Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli
UTEKELEZAJI wa zoezi la kukamata watumishi wa Serikali wanaotumia namba za kiraia kwenye magari ya umma kinyume cha sheria na utaratibu, unasuasua kutokana na kuwapo kwa taarifa za kutatanisha kuhusu kufanyika kwa kazi hiyo.
Taarifa zilizopatikana zinaeleza kuwa tangu Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli atangaze kufanyika kwa zoezi hilo akishirikiana na polisi, baadhi ya maofisa wa Serikali walibadilisha namba kimyakimya bila kutolewa taarifa yoyote.
Chanzo chetu cha habari kutoka Wizara ya Ujenzi, kimeeleza kuwa katika kazi hiyo, Dk Magufuli alitaka liwe linatangazwa na kufanyika mara moja.
Kilisema, badala yake inafanyika kwa siri na hakuna taarifa zinazotolewa waziwazi juu ya utekelezaji.
“Sijui nini kimetokea, tunaona zoezi liko kimya taarifa hazieleweki, tulisikia kuwa taarifa kuhusu zoezi hilo lilikuwa limeandaliwa na wizara, lakini mpaka sasa haijatolewa na hakuna kitu kinaendelea, nadhani kutakuwa kuna kitu kimetokea,”kilisema chanzo hicho
na kuongeza:
“Kila mtu wizarani ukimuuliza kuhusu zoezi hilo haelewi kinachoendelea.”
Lakini taarifa zilizopatikana kutoka vyanzo vingine vya habari zilieleza kuwa karibu magari 400 yamejiandikisha kupata namba za Serikali tangu zoezi la kakamatwa litangazwe.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Jerryson Lwenge alipoulizwa juu ya zoezi hilo alisema kuwa atafutwe naibu katibu mkuu wa wizara hiyo, John Ndunguru kwa kuwa ndiye anashikilia ofisi ya katibu mkuu kwa sasa.
“Sisi tupo Kenya kwenye mambo ya Afrika Mashariki mtafute naibu katibu mkuu ndiye anayeweza kukupa taarifa,” alisema Lwenge.
Hivi karibuni, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, John Ndunguru alivieleza vyombo vya habari kwamba Serikali iliweka utaratibu unaozuia matumizi ya namba za kiraia kwenye magari yake isipokuwa kwa kibali maalumu.
Alisema kuwa hali ya kuzuia namba hizo iliibuka baada ya kubainika kwamba kupitia namba hizo, magari ya umma yanatumika vibaya na baadhi kupotea.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohammed Mpinga alisema Waziri alitarajiwa kutoa ripoti jinsi zoezi hilo linavyoendelea kwa kuwa Waziri mwenyewe ndiye anatakiwa kuzungumzia suala hilo.
Alisema zoezi la ukamataji magari linaendelea kwa muda wa miezi mitatu mfululizo lakini hakusema idadi ya magari yaliyokamatwa hadi hivi sasa.
0 comments:
Post a Comment