
AKIFUNGUA mkutano mkuu wa nane wa CCM mjini Dodoma hivi karibuni, Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete amesema mpasuko uliomo ndani ya chama hicho unatokana na makundi yanayotaka uongozi wa juu, ukimwamo urais mwaka 2015.
Hata hivyo, Rais Kikwete amejitenga na makundi hayo huku akiwataka wale wanaomtaka awaunge mkono wamwache.
Kwanza nampongeza Rais Kikwete walau kwa kuwa wazi juu ya jambo muhimu linalokisumbua chama chake, lakini namshauri ‘afunguke’ zaidi.
Rais Kikwete amekuwa wazi kwa masuala ya msingi yanayokisumbua chama hicho tangu chaguzi zake zilipoanza. Alikuwa akitaja tatizo la rushwa na kuwataka wanachama kujiepusha nayo, japo ameonyesha udhaifu wa kuidhibiti rushwa hiyo.
Mimi ningependa tu kumbumbusha Rais Kikwete kwamba makundi hayo anayoyalalamikia, hata yeye yanamhusu,s tena yeye ndiyo aliyeyaasisi, vipi leo ayakane ?.
Hata mbuyu ulianza kama mchicha, na sasa inakuwa kazi ngumu kuukata, yanabaki maneno tu. Ndiyo Rais Kikwete alipoifikisha hapo CCM.
Itakumbukwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 ambao ulihusisha vyama vingi baada ya muda mrefu wa chama kimoja, Rais Kikwete alikuwa na mtandao wake huku akimhusisha mtu wake wa karibu, Edward Lowassa, wakati huo wakiwa na jina la utani la ‘Boys II Men’.
Kundi hilo lililohusisha vigogo kadhaa wa chama na wafanyabiashara, lilikuwa limesukwa kikamilifu kwa lengo la kuchukua madaraka mwaka 1995, huku likijinasibisha na ujana katika uongozi.
Lakini wakati ule alikuwepo Mwalimu Julius Nyerere na aliusoma mchezo mzima, akaona CCM itaingia mkenge, akalikataa kundi hilo.
Alionyesha kulikataa hata pale Rais Kikwete aliposhinda katika kinyang’anyiro cha kumpata mgombea urais kwa tiketi ya CCM, lakini uchaguzi ukarudiwa na Benjamin Mkapa akashinda.
Mwalimu alionyesha mapenzi yake kwa Mkapa kiasi cha kuzunguka nchi nzima kumpigia debe.
Inawezekana wala Mwalimu hakuwa na mapenzi ya dhati na Mkapa, lakini alifanya hivyo ili kuepusha dhahma.
Heri lawama kuliko fedheha.
Hata hivyo, kundi hilo liliendelea kusukwa chini kwa chini, hata baada ya kifo cha Mwalimu Nyerere, ndiyo kabisa likaendelea kuchanua katika vipindi vyote viwili vya urais wa Mkapa.
Siyo kwamba hakukuwa na makundi mengine, yalikuwepo lakini hili la kina Kikwete lilikuwa na nguvu na lilikuwa tishio.
Ndiyo maana ilipofika mwaka 2005, ilikuwa piga, ua, garagaza urais lazima agombee Kikwete na akaupata tena kwa ushindi wa ‘Tsunami’.
Ili kuonyesha uswahiba wao una nguvu, Kikwete akampa Lowassa uwaziri mkuu.
Lakini kama wanavyosema waswahili, ‘ngoma ikivuma sana hupasuka’, kabla hata Lowassa hajafaidi utamu wa akashikwa na mtego wa Richmond bungeni.
Jamaa walimng’ang’ania hadi akautema uwaziri mkuu, jambo lililomsikitisha sana Rais Kikwete.
Siku alipokuwa akiunda upya Baraza la Mawaziri, alisikika akisema, “Yaliyompata Lowassa ni ajali ya kisiasa”.
Eti mtu ametuhumiwa kwa ufisadi, Rais badala ya kuchukua hatua zaidi ya hapo, anasikitika !.
Lowassa naye amekuwa akijitapa huku na huko kuwa urafiki wake na Rais Kikwete siyo wa kukutana barabarani. Maana yake ni kwamba wao ni watu walioshibana.
Rais Kikwete naye amekuwa akimwagia sifa Lowassa kila anapopata nafasi. Kwa mfano kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Rais alitinga jimboni Monduli na kumwagia sifa Lowassa. Hivi karibuni pia akiwa jijini Arusha alisema Lowassa ni ‘jembe’.
Huo wote ni ushahidi kuwa watu hawa ni marafiki wakubwa na hawatupani.
Kutokana na makundi hayo, hata utendaji wa Rais Kikwete katika kutekeleza ahadi zake kwa wananchi umekuwa dhaifu, maana huwezi kutumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja.
Huwezi kutumikia makundi na wananchi kwa wakati mmoja.
Huwezi kupambana na rushwa wakati baadhi ya watuhumiwa ni wa kundi lako.
Sasa katika makundi yanayotajwa kuwania urais mwaka 2015 ndani ya CCM, Lowassa naye anatajwa na wala hajawahi kukanusha.
Nguvu zake zimejidhihirisha katika chaguzi za ndani za CCM mwaka huu akidaiwa kupenyeza mikono yake kila idara ya chama hicho ilimradi tu apitishwe mwaka 2015.
Kwa hali hii Rais Kikwete anaweza kuliruka kundi la Lowassa? Eti Rais anasema hausiki na kundi lolote !
Inawezekana ni kwa sababu yeye ni kiongozi na inabidi akemee maovu ndani ya chama, lakini kwa mlango wa nyuma wako pamoja. Si tunasikia kauli zake kila mara ?.
Ni vigumu mno kwa Rais Kikwete kuyakana makundi hayo, labda tu kama hataki ijulikane au iwe wazi.
Isitoshe, Kikwete kwa sasa anamaliza muda wake hivyo makundi hayo kwake hayana tija kubwa, ndiyo maana anayaponda huku akiwa amesahau kuwa ndiyo yaliyomfikisha hapo alipo.
Vinginevyo Rais Kikwete awe wazi tu kwa mtu anayempenda. Mbona Rais mstaafu wa Kenya alipomaliza muda wake alionyesha mapenzi yake kwa Uhuru Kenyatta? Mbona Nyerere alimpigia debe wazi wazi Mkapa? Inawezekana pia kwa Kikwete.
Elias Msuya ni mwandishi wa makala wa gazeti la Mwananchi; 0754 897 287.

0 comments:
Post a Comment