ALIYEKUWA Waziri wa Fedha, Basil Mramba ameiambia Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu mji Dar es Salaam, kuwa hakukurupuka kuipatia Kampuni ya
Alex Stewart mkataba, bali ni uamuzi wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa.
Mramba
alidai hayo jana alipokuwa akihojiwa na Wakili wa Serikali Mkuu,
Fredrick Manyanda kutokana na ushahidi wake aliotoa mahakamani kuhusu
tuhuma za kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo na kuisababishia
Serikali hasara ya Sh bilioni 11.7.
“Zoezi la kumpata mkaguzi wa dhahabu, Alex Stewart halikuhitaji pupa wala kufanywa kwa pupa, Rais Mkapa aliagiza utekelezaji ufanyike haraka na kuzitaka Benki Kuu Tanzania (BoT) na Wizara ya Fedha zitafute njia za kupata fedha za kuilipa kampuni hiyo ili ianze kazi.
“Kuna mambo ya msingi tulikubaliana, miongoni mwa hayo ni umuhimu wa
kukagua madini, BoT isimamie kupata mkaguzi anayefaa kwa utaratibu wa
zabuni, gharama zilipwe na Serikali na si kampuni za madini kwa sababu
tungetaka walipie, lazima tungebadili mikataba iliyokuwepo,” alidai
Mramba.
Alidai hawakufanya pupa, kwani aliweza kumshauri
aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona kuangalia na nchi
nyingine wanafanyaje na kumweleza kwamba, akikubaliana na ushauri huo
waendelee.
“Sikumwagiza Yona, bali nilimshauri hakuna waziri
mwenye kumwagiza waziri mwenzake, kwa sababu wote wana hadhi sawa,”
alidai Mramba na kumsisitizia Manyanda kuwa katika barua yake ya Aprili
28,2002 kaeleza zaidi ya mara mbili kwamba anamshauri.
Mramba,
alikubaliana na wakili Manyanda kwamba waziri ndiye msimamizi wa sera
katika wizara anayohusika nayo na kwamba, watendaji wanasimamiwa katika
utekelezaji na katibu mkuu wa wizara.
Kesi hiyo, inasikilizwa na jopo la mahakimu, John Mtemwa, Saul Kinemela na Sam Rumanyika.
Mramba,
aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona na aliyekuwa Katibu
Mkuu, Wizaya ya Fedha, Grey Mgonja wanadaiwa kutumia madaraka vibaya kwa
kutoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya Alex Stewart, nakuisababishia
Serikali hasara ya Sh bilioni 11.7.
CHANZO GAZETI LA MTANZANIA.
0 comments:
Post a Comment