MJUMBE wa amani wa kimataifa nchini Syria Lakhdar Brahimi Jumamosi amesisitiza mjini Damascus haja ya kusitisha mapigano, ili
kuzuwia umwagikaji zaidi wa damu nchini nchini humo.
Brahimi alikutana na waziri wa mambo ya kigeni Walid Muallem pamoja na
viongozi wa upinzani wanaokubalika na rais Bashar al-Assad , katika
juhudi za kupata kuungwa mkono mpango wake wa kupatikana usitishaji wa
mapigano , wakati wa sikukuu muhimu ya Kiislamu wiki ijayo.
Lakini mazungumzo hayo yaligubikwa na hali ya wasi wasi katika nchi
jirani ya Lebanon , ambako viongozi wa upinzani pamoja na waziri mkuu
walihusisha shambulio lililosababisha mauaji ya afisa wa ngazi ya juu wa
upelelezi na utawala wa Syria .
Mjumbe wa kimataifa Lakhdar Brahimi.
Nchini Syria kiasi watu 108 wameuwawa katika ghasia siku ya Jumamosi ,
42 kati yao ni raia, limeripoti shirika la kuangalia haki za binadamu
nchini humo, wakati mapigano yakiendelea katika maeneo ya kaskazini na
kuzunguka mji wa Damascus.
Kusitisha mapigano.
Wizara ya mambo ya kigeni imesema waziri Muallem amejadili pamoja na
Brahimi, kile walichokiita "hatua ya kusitisha mapigano, ili
kujitayarisha kwa mjadala wa dunia juu ya Syria, bila kuingiliwa na
ushawishi wa mataifa ya nje".
"Mjadala wa aina hiyo ndio njia pekee ya kutoka katika mzozo huo", wizara hiyo imesema.
Muallem pia amelalamika kwa Brahimi juu ya mataifa ya eneo hilo ambayo
Syria inayashutumu kwa kuwahifadhi, kuwapa silaha na kuwapa mafunzo
waasi, akisema kuwa vitendo vyao vinaathiri ujumbe wa mjumbe huyo wa
amani wa umoja wa mataifa ya mataifa ya Kiarabu, Arab League.
Uturuki na Saudia zalaumiwa.
Syria imeilaumu mara kwa mara nchi jirani ya Uturuki pamoja na nchi
yenye utajiri mkubwa wa mafuta ya Saudi Arabia na Qatar kwa kuunga mkono
wapiganaji waasi.
Brahimi ana matumaini ya kupata usitishaji wa mapigano wakati wa sikukuu
ya Waislamu ya Eid al-Adha, inayoanza Oktoba 26, akiamini kuwa hiyo
inaweza kusafisha njia ya hatua za muda mrefu za amani.
Hassan Abdel Azim kutoka taasisi ya uratibu wa kitaifa kwa ajili ya
mabadiliko ya kidemokrasia nchini Syria , kundi la upinzani
linalovumiliwa na utawala wa nchi hiyo , ameunga mkono pendekezo hilo la
kusitisha mapigano.
Kiongozi wa upinzani nchini Syria Hassan Abdel-Azim.
Usitishaji kama huo wa mapigano unaweza kusafisha njia kwa ajili ya
hatua za kisiasa , iwapo utapanuliwa kujumuisha kuachiwa huru kwa
wafungwa ambao wamekamatwa na utawala wa nchi hiyo pamoja na usambazaji
wa msaada wa madawa kwa raia walioathirika, amesema.
"Ghasia nchini
Syria zimefikia katika kiwango cha kutisha ambacho kinatishia usalama na
uhuru nchi hiyo", Abdel Azim ameongeza baada ya kukutana na Brahimi.
Nayo makundi ya upinzani
Ukichukua msimamo mkali zaidi , makundi ya upinzani ambayo yako nje ya
nchi hiyo yanasema utawala wa Syria ni lazima uchukue hatua ya mwanzo na
kusitisha mashambulio yake ya kila siku.
Brahimi anatarajiwa kuwa na mazungumzo na Assad baadaye leo (21.10.2012)
katika juhudi za ujumbe wake mjini Damascus kuleta amani.
Mjumbe huyo amefanya ziara katika mataifa kadha ambayo yana ushawishi
katika mzozo huu wa Syria katika muda wa wiki moja iliyopita, ikiwa ni
pamoja na ziara nchini Lebanon na Iran, na kuonya kuwa ghasia zinaweza
kusambaa na kuliwasha moto katika eneo lote.

0 comments:
Post a Comment