
BARAZA la Usalama la Umoja wa Mataifa limewawekea vikwazo waasi
wa M23 wa Kongo DRC baada ya waasi hao kudhibiti mji wa Goma ambao ni
makao makuu ya mkoa wa Kivu Kaskazini hapo jana.
Msemaji wa Umoja wa
Mataifa amesema, viongozi wa waasi wa M23 wanawekewa vikwazo kwa mujibu
wa azimio la Umoja wa Mataifa na kutaka kukomeshwa uungaji mkono wa nchi
za nje kwa waasi hao.
Hayo yanajiri huku waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda na
Uganda wakitangaza kwamba wana mpango wa kukomboa nchi nzima ya Kongo
DRC baada ya kudhibiti mji wa Goma. Vilevile maelfu ya askari na polisi
wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameasi serikali na kujiunga na
waasi wa M23 katika mji wa Goma.
Taarifa zinasema kuwa askari hao
waliojiunga na jeshi hawakuwa na khiyari baada ya waasi hao
kuwalazimisha kujiunga na kundi hilo na kuwataka ima kubakia kwenye mji
huo au kuondoka.
Msemaji wa waasi hao amesema kuwa, kundi hilo lina
mpango wa kudhibiti nchi nzima ya Kongo kwa kuanza kuelekea katika mji
wa Bukavu hadi katika mji mkuu Kinshasa, ulioko umbali wa kilometa 1,600
kutoka Goma.

0 comments:
Post a Comment