HATIMAYE marais wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC), wamezindua jengo la makao makuu ya umoja huo lililogharimu Euro
milioni 14, ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 28.
Jengo hilo limejengwa jirani na Kituo cha Mikutano cha Kimataifa
cha Arusha (AICC), likiwa na majengo matano yanayowakilisha nchi
wanachama.
Jumuiya ya Afrika Mashariki inayokadiriwa kuwa na watu
zaidi ya milioni 127, inaundwa na nchi za Uganda, Kenya, Rwanda,
Burundi na Tanzania.
Akizungumza jana katika uzinduzi huo Rais wa
Kenya, Mwai Kibaki ambaye pia ndiye mwenyekiti wa jumuiya hiyo
aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kutoa eneo la ujenzi.
Alisema
juhudi zilizofanywa na Rais Jakaya Kikwete, zinapaswa kuigwa kwa
viongozi wa Afrika Mashariki kutokana kuwa msukumo wa kuimarisha jumuiya
hiyo kila nyanja.
Viongozi wengine waliohudhuria sherehe hizo ni
Rais Kikwete, Rais Piere Nkurunzinza (Burundi), huku Rais Yoweri
Museveni (Uganda) na Rais Paul Kagame (Rwanda) wao walituma wawakilishi.
“Ukarimu
wa Rais Kikwete kutoa eneo hili pamoja na eneo jingine kule wilayani
Arumeru Kisongo, ni wa kipekee katika Jumuiya yetu hii,” alisema Rais
Kibaki.
Katika salamu zake hizo, Rais Kibaki pia alitumia fursa
hiyo kuishukuru Serikali ya Ujerumani, kwa kutoa msaada usio na masharti
kwa ajili ya ujenzi huo.
Rais Kibaki aliendelea kubainisha
kwamba, kuwapo majengo hayo sasa kutafanya Jumuiya hiyo iendelee
kuimarika katika shughuli zake za kila siku.
Awali Rais Kikwete
aliwaeleza wabunge wa jumuiya hiyo kuwa, wanawajibu wa kutoa sauti zao
kwa nchi wanachama, ili ziweze kuimarisha masuala ya miundombinu.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo wakati akifungua Bunge la jumuia hiyo, ambalo ukumbi wake umo ndani ya jengo hilo.
Alisema
endapo miundombinu ikiimarishwa kwa nchi wanachama, ni wazi kuwa
ufanyaji wa biashara mbalimbali utaongezeka na kupiga hatua za kiuchumi.
0 comments:
Post a Comment