
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Njombe, Alfred Maluma akifanya ibada hivi karibuni.
ASKOFU wa Kanisa Katoliki Jimbo la Njombe, Alfred Maluma amewataka Watanzania kutokubaliana na hatua ya mataifa ya Magharibi yanayozitaka nchi za Afrika ikiwamo Tanzania kuruhusu ndoa za jinsia moja.
Akihubiri hivi karibuni kwenye kilele cha maadhimisho ya Jublie ya miaka 27 tangu kuanzisha kwa jumuyia ya wanandoa Kanisa Katoliki nchini, Askofu Maluma aliwataka Wakristo wote na Watanzania kukemea kwa nguvu zote suala hilo, kwa kuwa ndoa ya jinsia moja siyo haki wala mpango wa Mungu.
Alisema ndoa ni jambo takatifu na kwamba, anashangazwa na watu wanaoamua kupotosha maana yake kwa kuruhusu ndoa za jinsia moja, suala ambalo ni kinyume na maadili na matakwa ya mpango wa Mungu.
Aliongeza kuwa Mungu alimuumba Adamu kisha akamuumbia Eva, ili waishi pamoja na kuanzisha familia.
Alisema hata wanyama ambao hawakupewa uwezo wa akili hawajamiani kinyume na maumbile, lakini binadamu ambao wamepewa utambuzi ili waitawale dunia wamekuwa wakioana jinsia moja na kufanya tendo la ndoa kinyume na maumbile.
“Hata ng’ombe ambao Mungu hakuwajalia akili kama binadamu, hawaingiliani kinyume cha maumbile, iweje binadamu wenye akili timamu waoane jinsia moja,” alihoji Askofu Maluma.
Alisema familia ni kitu cha msingi katika maisha ya binadamu na kwamba, hata familia ya kanisa imetajirishwa na tunu za familia zenye kuishi kwa amani, upendo, mshikamano na kufuata mila na desturi zilizo bora.
Pia, Askofu Maluma alitumia fursa hiyo kuwaasa wazazi na walezi kuacha tabia ya kuwapeleka watoto wadogo, shule za bweni hasa chekechea na msingi, kwa sababu wanakosa malezi bora ya wazazi.
Pia, alitaka kuwapo na uhusiano mzuri kati ya walimu na wazazi katika malezi ya watoto, ili kwa pamoja wajenge nafsi ya mtoto kufuata madili mema.
Alisema mambo ya utandawazi yameifanya jamii kusahau mila na desturi zao, kwa kuiga mambo yasiyokuwa na maadili, ambayo yanapelekea taifa kuwa na kizazi cha ovyo.

0 comments:
Post a Comment