BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

POLISI ADAIWA KUMLAZIMISHA MAJERUHI AKUMBATIE MAITI KATIKA OPERESHENI YA KUONDOA WAFUGAJI KILOMBERO


Jeneza lenye mwili wa marehemu, Dasu Litaligula (22) ukitolewa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya mt. Francis Ifakara kwa ajili ya mazishi katika kitongo cha Udagaji katika kata ya Chita baada ya kudaiwa kupoteza maisha kwa kupigwa na risasi na askari polisi wakati wa oparesheni ya kuondoa wafugaji inayoendelea katika hifadhi ya bonde la Kilombero kwa wilaya mbili za Ulanga na Kilombero tukio ambalo lililotokea Novemba 10 mwaka huu katika wilaya ya Kilombero mkoa wa Morogoro.
Jeraha la kidonda likiwa katika mguu wa kushoto wa majeruhi, Dase Litaligula (18) aliyedaiwa kupigwa risasi wakati wa tukio hilo na polisi.
Majeruhi Luhende Lutaligula (25) kushoto Dase Litaligula (18) kulia wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kudaiwa kujeruhiwa kwa kupigwa na risasi na mmoja kufariki dunia kwa tukio hilo na askari polisi wilayani Kilombero.

MAJERUHI aliyejeruhiwa katika oparesheni ya kuondoa wafugaji inayoendelea katika hifadhi ya bonde la Kilombero  Luhende Lutaligula (25) amesema polisi walimlazimisha kuukumbatia mwili wa marehemu ndugu yake wakati wakisafirishwa kutoka katika eneo la tukio kitongoji cha Udagaji katika kata ya Chita wilayani Kilombero kwa ajili ya kuuhifadhi mwili huo  katika hospitali ya mt. Francis iliyopo Ifakara yalipo makao makuu ya wilaya hiyo.

Akizungumza na  waandishi wa habari Lutaligula alisema kuwa baada ya ndugu yake kupigwa risasi katika eneo la makalio  na kufariki dunia,polisi hao walimlazimisha kuukumbatia  mwili wa marehemu Dasu Lutaligula (22) jambo ambalo alitekeleza huku wakikataa kutii amri ya kuulamba na kuurudisha utumbo wa marehemu kwa mdomo kama alivyotakiwa na askari hao.

Amesema  kuwa tukio hilo lilitokea wakati yeye na mwili wa marehemu ambaye ni mjukuu wake kiukoo  wakisafirishwa kutoka eneo la tukio kwenda hospitali ya St. Francis Ifakara kwa ajili ya kuuhifadhi mwili huo na yeye kupatiwa matibabu aliyopata kutokana na kujeruhiwa kwa risasi katika mkono wake wa kulia na kujeruhiwa kwa kitako cha bunduki kichwani.

Akifafanua zaidi kuhusiana na tukio hilo, majeruhi huyo amesema kuwa wakiwa marishoni walishangaa kuvamiwa na kundi la askari ambao walikamata ng’ombe wao wapatao 78 na kuwapeleka katika kambi hiyo kwa madai kuwa walikuwa wakitakiwa kuhama kwa kuwa walikuwa wakichungia katika eneo la hifadhi jambo ambalo halikuwa sahihi na walipobisha kwa kutaka ufafanuzi zaidi ndipo wakaanza kushambuliwa kwa risasi.

Naye kaka mkubwa wa marehemu huyo Ishirini Lutaligula (36) alisema kuwa familia yao inatarajia kulishataki jeshi la polisi mahakamani  kwa mauaji ya ndugu yao na wengine kujeruhiwa kwa kuwa nguvu iliyotumika ni kubwa sana ikilinganisha na idadi ndogo ya watuhumiwa ambao  walikuwa na uwezo wa kuwadhibiti pasipo kutumia risasi za moto.

Akizungumzia tukio hilo Katibu wa Umoja wa Wafugaji wilaya ya Kilombero, Patrick Malisha amesema umoja huo utaungana na familia ya marehemu katika kuhakikisha haki inatendeka ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani kwa askari aliyehusika na mauaji hayo.

Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile akizungumza na gazeti hili alisema kuwa nguvu iliyotumika kuzuia vurugu zilizoanzishwa na marehemu, Dasu Lutaligula na nduguze, zilikuwa za kawaida ambapo ameahidi kufanya uchunguzi juu ya tukio hilo ikiwemo na vitendo vingine vya askari wake kukiuka haki za binaadamu ndani ya jeshi hilo mkoani hapa.

Hili ni tukio la pili kutokea toka kuanzishwa kwa harakati za kuwaondoa wafugaji katika bonde la kilombero, katika tukio la awali wakulima watano waliuawa ,mwezi march mwaka huu wilayani Ulanga wakidaiwa kutaka kuwavamia askari waliokuwa wakiwazuia kufanya shughuli za kilimo katika eneo la bonde la kilombero.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: