KIKOSI MAALUM CHA ASKARI WA MEXICO KIKIWA KIMEWADHIBITI WAHALIFU.
JESHI maalumu la wanamaji nchini Mexico
limetangaza kufanikiwa kumkamata kiongozi wa juu wa kundi Zetas
linalojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya nchini humo.
Wanajeshi hao wamesema kuwa walimkamata Ivan Velazquez kiongozi
wa juu wa kundi la Zetas kwenye mji wa San Luis Potosi na kuongeza kuwa
kukamatwa kwake kumetokana na mgawanyiko ambao umeanza kujitokeza ndani
ya makundi ya uuzaji dawa za kulevya nchini humo.
Ivan anatajwa kuwa miongoni mwa viongozi wa juu wa kundi hilo ambao
walikuwa wanasakwa na Serikali kwa muda mrefu kwa tuhuma za kushiriki
mauaji ya raia wasio na hatia mjini Mexico.
Kukamatwa kwa kiongozi huyo kumeonekana kuwa ni mafanikio kwenye
operesheni iliyoanzishwa na rais Felipe Calderon ambaye ameapa Serikali
yake kukabiliana na makundi makubwa ya uuzaji dawa za kulevya nchini
humo.
Mtuhumiwa huyo anatarajiwa kuonyeshwa mbele ya waandishi wa habari
katika tukio ambalo linasubiriwa kufanyika muda wowote kuanzia sasa
ambapo wananchi watapata nafasi ya kumshuhudia kiongozi huyo.
Ivan ambaye hufahamika pia kwa jina la El Taliban amekuwa mmoja wa
waasisi wa kundi la zetas lilioanza kujipatia umaarufu nchini humo
kwenye miaka ya 1990 ambapo limekuwa likifanya biashara ya uuzaji dawa
za kulevya.
0 comments:
Post a Comment