibu mkuu wa polisi wa mji wa Garissa ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba polisi hao waliuwawa wakati walipokuwa wakielekea kwenye chuo cha ufundi ambapo walipangiwa kukilinda.
Ndiema amesema wanashuku wafuasi wa kundi la Al Shabaab
kuhusika na shambulio hilo na kwamba polisi imeimarisha usalama katika
mji huo.
Wakaazi wengi wa mji wa Garissa ni wale wenye asili ya Kisomali na mji huo uko kilomita 180 kutoka mpaka wa Kenya na Somalia.
Polisi nchini Kenya ilitowa onyo kwamba kuna hatari ya kufanyika
mashambulizi baada ya vikosi vya Kenya kuongoza mashambulzi dhidi ya
waasi wa Al Shabaab katika mji wa Kismayo nchini Somalia.
Magazeti ya
Kenya hapo jana yamesema polisi imegunduwa kifaa cha kutengenezea mabomu
kwenye mkoba uliokuwemo kwenye basi lililokuwa limebeba abiria kutoka
Garissa kwenda Nairobi hapo Ijumaa.
Kwa mujibu wa magazeti hayo abiria
wote 60 waliokuwemo ndani ya basi hilo wametiwa nguvuni baada ya kila
mmoja kuukana mzigo huo.
Washambuliaji walifanya mashambulizi kwa kutumia bunduki na mabomu kwa
makanisa mawili huko Garissa hapo mwezi wa Julai na kuuwa takriban watu
17.
0 comments:
Post a Comment