
NDEGE za kivita za nchi ya Israel zimeshambulia majengo ya serikali ya chama cha Hamas
huko Gaza ikiwemo ofisi ya waziri mkuu baada ya baraza la mawaziri la
Israel kuidhinisha kuitwa kwa wanajeshi wa akiba 75,000 kuvamia Gaza.
Ndege hizo za Israel zimeshambulia wizara ya ulinzi na jengo la ofisi ya
Waziri Mkuu Ismail Haniyeh ambapo hapo Ijumaa alikutana na Waziri Mkuu
wa Misri.
Kwa siku kadhaa miripuko mizito imekuwa ikilitingisha eneo la
Gaza linalokaliwa na idadi kubwa ya watu na kusababisha kufuka kwa moshi
mzito angani.
Waziri Mkuu wa Hamas, Ismail Hania.
Hamas yaendelea kurusha maroketi
Wanamgambo wa itikadi kali za Kiislamu nao wamekuwa wakiendelea
kuvurumiosha maroketi nchini Israel.
Licha ya machafuko hayo,waziri wa
mambo ya nje wa Tunisia amewasili Gaza leo hii kuonyesha.
mshikamanona na Wapalestina na kushutumu mashambulizi hayo ya Israel
kuwa sio halali na yasiokubalika.
Maafisa huko Gaza wanasema Wapalestina
41 wakiwemo raia 20 watoto wanane na mwanamke mmoja mjamzito wameuwawa
katika huko Gaza tokea Israel ilipoanza operesheni zake siku nne
zilizopita.
Raia watatu wa Israel wameuwawa na shambulio la roketi hapo
Alhamisi.
Jeshi la Israel limesema kikosi chake cha anga kimeshambulia takriban
maeneo 180 waliokuwa wameyalenga jana usiku ikiwa ni pamoja na makao
makuu ya polisi majengo ya serikali,vikosi vya kurusha maroketi na kituo
cha mafunzo cha Hamas katika Ukanda huo wa Gaza uliozongwa na
umaskini.
Jengo la ghorofa tatu la afisa wa Hamas Abu Hassan Salah pia
lilishambuliwa na kuharibiwa kabisa mapema leo alfajiri.
Waokoaji
wamesema takriban watu 30 wametolewa kwenye kifusi cha jengo hilo.
Waziri wa mambo ya nje wa Tunisia Rafik Abdelsslem amesema kile
inachokifanya Israel sio halali na hakikubaliki.
Wakati akitembelea makao
makuu ya Haniyeh yalioharibiwa amesema nchi hiyo haina kinga ya
kujifanyia mambo inavyotaka bila ya kuchukuliwa hatua na kwamba haiko
juu ya sheria.
Israel ilianzisha mashambulizi mazito ya anga hapo
Jumatano kwa lengo la kuwazuwiya Hamas kuvurumisha maroketi
kunakoliandama eneo la kusini mwa Israel kwa miaka kadhaa sasa.
Wapalestina wamevurumisha mamia ya maroketi kutoka Gaza ambapo moja
limeshambulia mji wa Jerusalem na matatu yameshambulia mji mkuu wa
kibiashara wa Tel Aviv.
Jerusalem ilikuwa haikuwahi kulengwa kwa njia
hiyo tokea mwaka 1970 na Tel Aviv tokea mwaka 1991.
Juu ya kwamba kumekuwa hakuna repoti za maafa na uharibifu kwa miji hiyo
mashambulizi hayo ya maroketi ya masafa marefu yamesababisha fadhaa na
kuzusha uwezekano wa Israel kuvamia Ukanda wa Gaza kwa kutumia vikosi
vyake vya nchi kavu.
Waziri wa mambo ya nje wa Israel Avigdor Lieberman
amekiambia kituo cha televisheni cha Israel cha Channel One kwamba
mashambulizi hayo yataendelea kwa kadri yatakavyohitajika na kwamba
hawajajiwekea kikomo kwa uwezo wao au kwa wakati.
Hamas imejizatiti kuendelea kupambana na Israel na imesema shauku yake
ya kufanya hivyo imezidi kuwa kubwa.
Kundi hilo la Waislamu wa itikadi
kali la Hamas limekuwa likiutawala Ukanda wa Gaza tokea mwaka
2007.
Israel iliwahamisha walowezi wake wa Kiyahudi kutoka Gaza hapo
mwaka 2005 lakini imeendelea kulizingira eneo hilo kwa vikwazo.
Benjamin Netanyahu.
Israel yumkini kuvamia Gaza
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekuwa na mkutano wa kupanga
mikakati wa saa nne hapo Ijumaa na mawaziri kadhaa waandamizi kujadili
kutanuwa mashambulizi yao ya kijeshi.
Duru za kisiasa zinasema baraza hilo limeamuwa kuongeza zaidi ya
maradufu fungu la hivi sasa la wanajeshi wa akiba kwa ajili ya uvamizi
wa Gaza hadi kufikia 75,000.Hata hivyo haimaanishi kwamba wanajeshi hao
wote wataitwa.
Waziri Mkuu wa Misri Hisham Kandil alifanya ziara huko Gaza iliopigiwa
debe hapo Ijumaa na kushutumu kile alichokielezea kuwa ni uchokozi wa
Israel na kusema kwamba serikali ya Misri iko tayari kusuluhisha
usitishaji wa mapigano.
Serikali ya itikadi kali za Kiislamu nchini Misri
ilioshika madaraka baada ya uchaguzi huru kufuatia uasi uliomn'gowa
madarakani dikteta mkongwe Hosni Mubarak ni mshirika wa Hamas lakini pia
ni mshirika wa mkataba wa amani na Israel wa mwaka 1979.
Katika ishara nyengine kwamba Netanyahu huenda akawa anajitayarisha kwa
uvamizi wa Gaza vikosi vya Israel vimeamuru kufungwa kwa barabara kuu
inayoelekea Gaza na barabara nyengine mbili zinazopakana na Ukanda wa
Gaza kwa matumizi ya magari ya kiraia.
Takriban Wapalestina milioni moja na laki saba wanaishi katika Ukanda wa Gaza.

0 comments:
Post a Comment